Sambamba na kuanza rasmi kazi yake, Rais mpya wa Gambia ametekeleza hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa nchi hiyo.
Katika fremu hiyo Rais Adama Barrow ameamuru kutiwa mbaroni
kamanda wa zamani wa idara ya usalama wa taifa ya Gambia. Yankuba
Badjie, aliyeongoza idara ya usalama wa taifa ya Gambia katika kipindi
cha rais wa zamani wa nchi hiyo Yahya Jammeh, na aliyeogopewa sana,
ametiwa mbaroni na polisi kwa ajili ya kuhojiwa. Itafahamika kuwa, idara
ya usalama wa taifa ya nchi hiyo kilikuwa chombo cha utesaji cha rais
huyo wa zamani. Malalamiko ya kutaka kuachiliwa huru shakhsia wa kisiasa
na kutoheshimiwa haki za binaadamu, ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa
yakilalamikiwa sana na wapinzani wa Gambia na hata asasi za kimataifa
katika uwanja huo.
Yahya Jammeh aliyetawala Gambia kwa miaka 22, anatuhumiwa
kuwakandamiza wapizani na kutumia utesaji na ukatili wa kutisha dhidi ya
waandamanaji na wanasiasa waliokuwa wakimkosoa. Suala hilo lilishika
kasi hasa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa rais uliopita,
ambapo akthari ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa na wapinzani
dhidi ya serikali walitiwa mbaroni nchini. Hata baadhi ya weledi wa
mambo waliutaja ushindi wa Adama Barrow kuwa uliotokana na natija ya
vitendo hivyo vya serikali iliyopita. Kwa kuwa na idara ya usalama wa
taifa yenye nguvu, Jammeh aliweza kuwakandamiza wapinzani na
waandamanaji nchini Gambia ambapo alizuia kila aina ya maandamano na
mikusanyiko ya wapinzani. Siku chache zilizopita, naibu mkuu wa shirika
la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch anayeshughulikia
masuala ya mipango ya shirika hilo alitoa ripoti iliyoeleza kwamba,
serikali ya Jammeh ilikuwa ikitumia vitisho na utesaji dhidi ya viongozi
wa vyama vya upinzani na kuwanyima haki zao za msingi.
Kiasi kwamba wahisani wa kimataifa walitaka kuwekewa vikwazo viongozi
wa serikali ya Gambia kutokana na mienendo yao hiyo. Hivi sasa raia wa
nchihiyo na ikiwa ni baada ya miezi kadhaa tangu kujiri mgogoro wa baada
ya uchaguzi wa tarehe Mosi Disemba mwaka jana, wanataraji kuona
mabadiliko katika utendajikazi wa Rais Barrow. Miongoni mwa ahadi
alizozitoa Adama Barrow katika kampeni za uchaguzi ni pamoja na
kuheshimu haki za raia na kuanzisha anga ya uhuru wa kisiasa nchini
humo. Kadhalika rais huyo mpya aliahidi kufanya marekebisho katika idara
ya usalama nchini. Inaonekana kuwa katika hatua ya awali ya ahadi zake
ameilenga idara ya usalama ili kwa njia hiyo awe ametekeleza moja ya
ahadi hizo na wakati huo huo kudhibiti usalama wa ndani ya nchi kwa
ajili ya kukabiliana na kila aina ya ukwamishaji mambo na mapinduzi ya
kijeshi kutoka kwa askari wanaomuunga mkono Yahya Jammeh.
Katika fremu hiyo, Rais Barrow amebadili jina la idara ya usalama wa
taifa na kuwa 'Idara ya usalama wa nchi.' Hata kama Jammeh ameondoka
nchini Gambia, lakini bado kuna askari wengi wanaomuunga mkono kiongozi
huyo wa zamani wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Barrow
anayehesabika kuwa mfanyabiashara mashuhuri wa Gambia, aliahidi pia
kwamba ataboresha hali ya uchumi, kuanzisha fursa za kazi na kuvutia
wawekezaji nchini. Hii ni kwa kuwa katika kipindi cha utawala wa Jammeh,
uchumi wa Gambia uliporomoka kutokana na siasa zake mbovu, hali ambayo
ilisababisha pia kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Hivi sasa Wagambia wana matumaini kwamba kipindi hiki cha utawala mpya
kitafungua anga mpya ya kisiasa na kuboresha hali ya kisiasa nchini
humo.
No comments:
Post a Comment