Wizara ya Ulinzi ya Tunisia imetangaza kuwa,
magaidi wawili wakufurishaji wameangamizwa katika maeneo ya milimani ya
jimbo la Kasserine la magharibi mwa nchi hiyo katika operesheni maalumu
ya jeshi ya kupambana na magenge ya kigaidi.
Televisheni ya Sky News imeinukuu
Wizara ya Ulinzi ya Tunisia ikitangaza habari hiyo jana na kuongeza
kuwa, jeshi la nchi hiyo limepambana na magaidi katika milima ya al
Samamah ya jimbo la Kasserine, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria
na kufanikiwa kuangamiza magaidi wawili na kuwatia mbaroni magaidi
wengine kadhaa.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Tunisia
imetangaza pia habari ya kutekwa idadi kubwa ya silaha kutoka kwa
magaidi hao, kwenye operesheni hiyo.
Eneo hilo la mpakani mwa Tunisia na
Algeria linatumiwa sana na magaidi wakufurishaji kufanya mashambulizi
ndani ya nchi hizo mbili.
Wakati huo huo, viongozi wa serikali ya
Tunisia, siku ya Alkhamisi waliongeza muda wa hali ya hatari nchini humo
kwa miezi mitatu zaidi kuanzisha tarehe 16 Februari.
Magenge ya kigaidi yameongeza harakati
zao nchini Tunisia tangu mwaka 2011 baada ya kutokea mapinduzi ya
wananchi yaliyoungóa madarakani utawala wa dikteta Ben Ali.
Hadi hivi sasa makumi ya watu wameshauawa wakiwemo wanajeshi, polisi, raia wa kawaida na watalii.
Viongozi wa Tunisia wameimarisha ulinzi
katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu mwaka 2015 baada ya kuuawa
askari 12 wa gadi ya Rais na pia shambulio la kikatili lililotokea mwaka
2016 karibu na mpaka wa nchi hiyo na Libya.
No comments:
Post a Comment