Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratejia cha
Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amesisitiza kuwa
vitisho vya rais mpya mwenye makelele wa Marekani haviwezi katu
kusitisha maendeleo ya kiulinzi ya Iran.
Ali Akbar Velayati aliyasema hayo jana katika mahojiano na
gazeti la Kifaransa la Le Monde na kanali ya televisheni ya France 24.
Dokta Velayati amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haivipi umuhimu
wowote na wala haishughulishwi na vitisho na vikwazo vinavyotangazwa na
serikali mpya ya Marekani dhidi yake na kuongeza kuwa Donald Trump
anaendelea kufuata njia na sera zilezile za marais waliopita wa Marekani
dhidi ya Iran.
Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha
Maslahi ya Mfumo wa Iran amefafanua kuwa tofauti pekee aliyonayo Trump
na marais wengine waliotangulia wa Marekani ni katika mbinu ya
utangazaji uadui wa Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na
kusisitiza kuwa wananchi wa Iran wana historia na ustaarabu mkubwa na
wamejiweka tayari kukabiliana na mashinikizo.
Akijibu suali la mwandishi wa habari wa kanali ya televisheni ya
France 24 kuhusu majaribio ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,
Velayati amesema, lengo la Iran la kufanya majaribio ya makombora ni kwa
ajili ya ulinzi tu na kwa msingi wa kuiramisha uwezo wake wa kujihami.
Kuhusiana na kadhia ya nyuklia, Mkuu wa kituo cha utafiti wa
kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran
amesema, kinyume na nchi nyingi ikiwemo Ufaransa ambayo haikusaini
Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT) mpaka
ilipokuwa imeshamiliki silaha za nyuklia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
haina nia ya kumiliki silaha hizo, kwa sababu kwa mujibu wa fatua ya
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, utumiaji wa silaha za aina hiyo ni
haramu.
Huku akiashiria kuwa Iran ni mwanachama wa NPT na kutumia nishati ya
nyuklia kwa malengo ya amani ni haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran, Dokta Veleyati amesisitiza kuwa sio tu Iran haina hatihati bali
iko imara na thabiti katika azma yake ya kutumia na kunufaika na
teknolojia ya nyuklia.../
No comments:
Post a Comment