Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amepata idhini ya
bunge kuanzisha mchakato wa kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya (EU), na
kuzima juhudi za kukwamisha mpango wake wa kuanzisha mazungumzo ya
kutengana kufikia Machi 31.
Wabunge waliidhinisha mpango wa waziri mkuu May kwa kura 494 dhidi ya
122, na hivyo kumpa mamlaka ya kuanzisha mchakato wa Brexit, na
kuhitimisha siku kadhaa za mjadala mkali.
Muswada huo sasa
unahitaji kuidhinishwa na baraza la mamwinyi la bunge la Uingereza
(House of Lords) kabla ya kuwa sheria, ambako theluthi mbili ya wabunge
walipiga kampeni dhidi ya Brexit, na ambako waziri mkuu hana wingi wa
wabunge.
Ushindi huo unaashiria hatua muhimu kuelekea kuanza kwa
kile kinachotarajiwa kuwa majadiliano magumu na marefu na Umoja wa Ulaya
kuhusu masuala kama vile biashara, uhamiaji na usalama ambavyo
vitabadili jukumu la Uingereza duniani.
Baada ya kunusurika uasi
mdogo ndani ya chama chake cha kihafidhina uliokuwa umetishia
kudhoofisha mamlaka yake na mkakati wa majadiliano, sheria hiyo ilipita
bila marekebisho yoyote na kwa wakati.
Bunge la wawakilishi likijadili muswada wa sheria ya Brexit 08.02.2017
Hilo
limeongeza matumaini kwamba muswada huo utapita pia kwa urahisi katika
baraza kuu la bunge la Uingereza lisilo la kuchaguliwa, wakati safari
yake itakapoanza huko Februari 20. Serikali inataka kukamilisha mchakato
wa kisheria kufikia Machi 7.
Ushirika wa kimkakati
Waziri
mkuu aliliambia bunge siku ya Jumatano kwamba wanaamini inawezakana
ndani ya kipindi cha miaka miwili kufikia makubaliano siyo tu kwa ajili
ya kujiondoa kwao, lakini pia ya kibiashara kuhakikisha wanaye ushirika
imara wa kimkakati huko mbeleni.
Duru zilizo karibu na
majadiliano katika baraza la juu la bunge zilisema wanatarajiwa
kuendelea kuishinikiza serikali kulihusisha zaidi bunge wakati wa
mchakato wote wa majadiliano.
Chama cha upinzani cha Labour na
chama kidogo cha Scottish National Party viliwasilisha marekebisho
vikitaka uthibitisho kuhusu ushiriki katika soko la pamoja, haki za
wafanyakazi na za raia wa Ulaya walioko Uingereza, lakini miswada hii
yote ilishindwa.
Chama cha Labour kiliwashurutisha wabunge wake
kutopinga sheria hiyo, lakini 52 kati ya wabunge wake 229 walikataa
kuunga mkono muswada huo, akiwemo Clive Lewis, msemaji wa kamati ya
biashara ya chama hicho aliejiuzulu papo kwa hapo.
Scotland huru haiwezi kuwa ndani ya EU
Wabunge
wa SNP walielezea kuvunjwa kwao moyo wakati wa kura hiyo ya Jumatano,
kwa kuimba wimbo wa Umoja wa Ulaya wa "Ode to Joy" uliotungwa na
Mjerumani Beethoven, kabla ya kunyamazishwa na naibu spika Lindsay
Hoyle.
Mbunge wa SNP Angus Robertson alimtuhumu May kwa kushindwa
kutumiza ahadi yake ya kuzihusisha Scotland, Wales na Iraland ya
Kaskazini katika mchakato huo. May aliahidi kufanya kazi kwa karibu na
mabunge yaliogatuliwa lakini alisema mahakama ya juu ya Uingereza
iliamua kuwa mabunge hayo hayana turufu juu ya makubaliano ya Brexit.
Waziri mkuu Theresa May akijibu maswali ya wabunge wakati mjadala kuhusu sheria ya Brexit.
"Muswada
unaopitia bungeni unaipa serikali mamlaka ya kuanzisha kipengele cha
50. Na pia ningependa kumkumbusha bwana Robertson juu ya nukta hii, kwa
sababu kila mara anazungumzia maslahi ya Scotland ndani ya Umoja wa
Ulaya. Scotland ilio huru haitakuwa ndani ya Umoja wa Ulaya," alisema
May.
UKIP washangilia
Lakini matokeo ya
kura hiyo yalishangiliwa na wapiganiaji wa Brexit kama vile Nigel
Farage, kiongozi wa zamani wa chama cha UK - Independence UKIP,
alieandika kwenye ukurasa wake wa twitter akisema. Sikuwahi kufikiria
nitaiona siku ambapo bunge la wawakilishi linapiga kura kwa wingi mkubwa
kuunga mkono Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
May
ameahidi kutoa kipaumbele kwa uhamiaji katika majadiliano ya Brexit,
hata kama hilo linakuja kwa gharama ya kuachia uanachama wa soko la
pamoja la Umoja wa Ulaya na wateja wake milioni 500.
No comments:
Post a Comment