Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amesisitiza kuwa, Marekani inatumia hila ya kurudia rudia vitisho vya
kuishambulia kijeshi Iran ili kuwatoa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu
katika uwanja wa vita vya kweli ambavyo ni vita vya kiuchumi.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali
Khamenei amesema hayo leo wakati alipoonana na maelfu ya wananchi wa
Azerbaijan (kaskazini magharibi mwa Iran) na kusema kuwa, kujitokeza kwa
wingi, kwa moyo mmoja na kwa hamasa kubwa wananchi wa Iran katika
matembezi ya Bahman 22 ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
ni jambo lililoyaletea fakhari kubwa mapinduzi hayo na mfumo wa Jamhuri
ya Kiislamu humu nchini.
Aidha amewashukuru wananchi wote wa Iran
kwa kuwaambia: Mwaka huu si vyombo vya habari vya ndani pekee
vilivyoripoti kushiriki kwa wingi sana wananchi wa Iran kwenye matembezi
hayo, bali hata maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu nao - tofauti na miaka
ya huko nyuma - mwaka huu wamekiri kuwa mamilioni ya wananchi wa Iran
wameshiriki kwenye maadhimisho hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ametoa uchambuzi kuhusu lengo hasa la serikali iliyopita na ya
hivi sasa ya Marekani la kutoa vitisho vya mara kwa mara vya
kuishambulia kijeshi Iran na kuongeza kuwa: Kama walivyofanya huko
nyuma, leo hii pia wanatoa matamshi hayo hayo ya kwamba chaguo la
mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran liko mezani. Na yule afisa wa
barani Ulaya naye aliyewaambia viongozi wa Iran kuwa, "kama si
makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, basi vita dhidi ya Iran lilikuwa ni
jambo lisiloepukika" lakini matamshi hayo ni uongo ulio wazi. Wanataka
kuzibabaisha akili zetu na kutufanya tusahau vita vya kweli, yaani vita
vya kiuchumi. Wanajaribu kuzivuta fikra zetu upande wa vita vya kijeshi
ili viongozi wa nchi yetu wasahau kuelekeza nguvu zao upande wa
maendeleo ya kiuchumi na vita vya kiutamaduni vya Wamagharibi dhidi ya
taifa la Iran.
Aidha ameashiria jinsi mashirika ya
kijasusi ya Marekani CIA na utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD pamoja
na mashirika ya kijasusi ya Uingereza na fedha za mafuta za watawala
"Maqarun" zinavyotumika kuandaa mazingira mabaya na kuendesha propaganda
chafu dhidi ya Mapinduzi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema:
Katika kipindi cha miaka yote hii, mamia ya kanali za televisheni na
mitandao ya kijamii ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu imekuwa ikifanya
njama za kuidunisha na kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata
hivyo kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika matembezi ya Bahman
22 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu huondoa vumbi lililopandikizwa na
maadui hao na kuyasafisha Mapinduzi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu pia amesema, maendeleo iliyopiga Iran kwenye kipindi cha miongo
minne iliyopita katika masuala ya miundombinu ni ya kustaajabisha.
Amesema: Baadhi ya maendeleo hayo kikawaida yasingeliweza kufikiwa hata
baada ya kupita miaka mia moja.
No comments:
Post a Comment