Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatahudhuria
dhifa ya chakula cha jioni inayoandaliwa na chama cha waandishi wa
habari wanaoripoti matukio ya Ikulu.
Tangazo la Trump linakuja siku moja baada ya kuwashutumu vikali
wanahabari kwa kuwataja kuwa ni adui wa watu kwa kudai wanaeneza taarifa
za uongo na za kupotosha. Kiongozi huyo mpya wa Marekani pia amewataja
wanahabari kuwa chama cha upinzani nchini Marekani. Dhifa hiyo
iliyoanzishwa mwaka 1921, huwa inahudhuriwa na watu mashuhuri, wanasiasa
wa Marekani na wanahabari.
Rais wa chama cha waandishi wa habari
wa Ikulu ya White House WHCA Jeff Mason amesema dhifa hiyo itaendelea
kama ilivyopangwa kwani ni desturi ya kusherehekea mchango muhimu
unaotekelezwa na mashirika ya habari katika taifa lililo huru,
kusherehekea uhuru, kuangazia mafanikio ya uandishi habari katika ulingo
wa kisiasa na kuwatambua wanafunzi bora wanaosomea uandishi ambao
wanawakilisha kizazi kijacho cha tasnia hiyo ya habari.
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama katika dhifa ya 2016
Trump awataja wanahabari wapinzani
Msemaji
wa Ikulu Sean Spicer mnamo siku ya Ijumaa aliwazuia wanahabari wa
mashirika kadhaa kuhudhuria kikao cha wanahabari katika Ikulu.
Wanahabari wa Mashirikia ya CNN, New York Times, Politico, Los Angeles
Times na Buzzfeed hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao cha wanahabari katika
ofisi ya msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani.
Katika kipindi cha
kampeini mwaka jana, kundi la Trump liliyapiga marufuku mashirika
kadhaa likiwemo gazeti la Washington Post na Buzzfeed dhidi ya kuripoti
katika mikutano ya kampeini likiyashutumu kwa upotoshaji ba kueneza
habari za uongo.
Spicer amesema Ikulu ya Marekani inapanga
kupambana dhidi ya kile alichokitaja kuangaziwa kionevu na vyombo vya
habari. Msemaji huyo wa Ikulu ameeleza kuwa hawatakaa tu na kuruhusu
taaarifa za uongo na za kupotosha zikitolewa.
Uhuru au upotoshaji wa habari?
Hatua
hiyo ya utawala wa Trump kuyashambulia mashirika ya habari nchini
Marekani imeashutumiwa vikali na makundi ya wanahabari na vyomvo hivyo
vya habari.
Taarifa kutoka kwa mhariri mkuu wa The New York Times
Dean Baquet ilisema jambo kama hilo halijawahi kutokea katika Ikulu ya
Rais ya White House katika historia yao ndefu ya kuripoti taarifa kutoka
tawala chungu nzima kutoka vyama tofauti vya kisiasa nchini Marekani.
Msemaji wa Ikulu ya Rais Sean Spicer
Baquet
alisema wanapinga vikali kuzuiwa kwa gazeti lao na mashirika mengine ya
habari na kuongeza kuruhusiwa kwa vyombo hivyo kuwa na uhuru na
kuangazia matukio ya serikali iliyo wazi bila shaka ni muhimu kwa
maslahi ya taifa.
Wakati wa kampeini zake kuingia madarakani,
Trump mwenye umri wa miaka 70 aliyashutumu vikali mashirika makuu ya
habari ya Marekani kwa kuwa na upendeleo na amezidisha shutuma hizo
baada ya kuingia madarkani kwa kudai wanahabari wanaangazia zaidi
mapungufu yake badala ya kuangazia mafanikio yake.
Stephen
Bannon, mkuu wa mipango na mshauri mwandamizi wa Trump ambaye pia ni
mkuu wa tovuti ya kihafidhina ya Breitbart, amebadhiri kuwa uhusiano
kati ya utawala huo mpya wa Marekani na wanahabari ambao amewataja
wapinzani utazidi tu kuwa mbaya jinsi rais huyo wa Marekani anavyozidi
kutoa ajenda zake.
No comments:
Post a Comment