Rais mpya wa Somalia, Mohamed Abdullahi
Mohamed Farmaajo aliyeapishwa jana mjini Mogadishu amemteua mkurugenzi
wa shirika moja la mafuta kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.
Shirika la habari la Reuters limetagaza habari hiyo na kuongeza
kuwa, Hassan Ali Khaire, Mkurugenzi wa Shirika la Mafuta na Gesi la
Soma la Uingereza na ambaye pia ana uraia wa Norway, ndiye Waziri Mkuu
mpya wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Tovuti ya radio ya serikali ya Muqdisho.net imewataka wananchi wa
Somalia kushirikiana na kufanya kazi bega kwa bega na Waziri Mkuu mpya
katika mchakato wa kuundwa serikali mpya.
Hata hivyo baadhi ya wadadisi wa mambo wamesema hatua ya Rais
Farmaajo ya kumteua mkuu huyo wa shirika la mafuta, huenda ikaibua suala
la mgongano wa maslahi.
Mohamed Mubarak, mwanaharakati mashuhuri wa kupambana na ufisadi
nchini Somalia amepongeza uteuzi wa Ali Khaire na kusisitiza kuwa, kuja
kwa Waziri Mkuu huyu mpya kunamaanisha kuwa nchi hiyo haitashuhudia
masuala ya rushwa kwa angalau miaka minne ijayo.
Baada ya kuapishwa katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi wa nchi
kadhaa za kanda hiyo chini ya hatua kali za ulinzi, rais mpya wa Somalia
ameahidi kurejesha heshima ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika lakini pia
akaonya kwamba, itachukua miongo miwili kurekebisha nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment