Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ameridhia muswada
tata wa mabadiliko ya katiba ambao kwa kiasi kikubwa utamuongezea
mamlaka rais huyo, huku kura ya maoni ikitarajiwa kupigwa ifikapo Aprili
16 mwaka huu.
Waungaji mkono wa Erdogan wanauona mpango huo unaochukua nafasi ya
bunge kwa kumpa mamlaka kamili Rais kuwa ni kama dhamana ya utulivu hasa
katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo inapitia mtikisiko mkubwa. Hata
hivyo wapinzani wanahofu kuibuka kwa utawala wa kimabavu katika nchi
hiyo ambayo imeshuhudia makumi kwa maelfu ya raia, kuanzia wanahabari
hadi wanajeshi wakitiwa vizuizini tangu mapinduzi yaliyoshindwa mwezi
Julai mwaka uliopita.
Taarifa fupi iliyotolewa kupitia tovuti ya
rais imesema muswada huo utakaompa mamlaka Rais ya kutoa amri, kutangaza
hali ya hatari, kuteua mawaziri na viongozi wa juu serikalini pamoja na
kulivunja bunge umepelekwa kwenye ofisi ya Waziri mkuu kwa ajili ya
kuchapishwa na kuwasilishwa kwa ajili ya kura ya maoni.
Mapema
mwezi huu, kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na Kansela wa
Ujerumani Angela Merkel alipofanya ziara nchini humo, Erdogan aliyatetea
kwa nguvu mapendekezo ya mabadiliko hayo, ambayo bado yanakabiliwa na
ukosoaji mkali kutoka kwa wapinzani wanaodai yatamuongezea mamlaka
makubwa zaidi.
Rais Recep Tayyip Erdogan na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walipokuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari nchini Uturuki
Naibu
waziri mkuu wa Uturuki, Numan Kurtulmus amewaambia wanahabari kwamba
jukumu lililopo sasa ni kwa bodi ya uchaguzi ambayo itatakiwa kutangaza
rasmi kwamba Aprili 16 ni siku maalumu kwa ajili ya kura ya maoni.
Kulingana
na Erdogan, mabadiliko hayo yataepusha kurejea kwa muungano wa vyama
ambao haukuwa na nguvu bungeni, lakini pia ni muhimu kwa wakati huu
ambapo Uturuki inakabiliwa na vitisho vya kiusalama, hususan kutokana na
mlolongo wa mashambulizi ya mabomu kutoka makundi ya Dola la Kiislamu,
IS na wapiganaji wa Kikurdi pamoja na mapinduzi yaliyoshindwa.
Katika
hatua nyingine, polisi nchini humo wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa
machozi kuwatawanya waandamanaji waliojaribu kuingia katika viunga vya
chuo kikuu cha Ankara kupinga hatua ya serikali ya kuwafukuza wahadhiri
330. takriban waandamanaji 12 wanashikiliwa.
Wahadhiri hao ni
miongoni mwa watumishi wa umma 4,500 waliotimuliwa siku ya Jumanne chini
ya amri ya serikali ya hali ya hatari iliyotangzwa tangu mapinduzi
yaliyofeli ya mwezi Julai mwaka uliopita.
No comments:
Post a Comment