Tuesday, April 25, 2017

MAREKANI YAWAWEKEA VIKWAZO WANASAYANSI 271 WA SYRIA

Marekani imewawekea vikwazo wafanyakazi zaidi ya 270 wa shirika la serikali ya Syria linalotuhumiwa kwa uundaji wa silaha za sumu, wiki kadhaa baada ya mashambulizi ya gesi ya sumu katika jimbo la Idlib.

IS Chemiewaffen Reaktionen Aleppo Syrien (picture-alliance/AP Photo)

Katika mojawapo ya hatua madhubuti kuwahi kuchukuliwa na Marekani, wizara ya fedha ya nchi hiyo imetangaza vikwazo vipya dhidi ya wanasayansi na baadhi ya maafisa wa nchini Syria kutokana na kuhusika kwao katika kuunda silaha za sumu, ambazo zinadaiwa kutumika kuwauwa raia zaidi ya watu 80 katika jimbo hilo la Idlib mapema mwezi huu.
Waziri wa fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, amesema vikwazo hivyo vipya vinakilenga kituo cha kisayansi kinachomuunga mkono Rais Bashar al-Assad na pia wafanyakazi 271 wa kituo hicho kinachoshughulikia mitaala na utafiti wa kisanyansi (SSRC).  Marekani inadai kwamba kituo hicho kilihusika na utengenezaji wa gesi ya sumu aina ya Sarin iliyotumika katika mashambulizi hayo.
Mnuchin ameeleza kwamba Marekani inatoa ujumbe madhubuti na pia haitavumilia matumizi ya silaha za sumu yatakayofanywa na yeyote yule. "Marekani inadhamiria kuuwajibisha utawala wa Assad kwa tabia yake isiyokubalika," alisema Munchin, aliyeongeza kuwa vikwazo hivyo ni pamoja na kuwazuia Wamarekani kufanya biashara na watu hao waliotajwa.
Vikwazo baada ya mashambulizi
USA Steven Mnuchin in New York (picture-alliance/Newscom)
Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, anasema vikwazo dhidi ya wanasayansi hao vinajumuisha kugomea kushirikiana nao kibiashara na kitaaluma.
Vikwazo hivyo vinakuja wiki chache baada ya jeshi la nchi hiyo kuushambulia uwanja wa ndege za kivita wa Syria mnamo tarehe 7 Aprili ili kuuadhibu utawala wa Assad na kutoa onyo dhidi ya kufanya mashambulizi zaidi kwa kutumia silaha za sumu. 
Uwanja huo ulishambuliwa kwa makombora 59 ya masafa ya kati aina ya "Tomahawk". Huko nyuma, tayari wizara ya fedha ya Marekani ilishawawekea vikwazo maafisa wengine 18 wa Syria mnamo Januari mwaka huu.
Mashambulizi hayo ya silaha za sumu pia yalijadiliwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini Urusi, ambayo nbi mshirika mkubwa wa Assad, iliitumia kura yake ya turufu kulizuia azimio lililoitaka serikali ya Syria itoe ushirikiano ili kuwezesha uchunguzi, huku Rais Assad akikanusha madai hayo dhidi ya nchi yake na kusema kwamba huo ni uzushi wa nchi za Magharibi.
Mnuchin amesema wizara yake "itashirikiana na wizara ya mambo ya nje pamoja na washirika wa kimataifa ili kuendeleza juhudi za kuhakikisha kwamba shughuli za kifedha za wote waliowekewa vikwazo zinafungwa."

SIKU YA MALARIA DUNIANI

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya malaria leo, shirika la afya duniani WHO limefahamisha hapo jana kuwa chanjo ya kwanza ya ugonjwa huo itaanza kufanyiwa majaribio nchini Kenya, Malawi na Ghana kuanzia mwaka 2018.

Malaria Mücke (picture alliance/blickwinkel/Hecker/Sauer)
Anopheles-mbu anayesababisha malaria
Chanjo hiyo ya kiwango kikubwa ilichukua miongo na mamilioni ya Dola kubuniwa.
Mratibu wa mpango wa kutekeleza chanjo hiyo Mary Hamel anasema chanjo hiyo kwa sasa imeshavuka ngazi ya kufanyiwa uchunguzi katika maabara na shirika la kudhibiti dawa la Ulaya limeisifu chanjo hiyo.
Chanjo hiyo iitwayo RTS,S ni kwaajili ya kuwakinga watoto wadogo dhidi ya aina mbaya ya malaria inayosababishwa na mbu aitwae Plasmodium falciparum. Itafanyiwa majaribio katika maeneo yatakayochaguliwa na nchi hizo tatu na maeneo hayo yanatakiwa kuwa na visa vingi vya maradhi ya malaria na pia kampeni za kupambana na ugonjwa huo.
Kulingana na Hamel, chanjo hiyo itatolewa kwa jumla ya watoto 360,000 walio kati ya umri wa miezi mitano na kumi na saba ili kubainisha iwapo dalili za kinga zilizooneshwa katika uchunguzi wa kliniki, zitaonekana pia katika hali ya kawaida ya maisha. Watoto watapokea chanjo hiyo mara tatu kwa mwezi wakiwa na umri wa miezi mitano na watapewa chanjo ya nne watakapotimiza miaka miwili.
Kenya, Ghana na Malawi zina mipango thabiti ya kinga ya malaria
Daktari Edward Mwangi ni afisa mkuu mtendaji wa muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali dhidi ya malaria nchini Kenya KeNaam, na anasema kinga hiyo ni muhimu na itasaidia pakubwa.
"Kwa mfano badala ya mtoto kuwa mgonjwa mara mbili au tatu kwa mwaka kutokana na malaria," alisema Edward, "atakuwa mgonjwa mara moja tu na jambo hili linapunguza idadi pia ya wale wanaokuwa wagonjwa ama wale wanaofariki kutokana na malaria mwisho wa siku," aliongeza afisa huyo wa KeNaam.
WHO inasema Kenya Ghana na Malawi ndizo nchi zilizochaguliwa kwa uchunguzi huo kutokana na kuwa nchi zote hizo zina mipango thabiti ya kinga lakini bado zina visa vingi vya malaria.
Pedro Alonso (picture-alliance/dpa/M. Trezzini)
Mkuu wa kitengo cha malaria WHO Pedro Alonso
WHO inatazamia kuangamiza malaria ifikiapo mwaka 2040 licha ya changamoto zilizoko katika vidonge na dawa zinazotumika kuwauwa mbu.
Daktari Mwangi lakini anasema kwamba chanjo hiyo haitokuwa mwisho wa malaria barani Afrika na sehemu zilizoathirika na maradhi hayo duniani.
Malaria ni changamoto kubwa ya kiafya inayoikabili dunia
"Chanjo hiyo ni nyongeza tu ya kupambana na malaria na labda kuuangamiza ugonjwa huo barani Afrika na sehemu nyengine," alisema Edward, "kwa hiyo kitakachofanyika ni kuwa, chanjo hiyo itatolewa, lakini zile mbinu zengine zinazotumika ili kujikinga dhidi ya malaria zitakuwa zikitumika pia, kama vile matumizi ya vyandarua na hata unapokuwa mgonjwa utaweza kutibiwa bado," aliongeza mkuu huyo wa KeNaam.
Simbabwe Moskitozelt (DW/P. Musvanh)
Utumizi wa vyandarua bado utaendelea hata baada ya chanjo hiyo kutolewa
Malaria inasalia kuwa mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za kiafya zinazoikabili dunia, kwani zaidi ya watu milioni 200 huambukizwa kila mwaka na takriban nusu milioni kuaga dunia, wengi wao wakiwa watoto kutoka Afrika. Utumiaji wa vyandarua na dawa za kuuwa mbu ndiyo njia za pekee ambazo zimetumika kujikinga dhidi ya malaria.
Nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara barani Afrika ndizo zilizoathirika pakubwa, huku ikiwa asilimia 90 ya visa vya malaria kote duniani mwaka 2015 vikitoka barani humo.
WHO inasema, juhudi za dunia za kukabiliana na malaria, zimepelekea visa vya vifo vinavyotokana na malaria kupungua kwa asilimia 62 kati ya mwaka 2000 na 2015. Lakini shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa linasema pia kwamba, takwimu kama hizo mara nyingi hutumiwa kwa masuala ya hesabu tu ila hali ni mbaya mno katika nchi 31 Afrika, kiasi ya kwamba haliwezi kuelezea iwapo kiwango kimekuwa kikiongezeka ama kushuka katika miaka 15 iliyopita.

Monday, April 24, 2017

UCHAGUZI WA RAIS WA IRAN KUFANYIKA KATIKA NCHI 102 DUNIANI

Tume ya Uchaguzi ya Iran imetangaza kuwa, uchaguzi wa rais wa awamu ya 12 wa Iran utafanyika katika nchi 102 kote duniani.
Katika taarifa, Katibu wa Tume ya Uchaguzi Ali Pur-Ali Mutlaq amesema Wairani wanaoishi nje ya nchi wataweza kupiga kura katika viituo 269 vya upigaji kura vilivyoko katika ofisi 131 za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi 102 kote duniani.
Ameongeza kuwa, wawakilishi wa Iran katika nchi hizo  tayari wameshapokea kila kitu kinachohusu uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wagombea sita wa urais mwaka huu ni pamoja na Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu, Mostafa Hashemi-Taba makamu wa rais wa zamani ambaye pia aliwahi mkuwa mkuu wa kamati ya kitaifa ya Olimpiki, Es'haq Jahangiri makamu wa kwanza wa serikali ya sasa, Mohammad-Baqer Qalibaf meya wa mji wa Tehran, Seyyed Ebrahim Raeisi msimamizi wa Haram Takatifu ya Imam Ridha AS na rais wa sasa  Hassan Rouhani ambaye anatetea nafasi yake ili amalize kipindi chake cha pili.
Zoezi la upigaji kura Iran
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi ujao wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran. Wairani wanaoishi nje ya nchi wanaweza kushiriki katika uchaguzi wa rais pekee.

Sunday, April 23, 2017

WAFARANSA WAPIGA KURA KUMCHAGUA RAIS

Raia wa Ufaransa Jumapili (23.04.2017) wamemiminika katika vituo vya kupigia kura, huku usalama ukiwa umeimarishwa. Ni duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais, unaotazamwa kama kiashirio cha mustakbali wa Umoja wa Ulaya.

Frankreich - Präsidentschaftswahl (Getty Images/AFP/A.-C. Poujoulat)

Kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Marine Le Pen, na wa siasa za wastani Emmanuel Macron wanatarajiwa kuongoza katika duru hiyo na kuingia katika duru ya pili itakayofanyika Mei 7, lakini mchuano ni mkali katika taifa hilo lililogawanyika kwa sasa. Waangalizi wanatabiri ushindi wa Le Pen unaweza kuwa pigo kwa Umoja wa Ulaya, ambao tayari umedhoofishwa na kura ya maoni ya Ungereza ya kujiondoa katika umoja huo.
 Macron, mwenye umri wa miaka 39, anagombea kuwa rais wa kwanza wa Ufaransa mwenye umri mdogo, na amekuwa akiuunga mkono Umoja wa Ulaya pamoja na maendeleo ya kibiashara katika kampeni zake.
Upigaji kura umwekwenda kinyume na matabirio ya kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura baada ya kampeni za uchaguzi kutawaliwa na kashfa na kushuka kwa  umashuhuri wa vyama vikuu ambayo vimekuwa vikipokezana madaraka kwa nusu karne iliopita.
Idadi kubwa yajitokeza
Infografik Wahlprogramm der Kandidaten Frankreich englisch
Wagombea wanne miongoni mwa kumi na moja.
Baada ya masaa tisa ya kupiga kura idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa asilimia 69.42 mojawapo ya kiwango cha juu kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40.Kikiwa chini kidogo ya kiwango cha uchaguzi wa mwaka 2012, saa moja ya ziada ya kupiga kura katika miji midogo inatarajiwa kukifanya iwango hicho kufikia asilimia asilimia 78 hadi 81.
Le Pen amepiga kura yake huko Henin-Beaumont mji uliokuwa ukizalisha makaa ya mawe hapo zamani ambayo ni ngome ya chama chake kaskazini mwa nchi hiyo.
Macron amepiga kura katika mji wa kitalii wa Le Touquet akiwa pamoja na mke wake Brigitte mwalimu wake wa shule wa zamani ambaye ni mkubwa wake kwa miaka 25.Fillon na Melenchon wote wawili wamepiga kura zao mjini Paris.
Takariban watu milioni 47 wanastahiki kupia kura katika taifa hilo la kanda ya sarafu lenye kushika nafasi ya ili kwwa kuwa na guvu kubwa za kiuchumi.
Uchaguzi warindima nje ya mipaka.
Frankreich Präsidentschaftswahl Francois Hollande (Reuters/R. Duvignau)
Rais Francois Hollande katika kituo cha kupigia kura.
Wakati wapiga kura wakipiga kura katika uchaguzi huo wanafanya chaguo ambalo litarindima kupindukia mipaka ya Ufaransa  kuanzia medani za vita nchini Ufaransa sakafu za biashara huko Hong Kong na kumbi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mustakbali wa Ulaya uko hatarini wakati nchi hiyo ikikabiliwa na uchaguzi tafauti na nchi nyengine ambao yumkini ukarekebisha utambulisho wa Ufaransa wa baada ya kipindi cha vita na kuashiria iwapo sera kali za mrengo wa kulia zinaongezeka au kupunguwa.
Takriban wagombea wote 11 wefanya kampeni dhidi ya Umoja wa Ulaya ambao unalaumiwa kwa matatizo lukuki.Wagombea wawili kati ya hao wana nafasi ya kushinda uchaguzi huo wa rais mwanasiasa wa sera kali za mrengo wa kulia Marie Le Pen na yule wa sera kali za mrengo wa kushoto Jean- Luc wanaweza kutaka kujitowa kwa Ufransa katika umoja huo pamoja na matumizi yao ya pamoja ya sarafu ya euro.
Kujitowa kwa Ufaransa kutakuwa balaa
 Marine Le Pen (Reuters/P. Rossignol)
Marine Le Pen akipiga kura yake.
Kujitowa kwa Ufaransa katika umoja huo kutakuwa kubaya zaidi kuliko kule kujitowa kwa Uingereza kutaashiria kifo kwa Umoja wa Ulaya,sarafu ya euro na fikra nzima ya umoja wa Ulaya iliozaliwa kutokana na damu iliomwagika wakati wa Vita Vikuu vya Dunia.
Ufaransa ni taifa manachama muasisi wa Umoja wa Ulaya na inashikilia kiti cha udereva pamoja na mwanachama mwenzake Ujerumani.
Masoko ya fedha tayari yana wasi wasi juu ya uwezekano wa kujitowa kwa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya  Frexit yakihofia udhibiti wa kuhamisha fedha,kuondolewa kwa mtaji,kufilisika na kesi za madai juu ya hati za dhamana na kondarasi.Timu ya Le Pen haizipi uzito habari za kutokea maangamizi ya aina hiyo kwa hoja kwamba itakavyokuwa sarafu ya euro inaelekea kusambaratika.
Le Pen na Melenchon pia wanalaumu mikataba ya biashara huru kwa kuuwa ajira za Ufaransa na wanataka kuijadili upya jambo ambalo litasababisha mzongo wa kifedha kwa umoja wote wa Ulaya na washirika wa biashara wa Ufaransa.
Iwapo Le Pen au Melenchon wataingia duru ya pili huo utaonekana kuwa ushindi wa wazi kwa kwa wimbi la sera kali za mrengo wa kulia lililonyeshwa wakati wa kumchaguwa Rais Donald Trump wa Marekani na kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.
Marekebisho sheria za ajira
Frankreich Präsidentschaftswahl Emmanuel Macron (Reuters/E. Feferbert)
Emmanuel Macron akipiga kura yake. mi
Emmamuel Macron wa sera za wastani na mhafidhina Francois Fillon wamejitolea kwa umoja wa Ulaya na watazifanyia mageuzi sheria za kazi lakini hawatofanya mabadiliko makubwa sana. Macron amejitangaza kama mgombea dhidi ya sera kuhami masoko za Trump.
Ufaransa ambayo ina nguvu za silaha za nyuklia na kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ina maelfu ya wanajeshi wake duniani na ni mshirika wa karibu wa Marekani katika kampeni ya kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislam.
Macron yumkini akaendeleza operesheni dhidi ya wapinagaji wa itikadi kali nchini Iraq na Syria na kanda ya Sahel barani Afrika pamoja na kuishinikiza Urusi kuhusiana na suala la Ukraine na hatua zake za kumpa nguvu Rais Bashar al Assad wa Syria

Saturday, April 22, 2017

KOREA KASKAZINI: TUMEJIANDAA KUIKABILI MAREKANI NA HATUTISHIKI NA MELI ZAKE ZA KIVITA

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza utayarifu wake wa kukabiliana na hatua yoyote ya kichokozi ya Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini sambamba na kutangaza habari hiyo imesema kuwa, katika kufuatilia nyendo za Marekani, Pyongyang imejiandaa kukabiliana na chokochoko za Washington. Katika ripoti hiyo, Pyongyang imezungumzia hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kutuma meli zake za kivita katika maji ya Peninsula ya Korea na kuongeza kuwa, Pyongyang haitishiki na jambo hilo.
Kim Jong-un akiwa na makomando wa nchi yake
Kadhalika Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, hatua hizo za Marekani kamwe haziiogofyi nchi hiyo na kwamba jeshi lake linasubiri amri ya kukabiliana haraka na Marekani. Marekani ilituma meli zake za kivita katika Peninsula ya Korea baada ya kushtadi mgogoro baina yake na Korea Kaskazini. Hii ni katika hali ambayo China na Korea Kaskazini zimesisitiza mara kadhaa kwamba, uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo, unatishia usalama wa nchi hizo sambamba na kusababisha kuibuka mashindano ya silaha katika eneo. Katika hatua nyingine, serikali ya Pyongyang imeionya China kwamba kuendelea vikwazo vya nchi hiyo dhidi yake, kutaharibu mahusiano ya nchi mbili.
Viongozi wa Uchina na Korea Kaskazini
Taarifa iliyotolewa na Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, kuendelea mwenendo huo wa vikwazo vya Uchina ni suala ambalo litakuwa na hatima mbaya katika mahusiano ya nchi hizo. Siku chache zilizopita, Beijing ilitangaza kusimamisha safari za ndege zake kwenda Korea Kaskazini huku ikisema kuwa, hatua hiyo haijatokana na sababu za kisiasa. Kabla ya hapo China ililalamikia hatua ya Pyongyang ya kufyatua kombora la balestiki kuelekea maji ya China na kukitaja kitendo hicho kuwa hatari. China na Korea Kaskazini zinafahamika kwa kuwa na mahusiano ya karibu kwa muda mrefu.

Thursday, April 20, 2017

UAMUZI WA MAHAKAMA KUU INDIA DHIDI YA VIONGOZI WA CHAMA TAWALA, KUBOMOLEWA MSIKITI WA BABRI

Mahakama Kuu ya India imetangaza kuwa, viongozi watatu wa ngazi za juu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) wanapaswa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuharibu Msikiti wa Babri na mauaji ya Waislamu.
Watu hao watatu wanatuhumiwa kwamba, waliwachochea Wahindu wenye misimamo mikali kuharibu Msikiti wa Babri katika mji wa Ayodhya, jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India tarehe 6 Disemba 1992, suala ambalo lilizusha hitilafu na machafuko makubwa ya kikaumu na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu. Wahindu wenye misimamo mikali waliharibu msikiti huo kwa lengo la kujenga hekalu la Ram mahala pale.
Majaji wa Mahakama Kuu ya India wamesema, Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa Msikiti wa Babri uliojengwa karne ya 16.
Machafuko yuliyosababishwa na kubomolewa msikiti huo na hitilafu zilizotokea baina ya Waislamu na Wahindu vimesababisha mauaji ya Waislamu zaidi ya elfu mbili na kujeruhiwa wengine wengi.  
Awali mahakama hiyo ilitosheka kwa kumkosoa aliyekuwa mkuu wa chama cha Bharatiya Janata, Subramanian Swamy kwa kufanya njama za kuboa Msikiti wa kihistoria wa Babri na kutaka kujenga maabadi ya Wahindu mahala pale.  Mahakama Kuu ya India ilisisitiza kuwa, chama cha Bharatiya Janata hakiwezi kufikia malengo yake katika jimbo la Uttar Pradesh kwa kutumia mabavu. 
Wahindu wakibomoa Msikiti wa Babri
Rai ya sasa ya Mahakama Kuu ya India inayotaka kupandishwa kizimbani viongozi wa ngazi za juu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) kwa kuhusuka na kuharibiwa Msikiti wa Babri na mauaji ya maelfu ya Waislamu inaweza kutambuliwa kuwa ni mpambano baina ya serikali na Idara ya Mahakama ya nchi hiyo. Chama cha Bharatiya Janata ambacho kilishika hatamu za uongozi nchini India baada ya kushinda uchaguzi wa Bunge mwaka 2014 - kama ilivyokuwa imetabiriwa- kilizidisha mashinikizo na ukandamizaji dhidi ya Waislamu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Katika mkondo huo huo, kwa wiki kadhaa sasa chama hicho kimekuwa kikishinikiza Mahakama Kuu ya India kwa shabaha ya kuilazimisha itoe hukumu kwa maslahi ya viongozi wake. Hata hivyo hukumu ya mahakama hiyo imekwenda kinyume na matakwa yake.
Waislamu wa India wana wasiwasi mkubwa kuhusu utendaji wa chombo hicho cha sheria na uwezo wake wa kulinda msingi wa kutopendelea upande wowote katika kesi muhimu sana baina ya Wahindu na Waislamu. Vilevile duru mbalimbali za India zinasema kuwa, Wahindu wenye misimamo mikali wangali wanashikilia misimamo yao kuhusu ujenzi wa maabadi ya Ram sehemu ya Msikiti wa kihistoria wa Babri licha ya uamuzi wa mahakama hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mpango wa kujenga maabadi hiyo sehemu ya Msikti wa Babri umekuwa ukitajwa sana katika ahadi za chama tawala cha Bharatiya Janata katika kampeni za uchaguzi. 
Msikiti wa Kihistoria wa Babri
Wahindu wenye misimamo mikali wanadai kuwa, kabla ya kujengwa Msikiti wa Babri kulikuwepo hekalu au maabadi ya Ram mahala hapo, madai ambayo hayana mashiko ya kihistoria.
Hivi sasa baada ya Mahakama Kuu ya India kutoa hukumu ya kupandishwa kizimbani viongozi wakuu watatu wa chama tawala kwa tuhuma za kuhusika na ubomoaji wa Msikiti wa Babri na mauaji ya maelfu ya Waislamu wa India, kuna wasiwasi kwamba chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) kitatumia njia mbalimbali za vishawishi na vitisho kwa ajili ya kumshinikiza jaji anayeshughulikia faili hilo ili atoa hukumu dhidi yua Waislamu. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema itakuwa vigumu sana kwa chama hicho kufikia malengo yake baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya India ya kupandishwa kizimbani viongozi hao watatu wa chama cha BJP.

UN YAIONYA SAUDIA DHIDI YA KUSHAMBULIA KWA MABOMU BANDARI YA YEMEN

Umoja wa Mataifa umeutaka muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia usishambulie kwa mabomu bandari ya kistaratejia ya Yemen.
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ametahadharisha kuwa, iwapo Bandari ya al-Hudaydah iliyopo katika Bahari Nyekundu itashambuliwa kwa mabomu na Saudia, basi yumkini idadi kubwa ya raia wa Yemen wakatumbukia katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Katika kikao na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Jordan, Amman hii leo, afisa huyo wa UN amefafanua kuwa: "Bandari ya al-Hudayda ni kituo nyeti kwa raia wa Yemen, hatuoni iwapo kuna haja ya eneo hilo la kistaratajia kushambuliwa na muungano wa kijeshi wa Saudia. Muungano huo unafaa kulipa uzito na umuhimu suala la kibinadamu unapokuwa katika kampeni na operesheni zake. Iwapo bandari hiyo itashambuliwa, sisi pamoja na asasi zingine za kufikisha misaada ya kibinadamu hatutaweza kufikisha chakula, dawa na mahitaji mengine ya msingi kwa raia wa Yemen."
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Bandari ya al-Hudaydah ndiyo bandari muhimu zaidi ya Yemen ambapo karibu asilimia 80 ya shehena za chakula na dawa zinazofikishwa kwa wananchi, hupitishwa kupitia bandari hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Yemen hapo jana walikusanyika mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a kulaani kufungwa Bandari ya al-Hudaydah sambamba na kukosoa mauaji ya kikatili dhidi ya watu wa taifa hilo, yanayofanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, tangu Machi mwaka 2015.

WAZIRI MKUU WA KOREA KUSINI, ATOA AMRI KULITAKA JESHI LA NCHI HIYO LIJIWEKE TAYARI KUKABILIANA NA PYONGYANGA

Waziri Mkuu wa Korea Kusini anayekaimu nafasi ya rais, amelitaka jeshi na vikosi vya nchi hiyo kujiweka tayari kutokana na kile alichokisema kuwa ni kushadidi kwa harakati za kijeshi za Pyongyang.
Hwang Kyo-ahn ameyasema hayo Alkhamis ya leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri la Korea Kusini kufuatia kuenea kwa habari zinazohusiana na uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio la sita la silaha ya nyuklia hivi karibuni. Kufuatia hali hiyo Hwang Kyo-ahn ametoa amri kwa jeshi la nchi yake kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na hatua yoyote ya kijeshi na harakati za Korea Kaskazini.
Jeshi la Korea Kusini
Kadhalika Waziri Mkuu wa Korea Kusini amelitaka jeshi la nchi hiyo kufuatilia kwa karibu mabadiliko na harakati zote za Pyongyang. Mgogoro katika eneo la Peninsula ya Korea ulishadidi baada ya Rais Donald Trum wa Marekani na makamu wake wa rais, Mike Pence kutoa matamshi ya vitisho kuilenga Pyongyang, vitisho ambavyo vilienda sambamba na kutumwa kwa meli tatu za kijeshi zinazobeba ndege za kivita karibu na pwani ya Korea Kaskazini.
Hwang Kyo-ahn, Waziri Mkuu wa Korea Kusini
Hatua hiyo ya Marekani ilitajwa na Korea Kaskazini kuwa, ya kichokozi na inayohatarisha usalama na amani ya peninsula hiyo. Mbali na hayo ni kwamba Korea Kaskazini imesisitiza mara kadhaa kwamba, madamu Marekani na waitifaki wake zitaendelea kutishia usalama wake, basi nayo itazidi kuimarisha uwezo wake wa kijeshi kukabiliana na chokochoko za adui.

SERA ZA MAREKANI KATIKA MASHARIKI YA KATI NI KUENEZA HOFU NA VITISHO DHIDI YA IRAN

James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Riyadh Saudi Arabia baada ya kukutana na mwenyeji wake kwamba, timu ya Rais Donald Trump inaandaa mikakati ya kuidhibiti na kuikwamisha Iran kupitia njia ya kuimarisha uratibu na Saudi Arabia na waitifaki wengine wa Marekani.
Jenerali Mattis amedai kwamba, Iran imekuwa ikivuruga amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati hivyo kuna haja ya kuzuia satwa na ushawishi wa taifa hili ili ipatikane njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen kupitia mazungumzo kwa upataishi wa Umoja wa Mataifa. Kwa hakika matamshi haya ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani si jambo jipya. Viongozi wa Marekani bila kujali ni wa chama cha Democrats au cha Repulican wamekuwa wakitumia lugha hizo za vitisho tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulipokuja na kukata mikono ya Marekani hapa nchini.
Kwa muktadha huo, uadui wa madola yanayotumia mabavu ulimwenguni hususan Marekani kwa taifa taifa la Iran ni jambo lisilo na shaka hata kidogo. Hii inatokana na kuwa, uadui wao uliendelea kushuhudiwa katika kipindi chote ambacho serikali mbalimbali na zenye utashi tofauti zilipoingia madarakani nchini Marekani.
Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Saudia
Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, lengo la viongozi wa Marekani katika kipindi hiki la kutumia lugha hizi za vitisho ni kutoa ishara ya kuweko mabadiliko ya kimsingi katika sera za Marekani katika kukabiliana na Iran. Hivi sasa siasa za Marekani dhidi ya Iran kwa namna fulani zinaonekana kuipa Saudi Arabia baadhi ya majukumu. Kiasi kwamba, akitoa natija jumla ya mazungumzo yake huko Riyadh, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa, Washington imefikia natija na Riyadh kuhusiana na jambo hilo.  Mattis amesema: Kwa hakika sisi tunapaswa kufanya kitu na kuimarisha muqawama wa Saudia mbele ya miamala ya Iran. Kama ambavyo tunafanya kazi tukiwa washirika, tunapaswa kuchukua hatua ambazo zitakufanyeni nyinyi viongozi wa Saudia na jeshi lenu muwe na utendaji mzuri zaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameyatoa matamshi na madai haya mjini Riyadh katika hali ambayo, kila mahala ambako kuna matatizo katika Mashariki ya Kati na popote pale ambako kunafukuta moto wa vita kuanzia Asia mpaka Ulaya na Afrika mpaka Amerika ya Latini basi kunashuhudiwa mkono wa Marekani na waitifaki wake.
Aidha stratejia ya Marekani katika Mashariki ya Kati inaeleweka wazi. Stratejia hiyo haina tofauti sana na duru zilizopita za uongozi nchini Marekani kabla ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump. Marekani ingali inawategemea watawala wa nchi za Kiarabu wa eneo hili katika uuzaji silaha zake kwa kisingizio cha kukabilia na vitisho ambavyo Marekani yenyewe imevipandikiza. Utawala wa Aal Saud nao ukitumia mbinu ya kale umekuwa ukinunua silaha nyingi kwa kutumia fedha za mafuta ikiwa na lengo la kununua muda zaidi kwa utawala wake unaotetereka na kulegalega.
Katika uwanja huo, himaya ya Marekani kwa uvamizi wa Saudia katika vita vya Yemen ni jambo muhimu, kwani kivitendo siasa za chokochoko za Saudia katika vita hivyo na vile vile katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq zimeshindwa na kugonga mwamba. Njia pekee iliyobakia kwa Aal Saud ni kutoa upendeleo kwa Marekani usio na masharti yoyote. Hata hivyo inawezekana kuyatazama matamshi haya ya Mattis katika engo nyingine. Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani anasema kuwa, Washington na washirika wake wanataka kuikwamisha Iran.
Matamshi haya kwa namna fulani yanaweza kuwa yana lengo la kupima radiamali ya Iran mkabala na lugha za vitisho za Marekani. Kwani viongozi wa White House wanatambua vyema msimamo wa Iran kuhusiana na jambo hilo. 
Ayatullah Ali Khamenei, alipokuna na makamanda wa jeshi kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi nchini Iran
Akihutubia Jumatano ya jana kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi hapa nchini, wakati alipokutana na kundi la makamanda wa jeshi, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa, moja ya nukta imara za mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni kuwa na moyo wa kishujaa na kusimama kwake kidete mbele ya makeke na upayukaji wa madola ya kibeberu. Aidha alisema kuwa, moja ya hila na ujanja unaotumiwa na madola vamizi ni kuyatisha mataifa na tawala za nchi nyingine na kutumia woga wa mataifa hayo kufanikisha malengo haramu ya madola hayo ya kibeberu na ndio maana mara zote utayaona madola hayo ya kiistikbari yakipenda kujigamba na kujionesha kuwa yana nguvu kubwa.
Kiongozi Muadhamu amesema bayana kwamba, kama Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran lingeyaogopa madola ya kibeberu na kulegeza kamba mbele yao, basi leo hii kusingekuwa na athari yoyote ile ya Iran na Uirani. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, adui yeyote yule, awe Mmarekani au mkubwa kuliko Marekani hawezi kufanya lolote mbele ya mfumo wa utawala unaotegemea vizuri nguvu za wananchi wake na ambao umesimama kidete mbele ya adui.

Wednesday, April 19, 2017

WANASIASA WA CHAMA TAWALA INDIA KIZIMBANI KWA KUCHOCHEA KUBOMOLEWA MSIKITI

Mahakama ya Juu nchini India imetoa hukumu kwamba wanasiasa wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata Party (BJP) wanapaswa kupandishwa kizimbani kwa kuhusika na kitendo cha kubomolewa msikiti wa kihistoria nchini humo.
Wakitoa uamuzi hii leo, majaji wa mahakama hiyo wamesema Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa Msikiti wa Babri wa karne ya 16, mwaka 1992.
Kadhalika Mahakama ya Juu ya India imepitisha kuwa, mwanasiasa mwingine mkongwe wa chama tawala nchini humo, Kalyan Singh anafaa kufunguliwa mashtaka pamoja na wenzake watatu kuhusiana na kadhia hiyo, kwa kuwa wakati wa ubomoaji wa msikiti huo wa kale, alikuwa mkuu wa Jimbo la Uttar Pradesh.
Vijana wenye misimamo mikali wa Kibaniani wakishangilia baada ya kubomoa msikiti wa kale Babri nchini India
Sanjay Jha, Msemaji wa Muungano wa Upinzani nchini humo amepongeza uamuzi huo uliotolewa leo Jumatano na Mahakama ya Juu ya India, akisisitiza kuwa, korti imeonelea kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa kuwapandisha kizimbani wanasiasa hao wa chama tawala.
Baada ya kubomolewa Msikiti wa Babri katika mji wa Ayodhya, Jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India tarehe 6 Disemba 1992, machafuko yalitawala eneo hilo, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

WANASIASA WA CHAMA TAWALA INDIA KIZIMBANI KWA KUCHOCHEA KUBOMOLEWA MSIKITI

Mahakama ya Juu nchini India imetoa hukumu kwamba wanasiasa wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata Party (BJP) wanapaswa kupandishwa kizimbani kwa kuhusika na kitendo cha kubomolewa msikiti wa kihistoria nchini humo.
Wakitoa uamuzi hii leo, majaji wa mahakama hiyo wamesema Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa Msikiti wa Babri wa karne ya 16, mwaka 1992.
Kadhalika Mahakama ya Juu ya India imepitisha kuwa, mwanasiasa mwingine mkongwe wa chama tawala nchini humo, Kalyan Singh anafaa kufunguliwa mashtaka pamoja na wenzake watatu kuhusiana na kadhia hiyo, kwa kuwa wakati wa ubomoaji wa msikiti huo wa kale, alikuwa mkuu wa Jimbo la Uttar Pradesh.
Vijana wenye misimamo mikali wa Kibaniani wakishangilia baada ya kubomoa msikiti wa kale Babri nchini India
Sanjay Jha, Msemaji wa Muungano wa Upinzani nchini humo amepongeza uamuzi huo uliotolewa leo Jumatano na Mahakama ya Juu ya India, akisisitiza kuwa, korti imeonelea kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa kuwapandisha kizimbani wanasiasa hao wa chama tawala.
Baada ya kubomolewa Msikiti wa Babri katika mji wa Ayodhya, Jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India tarehe 6 Disemba 1992, machafuko yalitawala eneo hilo, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Tuesday, April 18, 2017

RUSSIA NA CHINA ZATUMA MELI ZAO ZA KIJESHI KARIBU NA ENEO ZILIPO MELI ZA US, KOREA

Russia na China zimetuma meli zao za kijeshi katika eneo zilipo meli za Marekani karibu na pwani ya Korea Kaskazini kwa lengo la kufuatilia nyendo za meli za Marekani katika eneo hilo.
Gazeti la Japan la Yomiuri Shimbun limeandika kuwa, serikali ya Uchina imeomba msaada kwa Russia kwa ajili ya kuzuia kutokea mgogoro wa kivita huko Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa gazeti hilo, Beijinga na Moscow zimeamua kutuma meli zao za kivita kwa ajili ya kukusanya taarifa za kiintelijensia kutoka meli za Marekani, ili kuzuia kuongezeka kwa mgogoro baina ya Marekani na Korea Kaskazini.
Moja ya meli za kivita za Marekani zilizotumwa Korea
Wakati huo huo gazeti la Japan News, linaloandikwa kwa lugha ya Kingereza limesema kuwa, meli hizo za Uchina na Russia zitakuwa na kazi ya kutoa indhari na kupiga doria sambamba na kuzidisha ulinzi wa kujitawala anga na bahari ya eneo hilo. Awali Rais Donald Trump wa Marekani alitoa amri ya kutumwa meli tatu za kubeba ndege za kivita za 'USS Carl Vinson' 'Ronald Reagan' na 'USS Nimitz' kwenda pwani ya Korea, hatua ambayo ilitajwa na serikali ya Pyongyang kuwa ni ya kichokozi.
Moja ya meli za kivita za Uchina
Katika hatua nyingine serikali ya Korea Kusini imesisitiza azma yake ya kuweka ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD katika ardhi yake na kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika suala hilo. Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema Jumatatu ya jana katika kujibu baadhi ya tetesi zilizoashiria kuwa Seoul na Washington zimeamua kusitisha zoezi la uwekaji ngao hiyo,  kwamba habari hizo hazina ukweli wowote.

KOREA KASKAZINI YALAANI MAREKANI KWA 'KUHUJUMU ' AMANI

Balozi wa Korea Kaskazini ameituhumu Marekani kuhujumu amani na utengamano katika Rasi ya Korea wakati mvutano ukishamiri katika eneo hilo. Akizungumza katika Umoja wa Mataifa Balozi Kim In-ryong alisisitiza kuwa Korea Kaskazini iko tayari kwa vita kamili na Marekani. Alisema mwenendo wa Marekani wa kutumia ubabe kuzivamia nchi huru na baadaye kudai inachangia katika kulinda amani ya dunia ni kukosa uwajibikaji. Korea Kaskazini ambayo hujulikana pia kama Jamhuri wa Kidemokrasia ya Watu wa Korea ilizidisha mvutano wa kikanda kwa kufanya jaribio jingine la kurusha kombora ambalo lilishindwa Jumapili. Wanadiplomasia kadhaa wa nchi hiyo wamesema nchi yao itaendelea kufanya majaribio mengine kila wiki, kila mwezi na kila mwaka.

UPINZANI WATAKA KUFUTWA KWA MATOKEO UTURUKI

Chama kikuu cha upizani Uturuki kimeitaka tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya kura maoni ambayo yamempa madaraka mapya makubwa kabisa rais wa taifa hilo kutokana na ukiukaji mkubwa sana wa taratibu za kupiga kura.
Türkei Referendum | (picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis)
Chama kikuu cha upizani nchini Uturuki kimeitaka tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya kura maoni ya kihistoria nchini humo ambayo imempa madaraka mapya makubwa kabisa rais wa taifa hilo kutokana na ukiukaji mkubwa sana wa taratibu za kupiga kura.
Ujumbe wa kimataifa wa waangalizi ambao umeangalia kura hiyo ya maoni pia umegunduwa kuwepo kwa ukiukaji wa taratibu za kupiga kura kwa kusema upigaji kura huo hapo Jumapili ulikuwa haukukidhi viwango vya kimataifa.Hususan umekosowa uamuzi wa tume ya uchaguzi ya Uturuki kuzikubali kura ambazo zilikuwa hazina mihuri rasmi jambo mbalo imesema limedhoofisha usalama dhidi ya udanganyifu.
Tume hiyo ya uchaguzi ya Uturuki imethibitisha ushindi wa kura ya ndio katika kura hiyo ya maoni na kusema matokeo ya mwisho yataamuliwa katika kipindi cha siku 11 hadi siku 12 hivi.Shirika la habari la taifa Anadolu limesema kura za "ndio"  zilikuwa asilimia 51.4 wakati zile za "hapana" zilikuwa asilimia 48.6 .
Tafauti hiyo ya kura itaimarisha hatamu ya Erdogan madarakani nchini Uturuki kwa muongo mzima na inatazamiwa kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa kisiasa wa muda mrefu wa nchi hiyo na mahusiano yake ya kimataifa. Wapinzani wa mabadiliko hayo ya katiba hoja yao ilikuwa mageuzi hayo yanampa madaraka makubwa mno mtu ambaye amekuwa akizidi kuonyesha tabia za udikteta.
Alilazimika kupambana na mataifa yenye nguvu
Türkei Referendum Recep Tayyip Erdogan (picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis) Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Howard Eissenstat profesa mshiriki wa historia ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha St.Lawrence huko Canton,New York amesema "anatuhumu matokeo hayo ni finyu kuliko vile alivyokuwa ametegemea Erdogan".Ameongeza kusema " Erdogan aliwahi kutawala kwa ushindi wa kura chache hapo kabla na kwamba haoni ushindi wa kura chache kuwa ni kitu kengine ziada ya mamlaka.Msimamo wake emekuwa kutoujumuisha upinzani bali kuutokomeza".
Hapo Jumatatu Erdogan amewashambulia wakosoaji wake wa ndani na nje ya nchi kwa kusema "amelazimika kupambana na mataifa yenye nguvu duniani ambayo yalipinga kura ya ndio katika kura hiyo ya maoni ya kumuongezea madaraka."
Akihutubia wafuasi wake katika uwanja wa ndege wa Ankara hapo Jumatatu alipokuwa amewasili kutoka Istanbul amesema alikuwa "ameshambuliwa na mataifa yenye " mawazo "ya vita vya kidini dhidi ya Uislamu."
Haiko wazi iwapo alikukuwa akiyakusudia mataifa ya Ulaya yakiwemo Ujerumani na Uholanzi ambayo yaliwazuwiya mawaziri wake kufanya kampeni za mikutano ya hadhara kuwashawishi Waturuki wanaoishi katika nchi hizo kupiga kura ya ndio wakati wa kura hiyo ya maoni.
Merkel ataka serikali izungumze na upinzani
Merkel und Hollande Symbolbild (Getty Images/S. Gallup) Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa .
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameitolea wito serikali ya Uturuki kufanya mazungumzo ya kina na vyama vyote vya kisiasa pamoja na asasi za kiraia, kutokana na ushindi finyu wa kura hiyo ya maoni kuonesha namna taifa hilo lilivyogawika. Katika taarifa ya pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sigmar Gabriel, Merkel amesema Ujerumani inaheshimu uamuzi wa watu wa Uturuki juu ya katiba yao, lakini wakati huo huo wamemtaka Rais Erdogan kutambua dhamana kubwa aliyonayo katika kuivuusha nchi yake kwenye hatua ya pili.
Ufaransa nayo imejiunga na Ujerumani kumtaka Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki kufanya mazungumzo na wapinzani wake wa kisiasa, kufuatia ushindi huo finyu sana kwenye kura ya maoni.  Rais Francoise Hollande wa Ufaransa amesema kwenye taarifa yake Jumatatu, kwamba ni juu ya Waturuki wenyewe kuamua utaratibu wa kisiasa, lakini matokeo ya kura hiyo ya maoni yanaakisi namna taifa hilo lilivyogawika.Lakini ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema maamuzi ya kura hiyo ni jambo la ndani na Uturuki, na kwamba lazima yaheshimiwe.

Monday, April 17, 2017

ERDOGAN ASHINDA KURA YA MAONI WAPINZANI WADAI KULIKUWA NA UDANGANYIFU

Rais wa Uturuki Erdogan ameibuka mshindi katika kura ya maoni ya kihistoria Jumapili(16.04.2017) itakayoimarisha madarakani yake, na matokeo hayo yameiacha nchi hiyo ikigawanyika mno na upinzani unalalamikia udanganyifu.
Türkei Referendum Wahllokal in Istanbul Präsident Erdogan (Reuters/A. Konstantinidis) Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Mabadiliko  hayo  makubwa  ya  katiba  yaliyoidhinishwa  kupitia kura  hiyo  ya  maoni yanaunda  mfumo  wa  madaraka  ya  rais ambao  utampa  rais Erdogan  madaraka  zaidi  kuliko  kiongozi yeyote  tangu  muasisi  wa  Uturuki Mustafa Kemal Ataturk  na mrithi wake  Ismet Inonu.
Kambi  ya "ndio" imeshinda  kwa  asilimia  51.4 ya  kura  dhidi  ya asilimia  48.6 kwa  upande  wa  "hapana", tume  ya  uchaguzi imesema  katika  tarakimu  zilizonukuliwa  na  shirika  la  habari  la Anadolu, katika  zoezi  la  kuhesabu  kura  kwa  misingi  ya  asilimia 99.5 ya  masanduku  ya  kura. Watu waliojitokeza  kupiga  kura  ni asilimia  85.
Türkei Regierung erklärt Sieg bei Referendum (picture alliance/AA/H. Yaman ) Watu wakipunga bendera wakifurahia ushindi wa Erdogan
Matokeo  ya  kura  hiyo  pia  yanaathari  pana  kwa  Uturuki  ambayo imejiunga  na  jumuiya  ya  kujihami  ya  NATO mwaka  1952 na katika  kipindi  cha  mwisho  cha  nusu  karne  nchi  hiyo  imelenga katika  kujiunga  na  Umoja  wa  Ulaya.
Sherehe mitaani
Kundi  kubwa  la  watu  waliokuwa  wakipunga  bendera walisherehekea  ushindi  huo  mitaani, Erdogan  akiisifu  Uturuki kwa kuchukua "uamuzi  wa  kihistoria".
Türkei Referendum | Abstimmung (picture alliance/AA/E. Atalay) Mifuko ya kura kutoka katika vituo vya kupigia kura nchini Utruki
"Pamoja  na  umma, tumeweza  kufikia  mabadiliko  muhimu  katika historia  yetu," ameongeza.
Lakini  waungaji  mkono  wa upinzani  katika  wilaya  zinazompinga Erdogan  za  mjini  Istanbul  wameonesha  kutoridhishwa  kwa kupiga mabakuli  na  sufuria kwa  vijiko  na  umma  na  kufanya kelele  za  kupinga. Mamia  ya  watu  pia  waliingia  mitaani  katika maeneo  ya  Besiktas  na  Kadikoy.
Mkuu  wa  mamlaka  kuu  ya  uchaguzi  Sadi Guven  amethibitisha kwamba  kambi  ya  "ndio" imeibuka  mshindi, lakini  upinzani umeapa  kupinga  matokeo  hayo.
Kura  hiyo  ya  maoni  ilifanyika  chini  ya  amri  ya  hali  ya  hatari ambayo  imeshuhudia  watu  47,000 wakikamatwa  katika ukandamizaji  baada  ya  jaribio  lililoshindwa  la  mapinduzi  dhidi  ya Erdogan Julai  mwaka  jana.
Türkei Yildirim verkündet den Sieg der Ja-Sager (picture alliance/AA/A. Balikci) Waziri mkuu wa Uturuki na kiongozi wa chama tawala cha AKP Binali Yildirim
Mwishoni  mwa  kampeni iliyokuwa  na  hamasa  nyingi , kambi  ya "hapana" iliweza  kuongeza  idadi  ya  kura  wakati  kura  zaidi zikihesabiwa , baada  ya  kuwa  nyuma  kwa  muda  mrefu  katika matokeo  ya  awali, lakini  kambi  hiyo  ilishindwa  kuipita  kambi  ya kura  za  "ndio".
Wakati  huo  huo theluthi  mbili  ya  Waturuki  wanaoishi  nchini Ujerumani wamepiga  kura  zao  wakimuunga  mkono  rais Recep Tayyip Erdogan katika  kura  ya  maoni  inayotaka  kumpa  madaraka zaidi  rais. Asilimia  63.1  ya  wapigakura  Waturuki  nchini Ujerumani  wameunga  mkono  hatua  hiyo, limesema  shirika  la habari  la  Uturuki Anadolu  mapema  leo  Jumatatu.
Brexit-Hauptakteure - Jean-Claude Juncker (Getty Images/C. Court) Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker
Maoni ya viongozi mbali mbali
Taarifa ya  pamoja ya rais  wa  Halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya Jean-Calude Juncker  na  waziri  mwenye  dhamana  ya  masuala ya  kigeni  katika  Umoja  huo  Federica Mogherini  imesema , mabadiliko  ya  katiba  na  hususan utekelezaji  wake utatathminiwa kwa  misingi  ya  jukumu  la  Uturuki  kama nchi  inayotaka  kujiunga na  Umoja  huo  na  mwanachama  wa  baraza  la  Ulaya.

MAKUMI YA ASKARI WA SAUDIA WAANGAMIZWA NA WALENGA SHABAHA WA YEMEN

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa, walenga shabaha miongoni mwa jeshi la nchi hiyo na harakati ya Answarullah wamefanikiwa kuwaangamiza makumi ya askari wa Saudia katika mkoa wa Ma'rib, katikati mwa nchi hiyo.
Kikosi cha walenga shabaha katika jeshi la Yemen na harakati ya Answarullah kimetangaza kuwa, askari hao wa Saudia wameangamizwa katika operesheni iliyojiri katika eneo la al-Rabia, al Zughan, al Mashjah, al far'u, Kufal na al-Mukhadarah. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, askari wengine 11 wa Saudia wameangamizwa pia katika operesheni ya barabarani baada ya kutega bomu lililolipuliwa na jeshi la Yemen na kuwaangamiza askari hao vamizi karibu na kambi ya jeshi ya Habs, mkoa wa Jizan.
Askari vibaraka wanaoshiriki katika hujuma za Saudia Yemen baada ya kuuawa
Aidha askari mwingine wa gadi ya ulinzi wa mpakani na polisi watatu wote wa Saudia wameangamizwa kwa kupigwa risasi katika eneo la mpakani la Jizani baina ya nchi hiyo na Saudia. Katika hatua nyingine jeshi la Yemen na harakati ya wananchi limeshambulia eneo walipokusanyika askari vibaraka wa Saudia katika mji wa al-Mokha, mkoa wa Taiz na kuwasababishia hasara kubwa. Hii ni katika hali ambayo ndege za kivita za Saudia zimeshambulia maeneo ya raia ya Maqbanah, mkoa wa Taiz na kusababisha raia kadhaa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

WAISLAMU MAREKANI WAFANYA KONGAMANO KUBWA LA DINI TATU ZA MBINGUNI

Waislamu wa mji wa Baltimore, nchini Marekani wamefanya kongamano la 42 la kila mwaka la Waislamu wa nchi hiyo kwa kushiriki Waislamu elfu 20 kutoka maeneo mbalimbali ya taifa hilo.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Kiislamu ya (ICNA) nchini Marekani imetangaza kuwa, kongamano hilo la siku tatu limejadili kadhia ya 'Juhudi kwa ajili ya Mafanikio ya kweli na Ujumbe wa Mungu wa Musa, Issa na Nabii Muhammad (saw)' hapo mjini Baltimore katika jimbo la Maryland, mashariki mwa Marekani.
Watoto wa Kiislamu katika kikao hicho
Kadhalika ofisi ya Kiislalmu ya kaskazini mwa Marekani  (ICNA) imesisitiza kuwa, katika kongamano hilo kumefanyika pia vikao mbalimbali na kujadili masuala kama vile, kukabiliana na chuki dhidi ya dini ya Kiislamu, kutetea haki za Waislamu katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump, wa Marekani, ongezeko la jinai dhidi ya Waislamu na hatua hasi ya serikali ya rais huyo ya kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo.
Obama akiwa rais alipowatembelea Waislamu wa Baltimore, Marekani
Kadhalika Waislamu nchini Marekani wamepata kutoa malalamiko yao kuhusiana na matatizo mbalimbali yanayowakabili ndani ya taifa hilo hususan baada ya kuingia madarakani Rais Trump mwenye misimamo ya kibaguzi na chuki. Wakati huo huo, zaidi ya watu 1000 wasio na makazi walipatiwa misaada mbalimbali ikiwemo ya chakula, ambayo ilitolewa na kundi la wafuasi wa dini tatu za Uyahudi, Ukristo kwa kushirikiana na Waislamu wa Baltimore.