Hii leo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
yametimiza miaka 38 tangu yalipopata ushindi mwaka 1979. Tukio hilo
muhimu katika historia ya Iran na dunia nzima bado linapewa umuhimu
mkubwa na wanafikra na waandishi na limekuwa kigezo na ruwaza njema kwa
wapigania uhuru, haki na uadilifu kote duniani.
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulivuruga kabisa
mahesabu ya mabeberu na kutoa ilhamu ya darsa la kusimama kidete na
kupambana na dhulma na madola ya kidhalimu.
Mapambano ya wananchi wa Iran yalianza pale taifa lilipochukua uamuzi
wa kuwa huru na kujitawala kwa ajili ya maendeleo na ufanisi, suala
ambalo lilikwenda kinyume na maslahi na matakwa ya madola ya kibeberu.
Fikra ya harakati hiyo ya kimapinduzi ilivuka mipaka ya Iran na kuwa
kigezo bora cha kusimama kidete na chachu ya kukabiliana na madola
makubwa. Kwa sababu hiyo maadui wamezidisha njama za kutaka kuyabinya
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuzuia ujumbe wake wa kimataifa kwa
kutumia njia mbalimbali. Ni wazi kuwa, mpambano huo utaendelea kuwepo
maadamu taifa la Iran linaendelea kusimama kidete kwa ajili ya
kukabiliana na sera za kutaka makuu na kujipanua zaidi. Pamoja na hayo
kuna matatizo na vizingiti vingi katika njia hiyo ya mapambano dhidi ya
mabeberu kuanzia kwenye masuala ya kiuchumi hadi kwenye vitisho vya
mashambulizi ya kijeshi. Mapambano katika uwanja huu ni magumu sana na
yanahitaji azma kubwa, imani ya kweli na misimamo madhubuti. Vilevile
sharti la kufanikiwa katika mapambano hayo ni umoja na mshikamano.
Kwa miaka mingi sasa maadui wa taifa la Iran wameanzisha mashambulizi
makali ya kipropaganda na ya vyombo vya habari dhidi ya utawala wa
Kiislamu wa Iran tena kwa kutumia gharama kubwa ya fedha kwa lengo ya
kuficha mafanikio ya Iran ya Kiislamu na kudhihirisha baadhi ya nukta
hasi ili kuwakatisha tamaa na matumaini wananchi hususan tabaka la
vijana. Uadui huo unalenga msingi na utambulisho wa utawala wa Kiislamu.
Uhasama na uadui huo daima umekuwa ukionekana katika matamshi na
vitendo vya viongozi wa serikali ya Marekani. Kama alivyosema Kiongozi
wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ali Khamenei kwamba,
mwenendo huo unaonesha kuwa, dhati ya Marekani haibadiliki, na kwamba
hakuna tofauti yoyote baina ya serikali za Wademocrat na zile za
Warepublican katika kulifanyia uadui taifa la Iran na Waislamu kwa
ujumla.
Wachambuzi na wanadharia wengi mashuhuri duniani wanakubaliana
kwamba, licha ya kupita karibu miongo minne sasa ya uhai wake, Mapinduzi
ya Kiislamu ya Iran hayajatengana na kuachana na malengo na thamani
zake za awali licha ya vizingiti, mikingamo na uhasama wa Marekani na
mabeberu wenzake na kwamba, taifa la Iran lingali linasonga mbele katika
safu moja na yenye mshikamano. Kwa mshikamano na umoja huo Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran imeweza kuthabitisha nafasi yake katika eneo la
Mashariki ya Kati na duniani licha ya kuwepo mashinikizo na njama nyingi
kuanzia vita vya kulazimishwa, mzingiro wa kiuchumi na vikwazo vya
pande zote vya kidhalimu. Hii ina maana kwamba, kusimama kidete kwa
taifa la Iran mbele ya madola ya kibeberu si nara na maneno matupu.
Watu wanaoelewa vyema fikra za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran
wanajua kuwa mahudhurio na kushiriki kwa mamilioni ya wananchi katika
maandamano ya leo ya kuadhimisha ushindi wa mapinduzi hayo ni tangazo za
kushikamana wananchi na malengo, fikra na sera za Mapinduzi ya Kiislamu
na mwasisi wake hayati Imam Ruhullah Khomeini na ni dhihirisho la
kuendelea kusimama kidete kwa taifa la Iran mbele ya uadui na njama za
mabeberu wa dunia ya leo. Ujumbe wa maandamano ya mamilioni ya Wairan
hii leo pia ni jibu kwa vitisho, bwabwaja na eti 'machaguo yaliyo juu ya
meza' ya viongozi wa White House.
No comments:
Post a Comment