Taasisi tano za kimataifa zimetahadharisha juu ya kushadidi vitendo vya ukatili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Asasi hizo ukiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja
wa Ulaya zimetoa ripoti ambayo pia imetiwa saini na jumuiya za kiuchumi
za katikati mwa Afrika na Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Lugha ya
Kifaransa (Francophone), zikiyataka makundi yanayohusika katika
mapigano nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kuhitimisha hitilafu zao mara
moja.
Katika ripoti hiyo taasisi hizo zimeonya pia kwamba kila shambulizi
litakalowalenga raia wa kawaida, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na
asasi za kiraia nchini humo, litafuatiliwa kisheria katika vyombo vya
mahakama. Kwa upande mwingine asasi hizo zimepongeza askari wa kofia ya
buluu wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa MINUSCA katika kuwalinda
raia kunako hujuma za makundi ya waasi nchini humo. Aidha zimelaani
vikali hujuma na uharibifu uliowakumba raia na kuwafanya kuwa wakimbizi
ndani na nje ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ni vyema kuashiria kwamba, Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni kati
ya nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa
mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi
hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka nchini humo.
Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila
uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na
lile la Seleka.
No comments:
Post a Comment