Jamii ya kimataifa imebainisha wasiwasi wake
kuhusu kuwepo mkwamo katika mazungumzo ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa
katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika taarifa ya pamoja jumuiya za kimataifa zikiwemo Umoja
wa Afrika AU, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya EU na Jumuiya ya
Kimataifa ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa IOF zimesema zinahofu
kuhusu kuendelea kwa mkwamo kwenye mjadiliano ya kisiasa miongoni mwa
wadau nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuhusiana na
utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa yaliyoafikiwa Desemba 31 mwaka
jana.
Mashirika hayo manne yamesema yamebaini kwamba wiki sita baada ya
makubaliano ya kipindi cha mpito ili kuelekea kufanya uchaguzi huru wa
amani na haki Desemba 2017, pande husika bado hazijakamilisha
majadiliano ya utekelezaji wa mkataba.
Yameongeza kuwa hali hiyo inaweza kutia dosari nia njema iliyopelekea kutiwa saini makubaliano mwezi Desemba mwaka jana.
Hivyo mashirika hayo yametoa wito kwa wadau wote nchini DRC ikiwa ni
pamoja na upande wa serikali na wapinzani kuongeza maradufu juhudi kwa
nia njema ili kuharakisha na kukamilisha majadiliano yanayoendelea,
kwani wamesema kuna haja ya pande zote kushikamana katika mchakato wa
upatanishi na kuhakikisha makubaliano ya 31 Desemba yanatekelezwa kwani
ni muhimu sana kabla ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment