Upinzani dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri
Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeongezeka sana hivi sasa. Mamia
ya wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu wanaendelea
kuandamana wakimshikinikiza Netanyahu ajiuzulu.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni
hadi sasa ameshasailiwa mara kadhaa kutokana na kuhusika kwenye
ubadhirifu wa fedha ndani ya utawala wa Kizayuni. Kushindwa siasa za
Netanyahu katika miaka ya hivi karibu pamoja na vitendo vyake vya
ufisadi kama walivyo viongozi wengine wa Israel, kumeshadidisha migogoro
ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya utawala wa Kizayuni. Jambo
hilo aidha limewafanya wakazi wa utawala wa Kizayuni wafanye maandamano
ya mara kwa mara kuwalaani viongozi wa Israel. Waandamanaji hao
wanamlalamikia vikali Netanyahu na kutaka kundolewa kinga yake ya
kutoshtakiwa.
Waziri Mkuu wa Israel anashutumiwa
kupokea hongo ya mamilioni ya dola za Kimarekani kupitia mkataba
uliotiwa saini baina ya Israel na shirika moja la Ujerumani, wa kuuziwa
nyambizi utawala huo dhalimu. Aidha Netanyahu anashutumiwa kwa kumpigia
simu mmiliki wa gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot na kutaka kumpa
rushwa ili gazeti hilo lilinde manufaa ya Netanyahu na limsaidie kubakia
madarakani.
Maandamano hayo makubwa ya Wazayuni
yanafanyika katika hali ambayo, kwenye miezi ya hivi karibuni, kumezuka
vita vikubwa vya kugombea madaraka na kutoa hongo za kisiasa na kiuchumi
baina ya wanasiasa wa Israel. Jambo hilo linabainisha kwamba, utawala
wa Kizayuni unakaribia kutumbukia kwenye wimbi jipya za mizozo ya
kisiasa.
Baadhi ya wabunge wa utawala wa Kizayuni
wamekuwa wakitoa matamshi mbalimbali ya kumlaumu vikali Netanyahu na
wanamuona ni Waziri Mkuu asiye na uwezo wa kuongoza serikali. Hivi sasa
wimbi la mizozo ndani ya utawala wa Kizayuni imezidi kuvidhoofisha vyama
vikuu vya utawala huo pandikizi kikiwemo chama cha Likud kinachoongozwa
na Benjamin Netanyahu. Sambamba na kupamba moto mashinikizo ya kumtaka
Benjamin Netanyahu angóke madarakani, vita vya maneno na malumbano ya
kisiasa yameongezeka pia kati ya viongozi wa Israel. Upinzani unaozidi
kuongezeka dhidi ya Benjamin Netanyahu na masuala mengine mbalimbali
ikiwemo kufuatiliwa kesi tofauti zikiwemo za ufisadi wa Benjamin
Netanyahu, kunatilia nguvu mtazamo kwamba, Waziri Mkuu huyo wa Israel
amekaribia kungólewa madarakani na kumalizika umri wake wa kisiasa.
Vile vile kuendelea utawala wa Kizayuni
kukumbwa na migogoro tofauti kunazidi kuonesha kukaribia mwisho mbaya wa
utawala huo pandikizi. Wakazi wa utawala wa Kizayuni wanaonesha wazi
kuwa wamechoshwa na viongozi wa utawala huo ambao wananuka ufisadi wa
kila namna. Kila leo wakazi hao wanazidi kuonesha hasira zao kwa njia
tofauti ikiwa ni pamoja na hata kujichoma moto.
Wimbi la malalamiko ya wakazi wa utawala
wa Kizayuni dhidi ya siasa za viongozi wa Israel ni ushahidi mwingine
unaoonesha wimbi kubwa la migogoro ndani ya utawala ghasibu wa Israel.
Uhakika mwingine ni kuwa migogoro hiyo haitarajiwi kumalizika katika
siku za karibuni bali inaongezeka sekunde baada ya sekunde nyingine. Ni
kwa kuzingatia yote hayo ndio maana wachambuzi wa masuala ya kisiasa
wakauita mwaka huu wa 2017 kuwa ni mwaka wa kupamba moto na kushadidi
migogoro ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
No comments:
Post a Comment