Friday, February 24, 2017

MAPIGANO YA KIKABILA YA UMWAGAJI DAMU MASHARIKI MWA KONGO

Makumi ya watu wameuawa hadi sasa tangu kuanza tena mapigano katika mkoa wa Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Julai mwaka jana.
Richard Ngoie Kiatngala, Gavana wa mkoa wa Tanganyika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  amesisitiza wakati wa kuanza kikao cha kujadili amani na suluhu kati ya makabila ya Luba (Bantu) na Pygmees kuwa, katika mapigano hayo watu 150 wameuawa hadi sasa, 200 wamejeruhiwa, shule 400 zimebomolewa na vijiji 422 kuchomwa moto. Gavana huyo wa mkoa wa Tanganyika ameongeza kuwa kesi 200 za ubakaji zimethibitishwa kutokea kufuatia mapigano hayo ya kikabila; huku asilimia 76.4 ya wakazi wa mkoa wa Tanganyika wakikabiliwa na uhaba wa chakula na mlipuko wa maradhi ya kipindupindu na surua. 
Watu wa kabila la Pygmees wanaodaiwa kuvichoma moto vijiji vya jamii ya Luba  
Gavana wa mkoa wa Tanganyika ametaka kurejeshwa haraka amani na utulivu katika mkoa huo. Wakati huo huo Emmanuel Ramazani Shadary Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa hali ya mkoa wa Tanganyika inatia wasiwasi na kuzitolea mwito pande zinazozozana kufanya mazungumzo. Mkoa wa Tanganyika umekumbwa na mapigano ya umwagaji damu baina ya makabila mawili ya Luba na Pygmees tangu miezi kadhaa iliyopita hadi sasa.

No comments:

Post a Comment