Sunday, November 19, 2017

KUSAMBARATISHWA KIKAMILIFU DAESH (ISIS) NCHINI IRSQ

Kusambaratishwa kikamilifu DAESH (ISIS) nchini Iraq
Mabadiliko yanayojiri kwenye medani za vita nchini Iraq yanabainisha kusambaratishwa na kutokomezwa Daesh (ISIS) nchini humo; na kushindwa kikamilifu kundi hilo la kigaidi na kitakfiri ambako ni sawa na kupata mafanikio makubwa Wairaqi katika mapambano dhidi ya magaidi kumeakisiwa sana na duru mbalimbali za habari.
Vikosi vya jeshi la Iraq siku ya Ijumaa viliukomboa mji wa Rawah kutoka kwenye makucha ya magaidi wa Daesh. Kufuatia kukombolewa mji huo kulikochukua muda wa saa kadhaa tu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq Qasim Al-Araji alitangaza kuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limesha sambaratishwa kikamilifu nchini humo. Rawah ilikuwa miongoni mwa ngome za mwisho za Daesh ndani ya ardhi ya Iraq. Hivi sasa magaidi wa kundi hilo la ukufurishaji hawana mji mwengine wowote muhimu wa Iraq wanaoushikilia na kuukalia kwa mabavu isipokuwa wanaishia kuzunguka zunguka na kuranda randa kwenye maeneo ya mbali na katika baadhi ya vijiji.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iraq, Qassim Al-Araji
Mnamo mwaka 2014, kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na wa Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh liliishambulia Iraq, likayavamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo. Lakini tangu wakati huo hadi sasa, jeshi la Iraq lilkisaidiwa na vikosi vya kujitolea vya wananchi limeweza kuyakomboa maeneo hayo kutoka kwenye makucha ya kundi hilo; na kimsingi kundi hilo limeshasambaratishwa kikamilifu nchini humo.
Wapiganaji wa jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi
Hata hivyo baada ya kushindwa kijeshi kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, suali la kujiuliza hivi sasa ni je, kwa ushindi huo, Wairaqi sasa wataweza kupumua na kupata salama ya kuepukana na shari ya ugaidi? Au kundi hilo la kigaidi na kitakfiri litaanzisha mbinu nyengine mpya na kuendelea kuwaandamana wananchi wa Iraq kwa hujuma na jinai zake za kinyama? Kwa kuzingatia kuwa mashambulio ya kigaidi yalishadidi hivi karibuni katika nchi za Iraq na Syria, tunaweza kusema kuwa baada ya kushindwa kijeshi na kupoteza maeneo waliyokuwa wakiyashikilia kwa mabavu, magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wameshaainisha mkakati wanaokusudia kuutekeleza mnamo siku zijazo. Ili kufifisha kushindwa kwake kijeshi, kundi la Daesh (ISIS) limeanzisha mbinu na mkakati wa kuvuruga usalama, kwa kushadidisha mashambulio ya kujitoa mhanga ya miripuko ya mabomu pamoja na mauaji ili kuvuruga amani na uthabiti nchini Iraq, sambamba na kupanua wigo wa harakati zake katika nchi nyengine ikiwemo Afghanistan, Libya na kwengineko. Harakati za aina hiyo ni muendelezo wa njia na misimamo ya kufurutu mpaka iliyoanzishwa mwaka 2004 na Abu Mus'ab Az-Zarqawi kwa njia ya kuanzisha mauaji na kuwalenga raia; na baada ya kushadidi hitilafu baina ya Wairaqi ikaandaa mazingira ya kuzaliwa Daesh kutoka kwenye tumbo la Al-Qaeda na kupelekea hatimaye mwaka 2014 kushambuliwa na kukaliwa kwa mabavu kirahisi miji mbalimbali ya ardhi ya Iraq.
Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh
Leo hii baada ya miaka mitatu ya vita na mapigano makali ya kujitolea mhanga, yaliyowagharimu roho nyingi za watu na kuwasababishia pia uharibifu mkubwa, Wairaqi wameweza kuyakomboa maeneo yote ya ardhi yao yaliyokuwa yamevamiwa na kushikiliwa kwa mabavu na Daesh; hata hivyo ushindi huo wa kijeshi dhidi ya magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka sio mwisho wa mapambano, bali inapasa ifanyike kazi ya kuing'oa na kuitokomeza mizizi ya misimamo hiyo hatari. Katika hali kama hiyo, inavyoonekana, baada ya kulisambaratisha kijeshi kikamilifu kundi la Daesh nchini Iraq, vita na mapambano yajayo yatakuwa ni ya kitaarifa na kiintelijinsia ambayo hayatotegemea askari na vifaru pekee; bali yatategemea zaidi unasaji wa taarifa za kiintelijinsia. Katika mazingira ya sasa ambapo magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wamesha sambaratishwa kikamilifu nchini Iraq, Marekani, ambayo inahisi njama na mipango yake iliyokuwa imepanga dhidi ya Iraq na eneo kwa jumla imevurugika, hivi sasa inashughulika kupanga njama na mikakati mingine mipya ya kiadui. 
Mji wa Rawah uliokuwa ngome ya mwisho muhimu ya Daesh nchini Iraq
Ukweli ni kwamba kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limeshafutwa kwenye ramani ya Iraq, na hilo limewezekana kwa baraka na nafasi ya uongozi wa juu wa kidini na kwa kujitolea mhanga vikosi vya Iraq hususan vya jeshi la kujitolea la wananchi la Al Hashdu-Sha'abi. Na hii ni katika hali ambayo jeshi hilo la wananchi lingali linaendelea kuandamwa na njama na tuhuma za Marekani. Kutokana na matukio yaliyojiri huko Iraq wananchi wanapaswa kuwa macho zaidi katika kipindi kinachoanza hivi sasa cha baada ya kusambaratishwa Daesh nchini humo.../

WAFUNGWA WA KISIASA BAHRAIN WAZUILIWA KUWA NA MAWASILIANO YOYOTE NA NJE YA JELA

Wafungwa wa kisiasa Bahrain wazuiliwa kuwa na mawasiliano yoyote na nje ya jela
Duru zenye uhusiano na familia ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya al-Wifaq nchini Bahrain, zimeeleza kuwa utawala wa Aal-Khalifa umemwekea vizuizi vikubwa Sheikkh Ali Salman na shakhsia wengine mashuhuri wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa habari hiyo, Sheikh Ali Salman na shakhsia wengine wakubwa wanaoshikiliwa katikka jela za Bahrain wamezuiliwa kufanya mawasiliano na watu wa familia zao, kupiga simu au hata kusoma magazeti. Katika kuendelea kutolewa hukumu za kidhalimu za utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Sheikh Ali Salman anayeendelea kutumikia kifungo cha miaka tisa jela, utawala huo umewasilisha mahakamani mashitaka mapya dhidi ya shakhsia huyo ya kile kinachotajwa kuwa eti ni kufanya ujasusi kwa maslahi ya Qatar.
Shakh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya al-Wifaq nchini Bahrain
Katika uwanja huo, mwendesha mashtaka wa Manama amewasilisha mashtaka hayo dhidi ya Sheikh Ali Salman, Hassan Sultwan na Ali al-Usud, ambao nao pia ni wanachama wa Jumuiya ya Kitaifa ya al-Wifaq kwa tuhuma hizo hizo za kufanya ujasusi kwa ajili ya Qatar kwa lengo la kile alichokisema kuwa eti ni kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Bahrain. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hukumu dhidi ya shakhsia hao itatolewa tarehe 27 Novemba mwaka huu.
Maandamano ya Wabahrain
Sheikh Ali Salman alikamatwa mwaka 2014 na utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela mwaka 2015 kwa tuhuma za uchochezi na kuivunjia heshima Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Hata hivyo mahakama ya rufaa ya nchi hiyo na katika njama za kutaka kumfunga miaka mingi zaidi shakhsia huyo ilimbadilishia mashitaka na kuyafanya ya tuhuma za kutaka kubadilisha utawala na hivyo ikamuhukumu kifungo cha miaka tisa jela.

Saturday, November 18, 2017

VELAYATI AMUONYA RAIS WA UFARANSA ASIINGILIE MAMBO YA IRAN

Velayati amuonya Rais wa Ufaransa asiingilie mambo ya Iran
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amemuonya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa asiingilie masuala ya ndani ya Iran kwani kujiingiza katika masuala yasiyomuhusu hakuna faida kwa nchi yake.
Ali Akbar Velayati amesema hayo leo wakati alipohojiwa na shirika la habari la IRIB na sambamba na kumlaumu Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kuingilia masuala ya ulinzi ya Iran amesema, kitendo cha Paris cha kujiingiza katika suala la makombora ambalo ni la kiistratijia kwa Iran hakina matunda yoyote isipokuwa kuzidi kujipotezea heshima Ufaransa mbele ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesisitiza kuwa, Iran haiombi idhini ya mtu yeyote katika masuala yake ya kiulinzi na kusema wazi kwamba, kama Ufaransa inataka kuwa na uhusiano mzuri na Iran basi inapaswa iache kujiingiza katika masuala yake ya ndani kwani ni kinyume na maslahi ya kitaifa ya Ufaransa.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Amesisitiza kuwa, bila ya shaka yoyote majibu ya Iran kuhusu mwito wa Ufaransa juu ya mradi wake wa makombora ni hapana na hakuna hata uwezekano wa asilimia moja wa kukubaliana na jambo hilo.
Jana Ijumaa, Rais wa Ufaransa alidai eti kuna haja kwa Iran kuweka wazi stratijia zake za mradi wa makombora ya balestiki na kudai kuwa Iran inapaswa kuachana na siasa zake alizoziita eti ni za mashambulizi.
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amemjibu rais huyo wa Ufaransa na kumuonya asiingilie masuala ya ndani ya Iran kwani kila nchi ina haki ya kujilinda na kwamba nchi yoyote ile haina haki ya kuipangia itumie stratijia gani katika kuimarisha nguvu zake za ulinzi. 

Friday, November 17, 2017

UMASIKINI UNACHOCHEA MIMBA ZA UTOTONI TANZANIA

Utafiti: Umasikini unachochea mimba za utotoni Tanzania
Imeelezwa kuwa, umasikini na kipato cha chini cha baadhi ya familia nchini Tanzania ndicho chanzo cha mimba za utotoni katika jamii ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti katika warsha ya siku moja ya kutambulisha mradi na shirika hilo kwa wadau iliyofanyika mkoani Dodoma. Kwa mujibu wa shirika hilo, utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa kusaidiana na mashirika mengine, umebaini kwamba, umasikini wa familia husababisha familia zenye maisha magumu kupambana kwa bidii kutafuta chakula na mavazi ya watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jukwaa la Utu wa Mtoto ameeleza kuwa, utafiti wa Demografia ya Afya Tanzania wa 2016 (TDHS) unaonesha kwamba, asilimia 36 ya wasichana wa umri wa kati ya miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikia miaka 18. 
Maandamano ya kupinga ndoa za utotoni nchini Nigeria
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kumekuweko na kampeni ya kimataifa ya kukabiliana na ndoa za utotoni hasa barani Afrika.
Mwezi uliopita nchi ya Senegal ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliokuwa na lengo la kuongeza hatua za kutokomeza ndoa za utotoni katika nchi za Afrika Magharibi na Kati. Inaelezwa kuwa, wazazi ambao hali zao ni duni kimaisha, mara nyingi huwaozesha watoto wao mapema ili kupunguza mzigo wa ulezi, wakati huo huo, baadhi ya mila na desturi zinatajwa kuwa nazo zina mchango katika hilo.

Thursday, November 16, 2017

WAMAREKANI WAZIDI KUPIGANA RISASI KIHOLELA, MAKUMI WAUAWA NA KUJERUHIWA

Wamarekani wazidi kupigana risasi kiholela, makumi wauawa na kujeruhiwa
Watu 16 wameuawa na wengine 24 kujeruhiwa katika matukio 56 ya kupigana risasi kiholela yaliyotokea katika kipindi cha masaa 24 kwenye maeneo tofauti ya Marekani.
Kituo cha kutoa takwimu za mashambulizi ya silaha nchini Marekani kimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa mauaji na mashambulizi hayo yametokea katika kipindi cha masaa 24 yaliyopoita katika majimbo ya Florida, Michigan, Texas, Ohio na Pennsylvania. 
Kwa mujibu wa kituo hicho cha Marekani, katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita, kumeripotia matukio 164 ya kupigana risasi kiholela katika kona mbalimbali za Marekani ambayo yamepelekea watu 45 kuuawa na wengine 88 kujeruhiwa.
Umilikaji silaha ovyo, mgogoro mkubwa kwa Marekani

Takwimu zinaonesha kuwa, jamii ya Marekani ndiyo yenye silaha nyingi zaidi zinazomilikiwa na watu majumbani kuliko jamii nyingine yoyote duniani kiasi kwamba kati ya kila watu 100, 90 kati yao wana silaha nyepesi majumbani mwao.
Takwimu zinaonesha pia kuwa makundi ya utengenezaji silaha yana nguvu sana nchini Marekani na ndiyo yanayodhibiti vyama vya Democrats na Republican, hivyo serikali yoyote inayoingia madarakani haina nguvu ya kupiga marufuku umilikaji silaha ovyo nchini Marekani.

TAHARUKI ZIMBABWE, MUGABE ANG'ANG'ANIA MADARAKA, AU NA UN ZATOA KAULI

Taharuki Zimbabwe, Mugabe ang'ang'ania madaraka, AU na UN zatoa kauli
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye yuko katika ncha ya kuuzuliwa amekataa kuachia madaraka akisisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi halali wa nchi hiyo.
Duru za habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Mugabe amekataa upatanishi wa Askofu wa Kanisa Katoliki nchini humo Fidelis Mukonori, ambaye alikuwa anaongoza mazungumzo kati ya rais huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 93 na makamanda wa jeshi la nchi hiyo.
Jeshi hilo jana lilitangaza kuwa Mugabe na familia yake wako kwenye kizuizi cha nyumbani na kuongeza kuwa litawapandisha kizimbani wale liliowataja kama "wahalifu" waliomzunguka kiongozi huyo ambao wameisababishia nchi hiyo madhara na hasara za kiuchumi na kijamii.
Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefutwa kazi na kukimbilia uhamishoni
Wakati huo huo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake, Farhan Haq amezitaka pande zote husika kujizuia kuchua hatua inayoweza kuvuruga mambo zaidi, na kusisitiza kuwa mgogoro uliopo unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa na mazungumzo.
Naye Mkuu wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde ambaye pia ni Rais wa Guinea amesema AU inalaani vikali hatua ya majenerali wa jeshi la Zimbabwe kutwaa madaraka kwa nguvu na kusisitiza kwamba mfumo wa katiba unapaswa kuheshimiwa na pande zote.
Huku hayo yakiarifiwa, Morgan Tsvangirai, kinara wa upinzani nchini Zimbabwe amerejea nchini akitokea Afrika Kusini, kufuatia kile kinachotajwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagikaji wa damu.
Morgan Tsvangirai
Kwa mujibu wa gazeti la NewsDay la Zimbabwe, Tsvangirai ametangaza kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyepigwa kalamu nyekundu na Mugabe hivi karibuni, kuhusu uundwaji wa serikali ya mpito.

Monday, October 30, 2017

WATU 5 WAUAWA KATIKA MAANDAMANO DHIDI YA SERIKALI MJINI GOMA, KONGO DR

Watu 5 wauawa katika maandamano dhidi ya serikali katika mji wa Goma, Kongo DR
Maandamano ya wananchi ya kupinga serikali yaliyozusha makabiliano baina yao na polisi jana Jumatatu katika wilaya za Madjengon na Mabanga katika mji wa Goma mkoani Kivu ya Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesababisha vifo vya watu watano.
Maandamano hayo ambayo yalijiri jana jioni yaliitishwa na makundi ya wanaharakati wa kupigania demokrasia na mengineyo kama sehemu ya mgomo mkubwa unaoshinikiza kuondoka madarakani Rais Joseph Kabila na kudhihirisha hasira za wananchi kwa kushindwa kuendeshwa uchaguzi wa rais huko Kongo ili kumchagua rais mpya. Waandamanaji walichoma moto matairi ya gari na hivyo kusababisha msongamano wa magari katika barabara za mji wa Goma. Maandamano mengine kama hayo yanatazamiwa kufanywa siku chache zijazo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 
Mgogoro wa kisiasa Kongo DR umesababishwa na hatua ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kukataa kuachia madaraka baada ya muhula wake kumalizika mwezi Disemba mwaka jana. Uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika nchini humo kabla ya kumalizika mwaka huu chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Kinshasa na mrengo wa upinzani. Hata hivyo imeelezwa kuwa kushindwa kutekelezwa hatua hiyo si jambo la kushangaza kwa kuzingatia kuwa Tume ya Uchaguzi ya Kongo mwezi Julai mwaka huu ilitangaza kuwa kuna uwezekano uchaguzi huo usifanyike mwaka huu kutokana na kuwepo matatizo ya bajeti na kuendelea machafuko nchini humo.

UHURU KENYATA ATANGAZWA RASMI MSHINDI WA UCHAGUZI WA RAIS KENYA ULIOSUSIWA NA MPINZANI WAKE

Uhuru Kenyatta atangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa rais Kenya uliosusiwa na mpinzani wake
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya IEBC Wafula Chebukati amemtangaza Uhuru Kenyatta, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Jubilee Rais mteule na mgombea wake mwenza William Ruto kuwa Naibu Rais mteule baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa marudio wa rais uliofanyika siku ya Alkhamisi.
Akitangaza matokeo hayo jioni ya leo, Chebukati alisema uchaguzi huo ulikuwa huru, halali na wa haki.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti huyo wa IEBC, Kenyatta amejinyakulia kura 7,483,895 ambazo ni sawa na asilimia 98.27 ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi huo wa rais ambao ulisusiwa na mpinzani wake mkuu Raila Odinga.
Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati
Zoezi la kutangaza matokeo limefanyika bila kujumuisha majimbo 25 ya mkoa wa Nyanza ambayo yalishindwa kupiga kura siku ya Alkhamisi kutokana na fujo na machafuko yaliyokwamisha upigaji kura katika majimbo hayo.
Chebukati amesisitiza kuwa masharti yaliyokuwa yamewekwa na Mahakama ya Juu iliyofuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 kwa ajili ya uchaguzi wa marudio yametekelezwa, hivyo uchaguzi huo ni halali, huru na wa haki.
Aidha amesema uchaguzi wa marudio wa rais umeendeshwa na timu mpya iliyojumuisha wafanyakazi wa IEBC kutoka kila pembe ya nchi. Ameongeza kuwa hali katika majimbo 25 ya mkoa wa Nyanza ilisababisha uchaguzi ushindwe kufanyika katika maeneo hayo.
Akizungumza mapema leo, Naibu Mwenyekiti wa IEBC Consolata Nkatha alisema kura za maeneo ambayo uchaguzi haukufanyika hazitoathiri matokeo rasmi ya uchaguzi huo.
Raila Odinga
Mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani wa NASA Raila Odinga alisusia uchaguzi wa marudio akitaka pamoja na mambo mengine kutimuliwa maafisa waandamizi wa tume ya uchaguzi na kubadilishwa wachapishaji wa karatasi za kupigia kura na watayarishaji wa teknolojia itakayotumika katika mchakato wa uchaguzi huo.
Hayo yanajiri huku Wakenya wakisubiri kwa hisia tofauti msimamo wa kiongozi huyo wa upinzani ambao ameahidi kuutangaza baada ya rais Kenyatta kutangazwa rasmi mshindi wa uchaguzi wa marudio.../

Saturday, October 28, 2017

WAFUNGWA ZAIDI YA ELFU MOJA WA JELA YA TORA MISRI WAANZA MGOMO WA KULA

Wafungwa zaidi ya elfu moja wa jela ya Tora Misri waanza mgomo wa kula
Wafungwa wa jela yenye ulinzi mkali ya Tora mjini Cairo Misri wameanza mgomo wa kula chakula wakipinga mazingira mabaya yanatotawala jela hiyo.
Zaidi ya wafungwa elfu moja wa jela hiyo maarufu kwa jina la Jela la Nge wamenza mgomo wa kula wakilalamikia kunyimwa haki zao za kimsingi ikiwa ni pamoja na kuzuiwa jamaa zao kuwatembelea, kunyimwa huduma za afya na kadhalika.
Wakili Usama Biyumi anayeshughulikia kesi za wafungwa kadhaa wa jela hiyo amesema kuwa, ukatili wa idara ya jela hiyo dhidi ya wafungwa unaongezeka siku baada ya siku licha ya matakwa ya kukomeshwa mienendo hiyo.
Anesema kuwa maafisa wa jela hiyo wamekuwa wakizuia kuingizwa chakula kwa wafungwa na kupewa vyakula visivyokuwa salama.
Familia za wafungwa mbele ya jela ya Tora, Cairo
Biyumi ameongeza kuwa, mgomo huo ulianzishwa siku kadhaa zilizopita na baadhi ya wafungwa, na wafungwa wengine wa jela hiyo wamejiunga na wenzao hao baada ya matakwa yao kukataliwa na idara ya jela hiyo.
Wafungwa wa jela hiyo wananyimwa haki za kimsingi na manyanyaso yanashadidi zaidi kwa wafungwa wa kisiasa ambao wanashikiliwa katika seli zenye giza totoro na wanazuiwa kuzungumza na wenzao.
Misri imekuwa ikikosolewa na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kutoka na ukatili na manyanyaso yanayofanywa dhidi ya wafungwa katika jela za nchi hiyo. 

MAGHALA YA NYUKLIA YA MAREKANI; CHANZO CHA UKOSEFU WA AMANI DUNIANI

Maghala ya nyuklia ya Marekani; chanzo cha ukosefu wa amani duniani
Makamu wa Rais wa Marekani ameyataja maghala ya silaha za nyuklia za nchi hiyo kuwa suala linalopelekea kuwepo amani duniani.
Akiwa ziarani kukitembelea kituo cha jeshi la anga cha Minot, Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani amesema hakuna nguvu duniani inayopelekea kuwepo amani sawa na maghala ya silaha za nyuklia za Marekani. 
Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani 
Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo Marekani inatambulika ulimwenguni kama nchi pekee inayotumia silaha za nyuklia vitani. Miaka 70 iliyopita Wamarekani waliishambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Hiroshima na Nagasaki huko Japan na kusababisha vifo vya  raia wa nchi hiyo zaidi ya laki tatu baada ya kupitia mateso na masaibu chungu nzima. Kabla ya wakati huo, hakukuwa na silaha yoyote ya kivita iliyotengenezwa na binadamu iliyosababisha mauaji ya kutisha kama hayo. Mashambulizi hayo ya nyuklia yalizua hofu kubwa duniani kwa kadiri kwamba kwa mara ya kwanza katika historia, mwanadamu alikumbwa na wasiwasi wa kuangamizwa dunia nzima. 
Sehemu ya mji wa Hiroshima ulivyosambaratishwa na mashambulizi ya nyuklia ya Marekani 
Miaka minne tu baada ya Marekani kufanya mashambulio hayo ya nyuklia huko Japan, Umoja wa Kisovieti ulilifanyia jaribio bomu lake la kwanza la nyuklia na ni baada ya hapo ndipo kukaanza zama za ushindani wa silaha za nyuklia duniani. Ushindani huo mkubwa uliendelea na kuzifanya nchi mbili za Marekani na Urusi ya zamani mwezi Oktoba mwaka 1962 kukaribia kupigana vita vya nyuklia. Wakati huo kama Urusi ya zamani isingezirejesha karibu na Cuba meli zake zilizokuwa zimebeba makombora ya nyuklia, labda Rais wa wakati huo wa Marekani John F. Kennedy  angeamuru kupiganwa vita vya nyuklia; vita ambavyo katika masaa yake ya awali vingeweza kuua kwa uchache watu milioni 400. Marekani pekee hivi sasa imerundika katika maghala yake ya silaha, silaha za nyuklia ambazo zina uwezo wa kuiharibu dunia mara kadhaa. Hata kama Marekani katika miaka 70 iliyopita haijatumia silaha za aina hiyo, lakini imehusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja katika kuenea kwa silaha hizo hatari. Dunia sasa inahofia makabiliano ya kinyuklia kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini ambayo yanaweza kusababisha maafa makubwa kati ya pande mbili. 
Hasa ikitiliwa maanani kuwa amani ya dunia anayoikusudia Pence haitokani na uadilifu na ridhaa ya jamii, bali inatokana hofu ya Marekani kutekeleza mashambulizi ya nyuklia dhidi ya nchi nyingine. Kuwepo hofu na wasiwasi wa kusambaratika kikamilifu madola makubwa duniani miaka 70 baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kumezuia kuibuka migogoro kati ya madola hayo. Wakati huohuo nchi zilizokuwa zikimiliki nguvu za nyuklia kama Marekani zilihamisha uhasama na mashindano yao ya kijeshi kutoka ndani ya ardhi za nchi hizo na kuyahamishia katika maeneo yaliyobaki nyuma kimaendeleo na yale yaliyokuwa yakistawi huko Asia, Afrika na Amerika ya Latini. Watu wa maeneo hayo walipoteza maisha na kugharimika pakubwa kufuatia vita hivyo baina ya madola makuu duniani. Kwa ibara nyingine ni kuwa, amani iliyoipata Marekani kwa silaha zake za nyuklia na waitifaki wake wa Ulaya haijakuwa na natija nyingine ghairi ya kusababisha vita na umwagaji damu katika maeneo mengine ya dunia

HALI YA KIBINADAMU YEMEN INASHTUA, SAUDIA YAENDELEZA HUJUMA

Hali ya kibinadamu Yemen inashtua, Saudia yaendeleza hujuma
Mkuu wa misaada ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa amesema hali ya kibinadamu nchini Yemen ni ya kushtua huku Saudi Arabia ikiendeleza hujuma dhidi ya nchi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a, Mark Lowcock ambaye Jumamosi ya leo amemaliza safari ya siku tano nchini Yemen amesema kuwa, njia pekaa ya kumaliza vita Yemen ni kupitia mchakato wa kisiasa.
Lowcock amesema hali ya kibinadamu inazidi kuzorota huku ugonjwa wa kipindupindu ukienea kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa duniani. Amesema Yemen inakabiliwa na ukosefu mkubwa zaidi wa chakula duniani na kwamba idadi kubwa ya watu wamelazimika kuwa wakimbizi.
Watoto ni waathirika wa hujuma ya Saudia nchini Yemen
Vita vamizi vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vilianzishwa mwezi Machi mwaka 2015 kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi. Vita hivyo vingali vinaendelea kwa mwaka wa tatu sasa bila ya utawala wa Aal Saud na waitifaki wake kufikia malengo haramu waliyokusudia. Watu zaidi ya 13,000 , wengi wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa katika hujuma ya Saudia nchini Yemen.

UHURU KENYATTA AONGOZA KWA 96%, ODINGA ATAKA UCHAGUZI MPYA NDANI YA SIKU 90

Uhuru Kenyatta aongoza kwa 96%, Odinga ataka uchaguzi mpya ndani ya siku 90
Rais Uhuru Kenyatta anaongoza kwa asilimia 96 katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika Alkhamisi iliyopita nchini Kenya.
Matokeo ya awali ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta anaendelea kuongoza kwa kura zaidi ya milioni 7.
Wagombea wengine wanaomfuata kwa pamoja wamepata chini ya asilimia 5 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.
Wananchi wa Kenya Alkhamisi walielekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa marudio wa urais kufuatia kutenguliwa ule wa awali uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Jana Ijumaa, Raila Odinga, kinara wa muungano wa NASA ambao umebadilishwa jina na sasa litafahamika kama Vuguvugu la Mageuzi NRM alisema kujitokeza idadi ndogo ya watu katika uchaguzi huo ni ishara tosha kuwa kulikuwa na uchakachuaji katika uchaguzi wa Agosti 8, huku akisisitiza kuwa lazima uchaguzi mwingine ufanyike ndani ya siku 90.
Raila Odinga
Mahakama ya Juu ya Kenya ilitengua matokeo ya uchaguzi huo wa rais kwa hoja kwamba IEBC ilifanya baadhi ya makosa katika mchakato wa uchaguzi. Muungano wa upinzani (Nasa) umewahimiza wafuasi wake kutoshiriki uchaguzi huo baada ya kiongozi wa muungano huo Raila Odinga kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.  
Katika hatua nyingine, IEBC imetangaza kuakhirisha tena zoezi la upigaji kura lililotazamiwa hii leo, katika kaunti nne za Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya, ambazo ni ngome za NASA, ambazo siku ya Alhamisi wakazi wake hawakupiga kura kwa sababu za kiusalama.

RAIS ROUHANI: IRAN INA HAMU YA KUONGEZA KIWANGO CHA UHUSIANO NA USHIRIKIANO WAKE NA TANZANIA

Rais Rouhani alipoonana na balozi wa Tanzania, Bw. Mbarouk Nassor Mbarouk Rais Rouhani alipoonana na balozi wa Tanzania, Bw. Mbarouk Nassor Mbarouk
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tanzania ni lango muhimu la kuingilia eneo la mashariki mwa Afrika na kwa kuzingatia kuwa Iran ina nafasi na uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali na jambo hilo linaufanya wajibu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili kuwa na umuhimu wa kieneo.
Rais Rouhani amesema hayo leo Jumamosi hapa Tehran wakati alipopokea hati za utambulisho za Balozi  mpya wa Tanzania Bw. Mbarouk Nassor Mbarouk na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina hamu ya kuona kiwango cha uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania kinakuwa kikubwa.
Mheshimiwa Rais pia amesema, kuna nyuga nyingi za kustawisha uhusiano wa Iran na Tanzania kama vile sekta ya madini na nishati na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuipatia Tanzania uzeofu wake katika masuala mbalimbali.
Kwa upande wake, Balozi Mbarouk ameashiria namna Tanzania inavyolipa umuhimu mkubwa suala la kuimarisha uhusiano wake wa Iran katika sekta tofauti na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua nzuri katika nyuga nyingi na tofauti; za kisayansi, kiufundi na kiteknolojia hususan sekta na nishati na kwamba anaamini kuwa, Tanzania inaweza kufaidika na uzoefu wa Iran katika mambo tofauti.

Saturday, October 21, 2017

MAREKANI YAZIDI KUJIKITA KIJESHI AFRIKA; IDADI YA ASKARI WAKE BARANI HUMO YAONGEZEKA MARA TATU

Marekani yazidi kujikita kijeshi Afrika; idadi ya askari wake barani humo yaongezeka mara tatu
Gazeti la Kifaransa la Le Monde limeripoti kuwa Marekani imepanua wigo wa uingiliaji wake kijeshi katika nchi za Afrika kwa kuongeza idadi ya askari wake walioko kwenye nchi za bara hilo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, katika muendelezo wa sera za Washington za kudhamini maslahi yake, idadi ya askari wa Marekani wanaopelekwa katika nchi za Afrika kwa anuani ya "utoaji mafunzo, uratibu wa majeshi ya nchi za Kiafrika na kushiriki katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi" imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Ramani ya vituo vya vijeshi na vinginevyo vya Marekani barani Afrika
Le Monde limeongeza kuwa, katika harakati inayolenga kudhamini manufaa na maslahi yake barani Afrika, Marekani imekuwa ikivuruga uthabiti ndani ya nchi za bara hilo ili kuongeza idadi ya vikosi vya jeshi lake, kiasi kwamba baada ya Mashariki ya Kati, bara Afrika limekuwa eneo la pili lenye uingiliaji mkubwa zaidi wa kijeshi wa Marekani duniani.
Kwa mujibu wa viongozi wa Marekani, kati ya askari elfu nane wa kikosi maalumu cha nchi hiyo ambao tangu ulipoanza mwaka huu wa 2017 wametumwa katika pembe mbalimbali za dunia, zaidi ya askari 1,300 wako barani Afrika na wengine karibu 5,000 wako katika eneo la Mashariki ya Kati.../

SHAMBULIO LA MOGADISHU, SOMALIA YAFIKIA 358 WALIOUAWA

  • Idadi ya waliouawa katika shambulio la Mogadishu, Somalia yafikia 358
Idadi ya watu waliouawa katika shambulio la kigaidi la siku ya Jumamosi iliyopita katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu imeongezeka na kufikia 358.
Waziri wa Habari wa Somalia Abdurahman Othman ametangaza kuwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za karibuni kabisa kuhusu waathirika wa shambulio la kigaidi la mjini Mogadishu, watu wasiopungua 358 wameuawa, 228 wamejeruhiwa na wengine 56 hawajulikani waliko hadi sasa.
Abdurahman Othman ameongeza kuwa majeruhi 122 wa shambulio hilo la kigaidi wamesafirishwa kupelekwa Uturuki, Sudan na Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Shambulio hilo la tarehe 14 Oktoba lililofanywa kwa kutumia lori lililotegwa bomu lilitokea katika eneo la kibiashara la Hodan lenye msongamano mkubwa wa watu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Baadhi ya waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo
Majengo na magari yaliyokuweko umbali wa mita mia kadhaa yaliharibiwa vibaya na mripuko mkubwa uliosababishwa na bomu hilo na watu wengi waliteketea kwa moto wakiwa hai au miili yao kukatika vipande vipande.
Kabla ya shambulio la siku ya Jumamosi iliyopita, shambulio kubwa zaidi la kigaidi kutokea nchini Somalia lilikuwa la mwezi Oktoba mwaka 2011 ambapo watu 82 waliuawa na wengine 120 walijeruhiwa.
Ijapokuwa hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo lakini viongozi wa serikali ya Somalia hawana shaka kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Al Shabab ndilo lililofanya shambulio hilo...

Tuesday, September 12, 2017

MASHIRIKA YA KUTETEA HAKI ZA BINADAMU YAIKOSOA UN KWA KUTOCHUKUA HATUA DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU, MYANMAR

Jumuiya na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kutochukua msimamo imara mbele ya jinai zinazoendelea kufanywa na jeshi na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.
Mashirika hayo yanasema kinachofanyika nchini Myanmar ni maangamizi ya kizazi cha Waislamu wa Rohingya.
Mashirika hayo yameashiria jinai ya kuwalazimisha Waislamu zaidi ya laki tatu wa Myanmar kuyahama makazi yao katika kipindi cha kuanzia tarehe 25 mwezi uliopita na kusisitiza udharura wa kusitishwa uhalifu kama huo. Mashirika hayo pia yamezitaka nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinazotazamiwa kukutana leo mjini New York kwa ajili ya kuchunguza mgogoro wa Myanmar, zichukua hatua za maana katika uwanja huo. 
Waislamu wa Myanmar wakilazimishwa kuhama makazi na vijiji vyao
Siku chache zilizopita pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kusitisha ukatili unaofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.
Tangu Ijumaa ya tarehe 25 Agosti Waislamu wasiopungua elfu 6 na 334 wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuwa na wengine zaidi ya elfu 8 kujeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine.

Friday, September 1, 2017

MAHAKAMA YA JUU KENYA YAAMURU UCHAGUZI MPYA WA RAIS

Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamuru kurejewa kwa uchaguzi wa rais nchini humo, ikiyafuta yale ya awali yaliyokuwa yamempa ushindi Rais Uhuru Kenyatta. 
Kenias Oberstes Gericht (picture-alliance/AP Photo/S. Azim)
Mahakama hiyo imesema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu kwenye uchaguzi wa tarehe 8 Agosti kiasi cha kuvunja hata katiba ya taifa hilo la Afrika Mashariki. 
Uchaguzi mpya umeamuriwa kufanyika ndani ya siku 60 kutoka sasa. 
Mgombea wa upinzani, Raila Odinga, alikuwa amedai kuwa matokeo ya kura kwa njia ya elektroniki yalidukuliwa na kuchakachuliwa kumsaidia Uhuru Kenyatta wa chama tawala, Jubilee. 
Tume ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, ilikuwa imemtangaza Kenyatta mshindi wa asilimia 54 ya kura.
Wakeya kadhaa waliamua kuingia mitaani kupinga matoeo hayo na walikuwa wamedhamiria kuingia tena endapo mahakama ingelipitisha ushindi huu. 
Hii ni mara ya pili kwa Odinga kupinga matokeo mahakamani, lakini mwaka 2013 alishindwa.

TUME YA UCHAGUZI DRC KUTANGAZA RATIBA YA UCHAGUZI

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Corneille Nangaa amesema ratiba ya Uchaguzi mkuu itatangazwa hivi karibuni.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya tume hiyo kutangaza kuwa jumla ya wapiga kura milioni 40 wameandikishwa kwenye majimbo 24 na kwamba kuanzia tarehe nne itaanza kuandikisha wapiga kura kwenye majimbo mawili ya Kasai.
Serikali ya Kinshasa imesema zoezi la kuandikisha wapiga kura litaanza kukamilika kabla ya kutangazwa mambo mengine.
Mapema wiki hii Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) ilisema, zoezi la kuhakiki na kuandikisha wapiga kura wapya kwenye majimbo mawili ya Kasai ambako kumeshuhudiwa machafuko hivi karibuni, litaanza September 4 na kisha kuendelea kwenye majimbo mengine 24
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi CENI, Corneille Nangaa amewataka wananchi kuwasaidia maofisa wake kufanya kazi ya kuandaa uchaguzi kwa uhuru.
Rais Joseph Kabila
Katika hatua nyingine upinzani umekosoa takwimu za hivi karibuni zilitolewa na tume hiyo ukisema kwamba kiwango kikubwa hakiko sawa.
CENI ilisema jumla ya wapiga kura milioni 40 wameandikishwa kwenye majimbo mengine 24 huku taifa hilo likiwa na jumla ya raia milioni 70 wengi wao wakiwa bado hawajaandikishwa.
Mgogoro wa ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliibuka baada ya kuahirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais na kadhalika sisitizo la Rais Joseph Kabila la kutaka kuendelea kubakia madarakani. Licha ya kutiwa saini makubaliano baina ya wapinzani na serikali juu ya kufanyika uchaguzi wa rais tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu, lakini inaonekana kuwa, uchaguzi huo hautaweza kufanyika katika tarehe iliyopangwa.

WAISLAMU 400 WAFARIKI DUNIA MYANMAR KATIKA KIPINDI CHA WIKI MOJA

  • Waislamu 400 wafariki dunia Myanmar katika kipindi cha wiki moja
Waislamu takribani 400 wamefariki dunia nchini Myanmar katika kipindi cha wiki moja tokea jeshi la nchi hiyo lianzishe kampeni mpya ya kuwakandamiza Waisalmu wa jamii ya Rohingya.
Takwimu ramsi zinaonyesha kuwa watu 400 wamepoteza maisha katika jimbo la Rakhine tokea Ijumaa iliyopita. Kati ya walipooteza maisha ni wale waliouliwa na jeshi la nchi hiyo katika oparesheni  dhidi ya Waislamu huku wengine, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wakipoteza maisha wakati wakivuka mto kukimbia mapigano katika jimbo la Rakhine.
Jeshi la Myanmar Ijumaa iliyopita lilianzisha oparesheni kali dhidi ya Waislamu kwa madai kuwa watu wanaodaiwa kuwa ni Waislamu walihujumu vituo vya polisi jimboni Rakhine.
Mabuddha wenye misimamo mikali
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi duniani. 
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Bangladesh, Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

Sunday, July 30, 2017

MAKUMI WAUAWA NA KUJERUHIWA KATIKA MRIPUKO WA MOMU MOGADISHU, SOMALIA

Watu sita wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari kuripuka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Meja Mohamed Hussein, afisa mwandamizi wa polisi nchini humo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa bomu hilo limeripuka katika barabara yenye shughuli nyingi ya Makatul Mukaramah.
Amesema aghalabu ya wahanga wa hujuma hiyo inayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab, ni wapita njia na watu waliokuwa ndani ya maduka yaliyoko kandokando ya barabara hiyo.
Afisa huyo wa polisi ya Somalia ameongeza kuwa, yumkini idadi ya vifo ikaongezeka, kutokana na majeraha mabaya waliyopata baadhi ya wahanga wa shambulizi hilo. 
Askari wa AMISOM
Wakati huohuo, makabiliano makali kati ya askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab yameripotiwa katika wilaya ya Bulamareer, eneo la Shabelle ya Chini, yapata kilomita 140 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na AMISOM au jeshi la Somalia kuhusu idadi ya wahanga wa mapigano hayo, ingawaje genge la al-Shabaab linadai kuwa limeua makumi ya askari wa Umoja wa Afrika.
AbdiAziz Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za al-Shabaab amedai kuwa, kundi hilo la kigaidi limeua wanajeshi 39 wa AMISOM akiwemo kamanda wao.