Vikosi vya Kujitolea vya Wananchi wa Iraq,
maarufu kwa jina la al Hashdu al Sha'abi vimetangaza habari ya
kuangamizwa Liwali wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika wilaya ya
Tal Afar, magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineve).
Vikosi hivyo vimetangaza habari
hiyo na kuongeza kuwa, ndege za jeshi la Iraq baada ya kubadilishana
taarifa za kiintelijensia na vikosi vya al Hashdu al Sha'abi vimefanya
shambulizi la anga kwenye eneo alipokuwa amejificha 'Mustafa Yusuf'
Liwali wa kundi la kigaidi la Daesh katika wilaya ya Tal Afar na
kumuangamiza.
Habari nyingine kutoka nchini Iraq
zinasema kuwa, brigedi ya 11 ya vikosi vya al Hashdu al Sha'abi jana
Jumatano viliangamiza magaidi sita na kuwajeruhi wengine saba kusini
magharibi mwa wilaya ya Tal Afar. Mtandao wa habari wa Iraq Press
umeripoti habari hiyo na kusema kuwa Brigedi ya 11 ya al Hashdu al
Sha'abi imeangamiza magaidi hao na kuwajeruhiwa wengine saba katika
operesheni ya kusafisha kitongoji cha "Ain Talawi" cha kusini magharibi
mwa wilaya ya Tel Afar, magharibi mwa mkoa wa Nainawa.
Vikosi vya al Hashdu al Sha'abi jana
Jumatano vilianza hatua ya sita ya operesheni zake za kijeshi katika
upande wa magharibi wa mkoa wa Nainawa, wa kaskazini mwa Iraq na
kufanikiwa kukomboa vijiji kadhaa kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh.
Itakumbukwa kuwa, mwezi uliopita, eneo
la mashariki mwa mji wa Mosul lilikombolewa kikamilifu kutoka mikononi
mwa magaidi wa Daesh na hivi sasa raia waliolazimika kukimbia maeneo yao
kutokana na jinai za magaidi hao wakufurishaji wanaendeleo kurejea
kwenye maeneo yao, huko mashariki mwa Mosul.
No comments:
Post a Comment