Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema, matatizo yote ya eneo
la Mashariki ya Kati ni uingiliaji wa baadhi ya madola makubwa ikiwemo
Marekani katika masuala ya ndani ya eneo hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesema hayo leo jioni wakati alipoonana na Stefan Löfven,
Waziri Mkuu wa Sweden hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, Marekani na
madola mengine mengi ya Ulaya yamehusika moja kwa moja katika matukio
machungu ya nchini syria na Iraq na kwamba wananchi wa eneo hili
wamekasirishwa mno na uingiliaji wa madola hayo ya kibeberu.
Amesema, utatuzi wa matatizo ya eneo
hili inabidi ufanywe na wananchi wenyewe wa Mashariki ya Kati na huku
akiashiria namna hali inavyorejea kuwa ya kawaida nchini Iraq amesema,
mgogoro wa Syria nao unaweza kutatuliwa kwa njia hiyo hiyo na hilo
litawezekana iwapo tu wanaowaunga mkono magaidi wataacha kufanya hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesema, kitendo cha baadhi ya mabalozi wa nchi za Magharibi
cha kushirikiana na wapinzani wa serikali ya Syria na kuwapa silaha
waziwazi mwanzoni mwa mgogoro wa nchi hiyo ni mfano wa wazi wa
uingiliaji wa madola ya kibeberu katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Amesema, kuna wajibu wa kujua kwanza chanzo cha mgogoro huo ndipo
zichukuliwe hatua za kuutatua.
Ayatullah Khamenei amegusia pia safari
za mara kwa mara za viongozi na maafisa wa serikali za Ulaya hapa mjini
Tehran katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita lakini pamoja na
hayo, sehemu kubwa ya maafikiano yanayofikiwa hayajatekelezwa kivitendo
na kumwambia Waziri Mkuu wa Sweden kwamba: Kutokana na welewa nilio nao
juu yako, ni kwamba wewe ni mtu wa kuchukua hatua na kufanya mambo
kivitendo, hivyo tunachokitarajia ni kuona utekelezaji wa kivitendo wa
maafikiano yanayofikiwa na isiwe ni makubaliano yanayoishia kwenye
makaratasi tu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ameashiria pia kura ya ndio iliyopigwa na Iran kwa ajili ya
kuchaguliwa Sweden kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
na kuongeza kuwa, Baraza la Usalama ni chombo muhimu sana ambacho kwa
bahati mbaya kimekuwa mateka wa baadhi ya madola makubwa ya kibeberu.
Hata hivyo upo uwezekano wa kukizuia chombo hicho kuchukua maamuzi ya
kugongana na ya kindumilakuwili.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameitaja
hamasa ya kupigiwa mfano iliyooneshwa na wananchi wa Iran katika
maadhimisho ya Bahman 22 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu jana Ijumaa
na kusisitiza kuwa: Maadhimisho ya mapinduzi mbalimbali duniani
hufanyika kimaonyesho na kwa gwaride la jeshi kwenye eneo moja maalumu
lililohudhuriwa na baadhi ya watu tu, lakini maadhimisho ya ushindi wa
Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ambayo ni ya wananchi wenyewe; kwa
hakika ni sherehe za kweli za kitaifa zinazofanyika kona zote za Iran
ambazo zinawashirikisha watu wa matabaka yote.
No comments:
Post a Comment