Sambamba na kuanza hatua ya pili ya
operesheni za kuyasafisha maeneo ya magharibi mwa Mosul, kaskazini mwa
Iraq, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kudhibiti uwanja wa ndege wa mji
huo ambao ulikuwa ngome kuu ya magaidi wakufurishaji wa Daesh (ISIS.)
Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Iraq imesema kuwa, jeshi la
nchi hiyo limetumia mashambulizi mapana ya kila upande katika kuukomboa
uwanja huo wa ndege wa al-Ghazlani kusini magharibi mwa mji wa Mosul.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa polisi wa federali na kikosi cha radiamali
ya haraka ya jeshi la Iraq wamefanikiwa kusonga mbele na kuwaswaga
wanachama wa genge hilo la kigaidi kutoka uwanjani hapo.
Inaelezwa kuwa, awali magaidi hao walitumia zana mbalimbali za
kijeshi ikiwemo ndege zisizokuwa na rubani kwa lengo la kulizuia kusonga
mbele jeshi la Iraq, juhudi ambazo hata hivyo zimeishia kufeli. Habari
zaidi zinaarifu kwamba mamia ya wakazi wa maeneo ya magharibi mwa Mosul
wameziacha nyumba zao na kwenda maeneo mengine kwa ajili ya usalama.
Televisheni rasmi ya Iraq imeonyesha askari wa serikali wakiwasili
katika uwanja wa ndege wa al-Ghazlani. Kabla ya hapo Jenerali Shakir
Judat, kamanda wa jeshi la polisi nchini Iraq alinukuliwa akisema kuwa
jeshi la Iraq lilizishambulia ngome muhimu za genge la Daesh katika
uwanja huo wa ndege na kulitia hasara kubwa kundi hilo la Daesh
linaloungwa mkono na Marekani, Israel na Saudi Arabia.
Operesheni ya kulikomboa eneo la magharibi mwa Mosul kutoka katika
makucha ya wanachama wa genge la kigaidi na Kiwahabi la Daesh (ISIS)
zilianza Jumapili iliyopita kwa amri ya Waziri Mkuu wa Iraq, Haider
al-Abadi. Hii ni katika hali ambayo mwezi uliopita pia jeshi la Iraq kwa
kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Shaab lilifanikiwa
kuyakomboa maeneo ya mashariki mwa mji huo wa Mosul na kuwafanya maelfu
ya wakazi wa meneo hayo kurejea makwao.
No comments:
Post a Comment