Shirika la kimkataifa la kutetea haki za binaadamu la
Amnesty International limesema serikali ya Syria imewaua zaidi ya watu
13,000 tangu kuanza kwa vuguvugu la mapinduzi ya umma mwaka wa 2011
Katika ripoti ya utafiti uliofanywa kati ya 2011 na 2015, Amnesty
International imesema kati ya watu 20-50 walinyongwa kila wiki katika
gereza la Saydnaya, mauaji yaliyoidhinishwa na maafisa wa ngazi za juu
serikalini, wakiwemo wasaidizi wa Rais Bashar al Assad, na kufanywa na
jeshi la polisi.
Ripoti hiyo iliyataja mauaji hayo kuwa ni
"kampeni iliyopangwa ya mauaji ya kinyume cha sheria”. Naibu mkurugenzi
wa utafiti wa ofisi ya kikanda ya Amnesty mjini Beirut Lynn Maalouf
amesema shirika hilo limeorodhesha karibu mbinu 35 tofauti za mateso
nchini Syria tangu mwishoni mwa miaka ya 80, vitendo ambavyo
vimeongezeka tangu mwaka wa 2011. "Amnesty international inafichua
kampeni ya mpangilio ya mauaji ya kinyume cha sheria kwa njia kuwanyonga
watu wengi kila wiki, yanayofanywa Jumatatu na Jumatano. Kati ya watu
20 na 50, hutolewa kwenye vyumba vyao, na kupelekwa katika jumba jingine
mjini Sednaya na kunyongwa".
Mashirika
mengine ya haki za binaadamu yamepata ushahidi wa mateso makubwa
yaliyosababisha vifo katika magereza ya Syria: katika ripoti yake mwaka
jana, Amnesty iligundua kuwa zaidi ya watu 17,000 waliuawa kwa kuteswa
wakatiwa kizuizini kote Syria tangu mwaka wa 2011, ikiwa ni kiwango cha
wastani cha zaidi ya watu 300 kwa mwezi. Takwimu hizo zinaweza
kulinganishwa na vifo vilivyotokea katika viwanja vya mapambano vya
Aleppo, mojawapo ya maeneo makali ya vita nchini Syria, ambako watu
21,000 waliuawa kote mkoani humo tangu 2011. Maalouf anasema hakuna
sababu ya kuamini kuwa dhuluma hizo zimekomeshwa tangu mwaka wa 2015,
maana huenda maelfu ya watu wameuawa.
Ameongeza kuwa mauaji haya
hufanyika baada ya kuendeshwa kesi ya uongo inayodumu dakika moja au
mbili, lakini yanaidhinishwa na maafisa wakuu akiwemo Mufti mkuu, na
waziri wa ulinzi. Maalouf ametoa wito wa kuchunguzwa madai hayo "Tunatoa
mwito kwa Umoja wa Mataifa kuanzisha uchunguzi wa huru na wazi kuhusu
kinachotokea Sednaya na kwa hili kufanyika katika njia ya mafanikio,
tunaitaka serikali ya Syria kuwaruhusu waangalizi wake, waangalizi wa
Umoja wa Mataifa ambao wako huru, kuingia Sednaya, lakini pia katika
magereza yote na vituo vya kuwazuilia watu kote Syria".
Huwa
nadra kwa maafisa wa serikali ya Syria kuzungumzia madai haya ya mateso
na mauaji ya watu wengi. Katika siku za nyuma, walipinga ripoti za
mauaji ya kikatili yaliyoorodheshwa na mashirika ya kimataifa ya haki za
binaadamu, wakiritaja kuwa ni propaganda. Matokeo ya ripoti iliyotolewa
leo yalitokana na mahojiano yaliyofanyiwa wafungwa wa zamani 31 na
maafisa wengine 50 na watalaamu, wakiwemo walinzi wa zamani wa magereza
na majaji.
No comments:
Post a Comment