Mahakama ya Rufaa nchini Kenya leo imetoa
amri ya kuachiliwa huru viongozi wa muungano wa madaktari na kusema
kwamba, sasa wanaweza kufanya mazungumzo na serikali kuhusiana na mgomo
katika sekta ya afya ambao umekwamisha pakubwa huduma katika sekta hiyo.
Katika taarifa yake, Mahakama ya
Rufaa nchini Kenya imeamua viongozi wa chama cha wahudumu wa afya
waliokuwa wamefungwa jela mwezi mmoja waachiliwe huru mara moja.
Viongozi saba wa madaktari nchini Kenya
walifungwa Jumatatu baada ya kupatikana na hatia ya kutofuata uamuzi wa
mahakama wa kumaliza mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa miezi miwili
na nusu sasa. Viongozi hao wametakiwa kuhakikisha suluhu ya mgomo huo
inapatikana katika kipindi cha siku saba zijazo.
Mazungumzo ya kutafuta suluhu yataongozwa na Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) na Tume ya Taifa ya Haki za Kibinadamu (KNHCR).
Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali ya
Kenya kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara na
kuboresha mazingira ya utendaji kazi hospitalini
Wanataka pia serikali iwekeze zaidi
katika dawa, vifaa na mitambo hospitalini pamoja na kutoa pesa zaidi za
kufadhili utafiti wa kimatibabu. Wamekataa mshahara walioongezewa na
serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule
walioafikiana mwaka 2013. Karibu madaktari na wauguzi 5,000 kutoka
hospitali 2,000 za umma nchini Kenya, walianza mgomo wiki ya kwanza ya
mwezi Desemba na wagonjwa wamekuwa wakikosa matibabu. Mgomo huo wa
madaktari umewakasirisha mno Wakenya na kuwa changamoto kubwa kwa
serikali ya Rais Uhuru Kenyatta anayetarajiwa kutetea kiti chake katika
uchaguzi ujao wa Agosti mwaka huu.
No comments:
Post a Comment