Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence amewakikishia
viongozi wa Umoja wa Ulaya na NATO kwamba rais wa Marekani Donald Trump
amejitolea kwa dhati kuyaendeleza mahusiano na mataifa ya Ulaya leo
(20.02.2017) mjini Brussels.
Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence (kulia) na Jean-Claude Juncker
Pence amekutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels,
Ubelgiji, kituo chake cha mwisho cha ziara yake barani Ulaya, inayolenga
kuwatuliza viongozi wa nchi washirika wa Ulaya kwamba rais Trump
atawatelekeza. Akizungumza baada ya kukutana na rais wa Umoja wa Ulaya
Donald Tusk, Pence amesema Marekani imejitolea kwa dhati kuundeleza
ushirikiano na uhusiano na Umoja wa Ulaya.
Kiongozi huyo aidha
amesema licha ya tofauti zilizopo, mabara ya Ulaya na Amerika yana
utamaduni na maadili yanayofanana, na juu ya yote yana lengo moja la
kuimarisha amani na maendeleo kupitia uhuru, demokrasia na utawala wa
sheria, na Marekani itaendelea kujitolea daima kuyatimiza malengo hayo.
"Tunataka
kuchukua hatua na tunautolea mwito Umoja wa Ulaya uungane na Marekani
kuendelea kuimarisha juhudi za kukikabili kitisho cha ugaidi barani
Ulaya. Ushirikiano zaidi utahitajika pamoja na kubadilishana taarifa za
kijasusi kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kati ya Umoja wa
Ulaya na NATO. Na Marekani itautanua ushirikiano huo kwa lengo la
kuwalinda raia wetu."
Pence ameahidi Marekani itaendelea
kushirikiana na Ulaya kuimarisha uchumi wa kanda hizo mbili kubwa
duniani, kupambana na ugaidi na kuyalinda mataifa ya Ulaya Mashariki
ambayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi.
Mengi yamebadilika Marekani na Ulaya
Tusk,
ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Poland, kwa upande wake amesema
mengi yametokea Marekani na Ulaya katika kipindi cha mwezi mmoja na
ukweli uliopo ni kuwa mambo yamebadilika na hayako jinsi yalivyokuwa
zamani. Amesema usalama wa Ulaya unaitegemea jumuiya ya kujihami ya NATO
na ushirikiano wa karibu na Marekani kadri iwezekanavyo na kwamba Ulaya
inategemea msaada wa Marekani.
Mike Pence, kushoto, akiwa na Donald Tusk
"Sharti
tufanye kazi pamoja kuimarisha mifumo ya ushirikiano huu uwe wa kisasa,
lakini pia tunatakiwa tukubaliane kuhusu jambo moja. Wazo kwamba
jumuiya ya NATO haijapitwa na wakati, kama yalivyo maadili yaliyojikiti
katika misingi yake. Tujadili kila kitu, tukianzia utoaji michango ya
kifedha lakini kwa lengo la kuiimarisha NATO na wala sio kuidhoofisha,"
alisema Tusk.
Pence amekutana pia na rais wa kamisheni ya Umoja
wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, ambaye amesititiza kwamba Marekani
inaihitaji Ulaya iliyoungana. Juncker, ambaye ni waziri mkuu wa zamani
wa Luxembourg, pia amehimiza mshikamano katika Umoja wa Ulaya akisema
huu sio wakati wa Ulaya kugawika katika mataifa na mikoa kama ilivyokuwa
zamani.
Maandamano yafanyika
Waandamaji
kadhaa walikusanyika nje ya makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels
wakati wa zaira ya Pence, kuukosoa msimamo wa serikali ya rais Trump
kuhusu wanawake, mashoga na mabadiliko ya tabai nchi. Usalama
uliimarishwa maradufu katika eneo la majengo ya Umoja wa Ulaya wakati wa
ziara ya kiongozi huyo.
Wanawake walioandamana wakiwa nusu uchi Brussels
"Tuko
hapa kuandamana dhidi ya ziara ya Pence kwa sababu tumechukizwa na
uamuzi wa utawala wa Marekani kuhujumu haki za wanawake ulimwenguni
kote," alisema Irene Donadio, anayefanya kazi na shirika la kimataifa la
uzazi wa mpango, wakati alipozungumza na shirika la habari la Ufaransa,
AFP.
No comments:
Post a Comment