Watu wasiopungua 11 wameuawa Jumatatu katika
eneo la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya
kuzuka mapigano baina ya jeshi la serikali na wanamgambo watiifu kwa
chifu wa jadi aliyeuawa mwaka jana.
Kwa
mujibu wa Jean Rene Tshimanga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiraia ya
Kasai, mapigano hayo ya yamejiri karibu na mji wa Tshimbulu, mji ambao
jeshi liliua wanagambo 60 siku ya Ijumaa.
Tshimanga
amesema bado hajaweza kubaini ni wanagamabo au wanajeshi wangapi
waliouawa katika mapigano hayo. Hadi sasa maafisa wa utawala na wale wa
jeshi hawajatoa taarifa rasmi kuhusu mapigano hayo.
Chifu Kamuina Nsapu aliuawa mwaka jana
na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tangu wakati
huo, miji kadhaa na vijiji vya mji wa Kasai ya Kati na Kasai ya
Mashariki imekuwa ikishuhudiwa vurugu, machafuko na mapigano kati ya
vikosi vya kulinda usalama na wanamgambo hao wanaomuunga mkono kiongozi
wao wa zamani Kamuina Nsapu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, maeneo
ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakishuhudia
machafuko kwa zaidi ya miongo miwili sasa na yanahesabiwa kuwa ngome ya
makundi ya waasi yakiwemo makundi ya waasi kutoka nje ya nchi hiyo kama
LRA, FDLR na ADF-Nalu.
Mapigano yanaripotiwa kukithiri kote
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na hatua ya Rais Joseph Kabila
ya kukataa kuondoka madarakani baada ya muhula wake wa urais kumalizika
mwezi Disemba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment