Ujerumani leo yafanya uchaguzi wa Rais
Baraza maalum la wajumbe na wawakilishi kutoka majimbo
yote ya Ujerumani litakutana leo kumchagua rais mpya wa
Ujerumani. Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier
ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuchaguliwa.
Akiwa mwanasiasa anaependwa zaidi na umma hapa nchini Ujerumani
Frank-Walter Steinmier atachukua wadhifa wa urais kutoka kwa Joachim
Gauck mwenye umri wa miaka 76, mhubiri wa zamani na mwanaharakati wa
kutetea demokrasia ambaye mwaka jana alisema hatawania muhula mwingine
madarakani wa miaka mitano kwasababu ya umri wake.
Rais
anachaguliwa na kongamano maalum la wajumbe 1260 bungeni mjini Berlin
ambalo linajumuisha wabunge 630 na idadi kama hiyo ya wawakilishi wa
majimbo yote 16 ya Ujerumani. Steinmeier anaungwa mkono na serikali
baada ya Merkel kushindwa kumpata mgombea wa kihafidhina anayestahili
kuwa rais.
Umaarufu wa chama cha SPD waongezeka
Licha
ya kuwa kwa muda mrefu amekuwa mwanasiasa anayependwa Ujerumani,
alishindwa kumuondoa madarakani Merkel katika uchaguzi wa Ukansela wa
mwaka 2009. Uchaguzi wa leo unakuja wakati Ujerumani ikijiandaa kuelekea
uchaguzi mkuu mwezi Septemba mwaka huu ambapo Merkel anagombea muhula
wa nne madarakani.
Wasocial Democrats hivi sasa wana uungwaji
mkono mubwa kulingana na kura za maoni tangu kumteua aliyekuwa Rais wa
bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz kuwa mgombea wao wa Ukansela.
Kansela Angela Merkel na mgombea Ukansela Martin Schulz
Kuimarika
kwa chama cha SPD kunaongeza shinikizo kwa Merkel na chama chake
kujiandaa vyema na kufanya kampeini kali kuelekea uchaguzi. Lakini
kuchaguliwa kwa Rais ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kuteua
serikali mpya na majaji kumeonyesha kuwa kibarua kigumu kwa Merkel.
Tofauti
na Gauck ambaye hakuwa anaegemea chama chochote cha kisiasa, Steinmeier
amekuwa katika siasa za Ujerumani kwa muda mrefu. Kama mnadhimu mkuu wa
Kansela Gehard Schroeder alikuwa miongoni mwa waasisi wakuu wa mageuzi
ya kiuchumi mwaka 2003, mageuzi yanayotajwa kuchangia Ujerumani kuwa
nchi imara kiuchumi.
Steinmeier ndiye mwanasiasa anayependwa zaidi Ujerumani
Chini
ya utawala wa Merkel, amehudumu mara mbili kama waziri wa mambo ya nje
kuanzia mwaka 2005 hadi 2009 na tena kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka huu.
Anaheshimika pakubwa kwa kujaribu kuutatua mzozo wa Ukraine. Mwanasiasa
huyo ambaye ni mwanadiplomasia mtajika, alimshutumu vikali Donald Trump
wakati wa kampeini za uchaguzi wa rais wa Marekani.
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck na mgombea urais Frank Walter Steinmeier
Alipoulizwa
mwezi Agosti kuhusu kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo Ujerumani na
kwingineko, Steinmeier aliwashutumu wale aliowataja wanaofanya siasa za
kuingiza uoga, akikitaja chama cha mrengo wa kulia cha siasa kali
zinazowapinga wahamiaji Ujerumani Alternative für Deutschland AfD,
waliopelekea Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya na wanaoeneza
chuki kama Donald Trump.
Alipoteuliwa kugombea urais mwezi
Novemba, Steinmeier alitoa wito wa kuwepo imani wakati ulimwngu
unapokumbwa na mizozo akiongeza Rais wa Ujerumani sharti awe mtu ambaye
harahisishi mambo bali anayewatia moyo watu. Merkel amemsifu Steinmeier
na kumtaja kuwa ni kiongozi wa maana na mwafaka wakati ambapo kuna
msukosuko na hali ya sintofahamu ulimwenguni.
Steinmeier
anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wagombea wengine watatu akiwemo
Alexander Hold wa chama kidogo cha siasa za wastani za mrengo wa kulia-
Freie Waehler, mtafiti kuhusu umasikini Christoph Butterwegge wa chama
cha mrengo wa kushoto cha Die Linke na Albrecht Glaser wa chama cha
siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Deutschland AfD
No comments:
Post a Comment