Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema leo
kuwa nchi hiyo itazifanyia marekebisho sheria zake ili kuruhusu
utaifishaji wa ardhi bila ya kuwalipa fidia wamiliki wa ardhi hizo,
katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo inajaribu kuharakisha zoezi la
kuwagawia tena ardhi raia weusi walio wengi wa nchi hiyo.
Itafahamika
kuwa sehemu kubwa ya ardhi ya Afrika Kusini inamilikiwa na wazungu kwa
zaidi ya miongo miwili baada ya kumalizika utawala wa ubaguzi wa rangi
nchini humo (Apartheid). Rais Zuma amesema katika hotuba yake akiashiria
sera za kilimo za serikali yake kuwa, wanahitaji kuchukua hatua
madhubuti zitakazobadili uchumi wa nchi hiyo kwa haraka, likiwemo suala
la umiliki wa ardhi.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa msimamo huo mkali ulioonyeshwa na
chama tawala ANC unajiri sambamba na miito iliyotolewa na chama cha
upinzani cha Economic Freedom Fighters ambacho kimetaka kutaifishwa
ardhi zinazomilikiwa na wazungu huko Afrika Kusini. Wachambuzi hao pia
wanasema kuwa serikali ya Afrika Kusini imechukua hatua hiyo ili kuungwa
mkono kisiasa chama tawala katika ngome za vijijini kabla ya kufanyika
uchaguzi wa ndani ya chama mwezi Disemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment