Tuesday, May 30, 2017

13 ASKARI WA SUDANI KUSINI WATUHUMIWA UBAKAJI, MAUAJI WAPANDISHWA KIZIMBANI

Wanajeshi 13 wa Sudan Kusini wamefunguliwa mashtaka ya ubakaji na mauaji katika kesi inayoonekana kutumiwa na serikali ya Juba kuonyesha kuwa ina uwezo wa kusikiliza kesi za jinai za kivita.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wanajeshi hao wanatuhumiwa kuhusika na ubakaji wa wafanyakazi wa kufikisha misaada ya kibinadamu nchini humo raia wa kigeni sambamba na kumuua askari mwenzao.
Abukuk Mohammed Ramadhan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kijeshi nchini humo amesema wanajeshi hao pia wanakabiliwa na mashtaka ya uporaji na uharibifu wa mali na kusisitiza kuwa jambo la muhimu ni mahakama hiyo isikilize kesi hizo kwa njia inayofaa.
Mike Woodward, Mkurugenzi wa Hoteli ya Terrain mjini Juba ameiambia mahakama hiyo kuwa, wanajeshi kati ya 50 hadi 100 wa Sudan Kusini walifika hotelini hapo mnamo Julai 11 na kuanza kupora, kabla ya kuwabaka wanawake watano wafanyakazi wa asasi ya kufikisha misaada ya kibinadamu waliokuwepo hotelini hapo na kisha kumuua kwa kumfyatulia risasi mwandishi wa hahari kwa jina John Gatluak.

Jenerali Malong aliyepigwa kalamu nyekundu hivi karibuni


Mapema mwezi huu, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alitangaza kumfuta kazi Jenerali Paul Malong Awan, kamanda mkuu wa jeshi la nchi hiyo, kufuatia majenerali wengi wa ngazi ya juu jeshini kujiuzulu kutokana na kuwepo ubaguzi na jinai nyingi za kivita zinazofanywa na jeshi la Sudan Kusini.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

No comments:

Post a Comment