Rais Hassan Rouhani amesema, baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA waliowengi katika jamii ya kimataifa wameipa haki Iran na kuyatetea makubaliano hayo na kuongeza kwamba hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni nzuri kwa ajili ya kuendeleza makubaliano hayo ya nyuklia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyaeleza hayo mbele ya hadhara ya maulamaa na wanazuoni wa mjini Tehran na kubainisha kuwa: Leo akthari ya nchi zinaitakidi kuwa njia iliyofuata Iran ilikuwa sahihi na Marekani ndio iliyofanya makosa, na hayo ni mafanikio makubwa.
Rais Rouhani amefafanua kuwa Marekani inatoa mashinikizo kwa nchi za Ulaya kwamba zichague kati ya Marekani na Iran lakini nchi hizo zinasema 'sisi tunachagua makubaliano ya JCPOA'.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa msingi inaofungamana nao Iran ni kwamba kama itaweza kupata haki zake kwa kubaki kwenye makubaliano ya JCPOA itaendelea kufungamana na makubaliano hayo ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Mei 8 kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano hayo ya nyuklia ya Iran ambayo rasmi yanajulikana kama JCPOA. Trump aidha alisema ataiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya nyuklia katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa mno na uamuzi huo wa upande mmoja uliochukuliwa na rais wa Marekani.
Hii ni katika hali ambayo nchi zilizosalia katika JCPOA, yaani Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Ujerumani na Umoja wa Ulaya, zimesisitiza kuwa zitandelea kuunga mkono mapatano hayo.
Wakati huohuo katika siku za karibuni Iran na nchi za Ulaya zimefanya mazungumzo kadhaa kwa lengo la kuyaendeleza makubaliano ya JCPOA baada ya Washington kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.
Inafaa kukumbusha pia kuwa mnamo siku ya Jumatano iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alibainisha masharti ya Iran kuendelea kubakia katika JCPOA na kusisitiza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwasilisha azimio dhidi ya Marekani katika Baraza la Usalama, ziahidi pia kuwa kadhia za makombora na ushawishi wa Iran katika eneo hazitajadiliwa na pia zikabiliane na vikwazo vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran." Aidha Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kununua mafuta ya Iran kwa kiwango ambacho Iran inahitaji na pia benki za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kutekeleza malipo ya kifedha kwa ajili ya biashara na serikali pamoja na sekta binafsi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../
No comments:
Post a Comment