Mahakama ya rufaa yakataa kuruhusu utekelezwaji wa amri inayopinga kuingia Marekani
Mahakama ya rufaa nchini Marekani imekataa ombi la wizara ya sheria
kutaka amri ya kuzuia watu kutoka mataifa 7 hasa ya kiislamu kuingia
Marekani itekelezwe, tofauti na uamuzi wa awali wa mahakama ya Seattle
kusitisha kwa muda utekelezwaji wa amri hiyo. Mahakama ya rufaa imetaka
majimbo ya Washington na Minnesota ambayo awali yaliwasilisha pingamizi
dhidi ya amri hiyo kuwasilisha pingamizi zao kwa wizara ya sheria kuhusu
amri hiyo kabla ya saa sita adhuhuri majira ya Marekani. Rais Trump
anatarajiwa kuzungumzia rufaa hiyo aliyotaka kushughulikiwa kwa dharura
siku ya Jumatatu. Hapo awali, Trump alimshambulia jaji James Robart
aliyezuia amri hiyo. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump aliandika
jaji huyo anatatiza amri inayonuia kuzuia mashambulizi ya kigaidi nchini
Marekani. Mnamo siku ya Ijumaa, wiki iliyopita jaji huyo wa mahakama ya
wilaya ya Seattle alisitisha utekelezwaji wa amri hiyo ya Trump kwa
misingi ya kusubiri tathmini pana ya kisheria.
No comments:
Post a Comment