Monday, February 13, 2017

TAHADHARI KUHUSU NJAMA ZA MAREKANI NA ISRAEL ZA KUIBUA MIFARAKANO BAINA YA WAISLAMU

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu amesema: "Maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wanatumia uwezo wao wote kuibua mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu."
Ayatullah Muhsin Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukuribisha Madhehebu ya Kiislamu yenye makao yake hapa mjini Tehran ameyasema hayo katika mkutano aliofanya na maulamaa wa Kishia na Kisunni huko Hyderabad  nchini India.
Ameongeza kuwa, kama tunavyosoma katika Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume SAW, ni wajibu wa jamii ya Kiislamu kufanya jitihada zaidi za kuleta umoja miongoni mwa Waislamu wote na kuzuia adui na kujipenyeza kiutamaduni katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Araki ameongeza kuwa, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA na hivi sasa chini ya uongozi wenye busara wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kumekuwa na mabadiliko makubwa na muhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu na  Uislamu halisi unazidi kuenea.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu amesema: "Jamii wa Kiislamu nchini India na Maulamaa wa Kisuni na Kishia wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu."
Ayatullah Araki aidha Jumapili usiku alishiriki katika kongamano la "Umoja wa Umma katika Sira ya Bibi Fatima Zahra SA" mjini Heydarabad ambapo pia alisisitiza kuhusu umoja wa Kiislamu.

No comments:

Post a Comment