Spika wa bunge la Uingereza amesema rais wa Marekani
Donald Trump hafai kualikwa kulihutubia bunge hilo wakati atakapofanya
ziara rasmi nchini humo.
Spika wa bunge la Uingereza John Bercow
Matamshi hayo ya Spika John Bercow yanaondoa uwezekano kwa Trump
kupewa heshima hiyo wakati wa ziara yake baadae mwaka huu. Bercow
aliwambia wabunge kwamba angepinga mwaliko huo hata kabla ya marufuku
ya Trump inayowazuwia raia kutoka mataifa saba yenye Waislamu wengi
kuingia nchini Marekani.
"Kabla ya kuwekwa marufuku ya uhamiaji,
binafsi ningepinga vikali kuruhusiwa rais Trump kutoa hotuba katika
ukumbi wa Westminster. Baada ya kuwekwa kwa marufuku ya uhamiaji na rais
Trump, ninapinga hata vikali zaidi hotuba ya rais Trump katika ukumbi
wa Westminster," alisema Bercow bungeni siku ya Jumatatu.
Si matamshi ya kawaida
Matamshi
ya Bercow hayakuwa ya kawaida kwa sababu maspika wa bunge la Uingereza
wanatarajiwa kutoegemea upande wowote wa kisiasa. Ni mmoja wa maafisa wa
bunge ambao wangekubali kumualika mgeni wa nje kuwahutubia wabunge.
Rais Donal Trump anakosolewa kutoka kila kona ya dunia kutokana na mfumo wake wa utawala.
Viongozi
wa dunia waliowahi kupewa heshima ya kutoa hotuba kwa mabaraza yote ya
bunge ni pamoja na Nelson Mandela, na mtangulizi wa Trump Barack Obama.
Bercow
alishangiliwa na wabunge pale aliposema kwamba, inagwa Uingereza
inathamini uhusiano wake na Marekani, "upinzani wetu dhidi ya ubaguzi wa
rangi na kijinsia, na uungwaji wetu wa usawa mbele ya sheria na
mahakama huru, ni mambo yenye umuhimu mkubwa zaidi.
Trump atazuru
Uingereza kama mgeni wa Malkia, ziara iliotangazwa na waziri mkuu
Theresa may alipomtembelea Trump mjini Washington mwezi uliopita.
Lakini
baadhi ya raia wameonyesha mashaka na uharaka wa serikali kuwa karibu
na rais huyo mwenye kuchochea mgawanyiko. waraka wa mtandaoni unaopinga
ziara ya Trump umesainiwa na zaidi ya watu milioni 1.8, na utajadiliwa
bungeni Februari 20.
Mpambano mahakani
Mahakama
nchini Marekani zimesitisha kwa muda marufuku hiyo, na kuzusha maneno
makali kutoka kwa rais huyo anaewasiliana kwa sehemu kubwa zaidi kupitia
mtandao wa twita.
Mahakama ya rufaa mjini San Francisco leo
itasikiliza hoja juu ya iwapo marufuku hiyo irejeshwe, kutoka kwa
mawakili wa wizara ya sheria ya Marekani, na mawakili wa upande
unaopinga kutoka majimbo ya Minnesota na Washington.
Mahakama ya tisa ya rufaa ya Marekani mjini San Francisco, ambayo inasikiliza rufaa kuhusu marufuku ya uhamiaji ya Trump.
Trump
anasema hatua hizo zinalenga kulinda nchi dhidi ya kitisho cha ugaidi,
na kumdhihaki Jaji James Robart aliesitisha marufuku hiyo, na ambaye
aliteuliwa na Mrepublican mwenzake George W. Bush, akimueleza kama
"anaejiita Jaji."
Benki Kuu Ulaya yaonya
Wakati
huo huo, Benki Kuu ya Ulaya ECB imeelezea wasiwasi kuhusu hatua
zinazopangwa kuchukuliwa na utawala wa Trump kulegeza sheria za udhibiti
wa sekta ya benki, ikisema hatua kama hizo zilisaidia kusafisha njia ya
mgogoro wa kifedha duniani.
Rais wa benki hiyo Mario Draghi
alisema wakati wa kikao katika bunge la Ulaya, kwamba haoni sababu
yoyote ya kulegeza sheria hizo zinazofahamika kama sheria za Dodd-Frank,
ambazo zimepelekea kuwepo na sekta imara zaidi ya fedha kuliko
ilivyokuwa kabla ya mgogoro wa mwaka 2007/2008.
No comments:
Post a Comment