Tuesday, September 12, 2017

MASHIRIKA YA KUTETEA HAKI ZA BINADAMU YAIKOSOA UN KWA KUTOCHUKUA HATUA DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU, MYANMAR

Jumuiya na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelikosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kutochukua msimamo imara mbele ya jinai zinazoendelea kufanywa na jeshi na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.
Mashirika hayo yanasema kinachofanyika nchini Myanmar ni maangamizi ya kizazi cha Waislamu wa Rohingya.
Mashirika hayo yameashiria jinai ya kuwalazimisha Waislamu zaidi ya laki tatu wa Myanmar kuyahama makazi yao katika kipindi cha kuanzia tarehe 25 mwezi uliopita na kusisitiza udharura wa kusitishwa uhalifu kama huo. Mashirika hayo pia yamezitaka nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinazotazamiwa kukutana leo mjini New York kwa ajili ya kuchunguza mgogoro wa Myanmar, zichukua hatua za maana katika uwanja huo. 
Waislamu wa Myanmar wakilazimishwa kuhama makazi na vijiji vyao
Siku chache zilizopita pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kusitisha ukatili unaofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.
Tangu Ijumaa ya tarehe 25 Agosti Waislamu wasiopungua elfu 6 na 334 wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuwa na wengine zaidi ya elfu 8 kujeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine.

Friday, September 1, 2017

MAHAKAMA YA JUU KENYA YAAMURU UCHAGUZI MPYA WA RAIS

Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamuru kurejewa kwa uchaguzi wa rais nchini humo, ikiyafuta yale ya awali yaliyokuwa yamempa ushindi Rais Uhuru Kenyatta. 
Kenias Oberstes Gericht (picture-alliance/AP Photo/S. Azim)
Mahakama hiyo imesema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu kwenye uchaguzi wa tarehe 8 Agosti kiasi cha kuvunja hata katiba ya taifa hilo la Afrika Mashariki. 
Uchaguzi mpya umeamuriwa kufanyika ndani ya siku 60 kutoka sasa. 
Mgombea wa upinzani, Raila Odinga, alikuwa amedai kuwa matokeo ya kura kwa njia ya elektroniki yalidukuliwa na kuchakachuliwa kumsaidia Uhuru Kenyatta wa chama tawala, Jubilee. 
Tume ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, ilikuwa imemtangaza Kenyatta mshindi wa asilimia 54 ya kura.
Wakeya kadhaa waliamua kuingia mitaani kupinga matoeo hayo na walikuwa wamedhamiria kuingia tena endapo mahakama ingelipitisha ushindi huu. 
Hii ni mara ya pili kwa Odinga kupinga matokeo mahakamani, lakini mwaka 2013 alishindwa.

TUME YA UCHAGUZI DRC KUTANGAZA RATIBA YA UCHAGUZI

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Corneille Nangaa amesema ratiba ya Uchaguzi mkuu itatangazwa hivi karibuni.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya tume hiyo kutangaza kuwa jumla ya wapiga kura milioni 40 wameandikishwa kwenye majimbo 24 na kwamba kuanzia tarehe nne itaanza kuandikisha wapiga kura kwenye majimbo mawili ya Kasai.
Serikali ya Kinshasa imesema zoezi la kuandikisha wapiga kura litaanza kukamilika kabla ya kutangazwa mambo mengine.
Mapema wiki hii Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) ilisema, zoezi la kuhakiki na kuandikisha wapiga kura wapya kwenye majimbo mawili ya Kasai ambako kumeshuhudiwa machafuko hivi karibuni, litaanza September 4 na kisha kuendelea kwenye majimbo mengine 24
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi CENI, Corneille Nangaa amewataka wananchi kuwasaidia maofisa wake kufanya kazi ya kuandaa uchaguzi kwa uhuru.
Rais Joseph Kabila
Katika hatua nyingine upinzani umekosoa takwimu za hivi karibuni zilitolewa na tume hiyo ukisema kwamba kiwango kikubwa hakiko sawa.
CENI ilisema jumla ya wapiga kura milioni 40 wameandikishwa kwenye majimbo mengine 24 huku taifa hilo likiwa na jumla ya raia milioni 70 wengi wao wakiwa bado hawajaandikishwa.
Mgogoro wa ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliibuka baada ya kuahirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais na kadhalika sisitizo la Rais Joseph Kabila la kutaka kuendelea kubakia madarakani. Licha ya kutiwa saini makubaliano baina ya wapinzani na serikali juu ya kufanyika uchaguzi wa rais tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu, lakini inaonekana kuwa, uchaguzi huo hautaweza kufanyika katika tarehe iliyopangwa.

WAISLAMU 400 WAFARIKI DUNIA MYANMAR KATIKA KIPINDI CHA WIKI MOJA

  • Waislamu 400 wafariki dunia Myanmar katika kipindi cha wiki moja
Waislamu takribani 400 wamefariki dunia nchini Myanmar katika kipindi cha wiki moja tokea jeshi la nchi hiyo lianzishe kampeni mpya ya kuwakandamiza Waisalmu wa jamii ya Rohingya.
Takwimu ramsi zinaonyesha kuwa watu 400 wamepoteza maisha katika jimbo la Rakhine tokea Ijumaa iliyopita. Kati ya walipooteza maisha ni wale waliouliwa na jeshi la nchi hiyo katika oparesheni  dhidi ya Waislamu huku wengine, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wakipoteza maisha wakati wakivuka mto kukimbia mapigano katika jimbo la Rakhine.
Jeshi la Myanmar Ijumaa iliyopita lilianzisha oparesheni kali dhidi ya Waislamu kwa madai kuwa watu wanaodaiwa kuwa ni Waislamu walihujumu vituo vya polisi jimboni Rakhine.
Mabuddha wenye misimamo mikali
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi duniani. 
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Bangladesh, Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

Sunday, July 30, 2017

MAKUMI WAUAWA NA KUJERUHIWA KATIKA MRIPUKO WA MOMU MOGADISHU, SOMALIA

Watu sita wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari kuripuka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Meja Mohamed Hussein, afisa mwandamizi wa polisi nchini humo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa bomu hilo limeripuka katika barabara yenye shughuli nyingi ya Makatul Mukaramah.
Amesema aghalabu ya wahanga wa hujuma hiyo inayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab, ni wapita njia na watu waliokuwa ndani ya maduka yaliyoko kandokando ya barabara hiyo.
Afisa huyo wa polisi ya Somalia ameongeza kuwa, yumkini idadi ya vifo ikaongezeka, kutokana na majeraha mabaya waliyopata baadhi ya wahanga wa shambulizi hilo. 
Askari wa AMISOM
Wakati huohuo, makabiliano makali kati ya askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab yameripotiwa katika wilaya ya Bulamareer, eneo la Shabelle ya Chini, yapata kilomita 140 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na AMISOM au jeshi la Somalia kuhusu idadi ya wahanga wa mapigano hayo, ingawaje genge la al-Shabaab linadai kuwa limeua makumi ya askari wa Umoja wa Afrika.
AbdiAziz Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za al-Shabaab amedai kuwa, kundi hilo la kigaidi limeua wanajeshi 39 wa AMISOM akiwemo kamanda wao.

Friday, July 28, 2017

MAREKANI YARUSHA KOMBORA KUIJIBU KOREA KASKAZINI

Korea Kusini na Marekani wamefanya zoezi la pamoja la kurusha makombora ya ardhini baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio jingine la kombora. Afisa wa Ulinzi wa Marekani alithibitisha kufanyika kwa zoezi hilo la kulipiza kisasi bila ya kutoa taarifa zaidi. Korea Kaskazini ilirusha kombora la masafa marefu linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine hapo jana, ambalo wataalamu wanasema lina uwezo wa kufikia miji kadhaa ya Marekani. Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imesema kombora hilo la Korea Kusini liliruka umbali wa kilomita 1,000 kabla ya kuanguka katika Bahari ya Japan. Rais wa Marekani Donald Trump amelilaani jaribio hilo la pili la Korea Kaskazini la kombora la kuruka kutoka bara moja hadi jingine na kulitaja kuwa ni kitisho kwa ulimwengu.

TRUMP AMTEUA KELLY KUWA MKUU WA UTUMISHI WA SERIKLI

Rais wa Marekani Donald Trump amemteua Waziri wa Usalama wa Ndani John Kelly kuwa mkuu wa utumishi wa serikali baada ya kumwachisha kazi Reince Priebus aliyehudumu katika wadhifa huo kwa miezi sita

Kombobild Reince Priebus und John Kelly (Reuters/J. Roberts)
Baada ya miezi kadhaa ya uvumi kuhusu hatima ya Priebus, Trump alitangaza uamuzi wake kwenye mtandao wa Twitter wakati aliwasili mjini Washington baada ya kutoa hotuba jijini New York ambayo aliitumia kummwagia sifa Kelly kwa kazi anayofanya katika wizara ya Usalama wa Ndani.
Alisema "nna furaha kuwafahamisheni kuwa nimemteua Jenerali/Waziri John F Kelly kuwa Mkuu wa Utumishi wa serikali katika Ikulu ya White House".
Wakati ujumbe huo ulianza kusambaa mjini Washington, Priebus aliondoka katika ndege ya rais Air Force One wakati mvua kubwa ikinyesha na akaingia kwenye gari pamoja na maafisa waandamizi wa Ikulu ya White House Steven Miller na Dan Scavino.
Muda mfupi baadaye, Miller na Scavino walitoka nje ya gari hilo na kuingia kwenye gari jingine. Gari lililombeba Priebus kisha likaondoka pamoja na msafara wa rais.
Priebus, kiongozi wa zamani wa Kamati ya Kitaifa ya chama cha Republican, amekuwa akilengwa na uvumi wa mara kwa mara kuhusu usalama wa kazi yake wakati kukiwa na malumbano ya kindani na sintofahamu ndani ya Ikulu ya White House.
Trump ermuntert Polizisten zu mehr Gewalt (Reuters/J. Ernst)
Trump amewafuta kazi maafisa waandamizi wanane tangu alipoingia madarakani
Mnamo siku ya Alhamisi, alishambuliwa hadharani na mkurugenzi mkuu mpya wa mawasiliano katika Ikulu ya White House aliyeteuliwa na Trump, Anthony Scaramucci ambaye alimtuhumu Prebius kwa kutoa habari za kumharibia jina kwa vyombo vya habari.
Priebus alisema aliwasilisha ombi la kujiuzulu kwake siku ya Alhamisi na kuwa rais alikubali ijapokuwa wale walio karibu na rais huyo walisema kutimuliwa kwake kumekuwa kukishughulikiwa kwa wiki kadhaa sasa.
"nadhani rais alitaka kwenda mkondo tofauti," Priebus aliiambia televisheni ya CNN saa chache tu baada ya kutangazwa kutimuliwa kwake. Aliongeza kuwa anakubali kwamba Ikulu ya White House huenda ikanufaika na hatua ya kufanyiwa marekebisho na akasema "mimi daima ntakuwa shabiki wa Trump. Niko kwenye Team Trump."
Kelly ataapishwa rasmi kuchukua wadhifa huo siku ya Jumatatu. Wizara yake ya Usalama wa Ndani inahusika na kuweka usalama mipakani na amechukua msimamo mkali kuhusu wahamiaji walioko ndani ya Marekani.
Tangu alipoingia katika Ikulu ya White House miezi sita iliyopita, Trump amewaachisha kazi mshauri wake wa usalama wa taifa, naibu mshauri wa usalama wa taifa, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI, msemaji wa ikulu, mkurugenzi wa mawasiliano, naibu mwaneshiria mkuu, naibu mkuu wa utumishi wa serikali na sasa mkuu wa utumishi wa serikali, mabadiliko ya viongozi wakuu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya kisiasa nchini Marekani.