Wakati mazungumzo ya kusaka amani nchini
Burundi yanaendelea mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, makundi
mbalimbali ya kijamii kutoka Burundi yametoa wito wa kutaka
kushirikishwa katika mchakato huo wa kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa
kisiasa.
Hayo
yamekuja baada ya Waswahili wanaounda jamii ndogo ya raia wa Burundi
kufanya maandamano mbele ya ukumbi kunakofanyika mazungumzo hayo jijini
Arusha, wakitaka nao wajumuishwe kwenye meza ya mazungumzo hayo.
Kadhalika jamii hiyo, imemtaka rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin
Willium Mkapa, kutolipuuza suala hilo na kutishia kuwa hawatokuwa tayari
kukubaliana na maamuzi ya mazungumzo ambayo yamewatenga. Hata hivyo
polisi ya Tanzania imewatia mbaroni waandamanaji kadhaa kati yao. Ni
vyema kuashiria kuwa, tangu kulipotiwa saini makubaliano ya amani ya
mjini Arusha miaka kadhaa iliyopita na ambayo yalihitimisha vita vya
miongo kadhaa nchini Burundi, jamii ya Waswahili wa nchi hiyo imekuwa
ikilalamikia kile inachokisema kuwa ni kusahaulika na kutengwa katika
mchakato huo.
Kadhalika jamii hiyo inadai kuwa, kuendelea kutengwa katika maamuzi
ya kuainisha mustakbali wa taifa la Burundi, ni kuzidi kupalilia mzozo
ambao unaweza kuibuka wakati wowote. Katika vita vya kikabila baina ya
jamii ya Watutsi na Wahutu nchini Burundi, maelfu ya watu waliuawa na
wengine wengi kuwa wakimbizi nje ya nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment