Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa
taarifa likilaani vikali matukio ya utumiaji mabavu yaliyotokea katika
miezi ya hivi karibuni huko Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na
kuihimiza serikali ya nchi hiyo kuchunguza mara moja matukio hayo.
Katika taarifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
limeashiria ghasia katika miezi ya hivi karibuni huko Kasai na
kutokana na hali hiyo, wajumbe wa Baraza hilo wamesema wana hofu
kutokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa
kukiwemo wanamgambo kutumikisha watoto vitani na jeshi la serikali kuua
raia.
Wamesema vitendo vyote hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya
sheria za kimataifa hivyo wametaka serikali iwajibike kulinda raia na
ijizuie kutumia nguvu za kijeshi kupita kiasi.
Wameitaka serikali kufanya uchunguzi usioegemea upande wowote na
wahusika wafikishwe mbele ya sheria huku wakisema kuwa ujumbe wa umoja
huo DRC, MONUSCO utakuwa tayari kusaidia iwapo utaombwa kufanya hivyo.
Kuhusu uchaguzi, wajumbe hao wamesisitiza umuhimu wa serikali ya DRC
na wadau wa kitaifa kuchukua hatua zote muhimu za kuandaa uchaguzi huo
bila kuchelewa na kuhakikisha mazingira ni salama kwa uchaguzi huru na
wa haki.
Wametoa wito kwa wadau wa maendeleo wa DRC kusaidia ili kufanikisha
uchaguzi huku wakisema wako tayari kufanikisha utekelezaji wa
makubaliano ya tarehe 31 mwezi Disemba mwaka jana yanayohusisha pia
uchaguzi.
Siku chache zilizopita, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa
Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein aliitaka serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo kuchukua hatua za haraka kusitisha ukiukwaji
mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia
yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo. Alisema kuna habari za kuaminika na
madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo la Kasai ya
Kati na Mashariki na jimbo la lomami, huku kukiwa na kuzorota kwa kasi
hali ya usalama na watu wakilengwa na askari kwa madai ya kuwa na
uhusiano na wanamgambo wa ndani.
No comments:
Post a Comment