Katika hali ambayo juhudi za kuondokana na
mgogoro wa kisiasa nchini Burundi bado zinaendelea, serikali ya
Bujumbura imeiomba Tanzania kuwatia mbaroni wapinzani wake ambao
wanaosakwa na mahakama za nchi hiyo, ambao kwa hivi sasa wako kaskazini
mwa Tanzania.
Bernard Ntahiraja, naibu wa
Alain-Aimé Nyamitwe, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Burundi amesema
kuwa baadhi ya watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi,
walishiriki katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika mjini Arusha
Tanzania kati ya tarehe 16 na 18 za mwezi huu, kwa lengo la kuupatia
ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Jumatano
iliyopita, Philippe Nzobonariba, Msemaji wa Serikali ya Burundi
alitangaza kuwa serikali ya Bujumbura haingeshiriki mazungumzo hayo
kutokana na kile alichosema ni ushiriki wa wapinzani walioshiriki katika
jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza.
Ususiaji wa mazungumzo hayo na serikali ya Burundi umejiri katika hali
ambayo licha ya kupita mwaka mmoja tangu Rais Nkurunziza ashiriki
uchaguzi wa rais kwa muhula wa tatu na kuibuka mshindi, bado mgogoro wa
kisiasa nchini Burundi unaendelea kushuhudiwa. Wapinzani waliitaja hatua
ya rais huyo ya kugombea tena uchaguzi wa rais uliopita kuwa ni kinyume
cha katiba na makubaliano ya Arusha, ambayo yalihitimisha vita vya
ndani nchini Burundi.
Katika kipindi hiki chote mgogoro wa
kisiasa umezidi kushtadi nchini Burundi huku anga ya kisiasa ikizidi
kuharibika. Mauaji ya kuvizia, kamatakamata vitendo vya ukatili na
ukandamizaji dhidi ya wapinzani ni miongoni mwa mambo ambayo
yameshuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Vitendo hivyo vimeifanya jamii ya kimataifa kupiga makelele, huku
viongozi wa serikali ya Bujumbura wakikana katakata tuhuma hizo
wanazoelekekezewa. Licha ya juhudi kubwa za viongozi wa kieneo kufanyika
kupitia upatanishi wa Uganda na Tanzania kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi
mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo, lakini bado viongozi wa chama tawala
cha CNDD-FDD na Rais Pierre Nkurunziza wamekataa kukubaliana na
upatanishi huo. Hii ni katika hali ambayo Rais Nkurunziza amekataa
kuwafungulia njia maripota wa haki za binaadamu kuingia nchini humo.
Katika mazingira hayo, mkwamo wa kisiasa nchini Burundi umezidi kupanuka
huku rais huyo akitumia mkono wa chuma kukabiliana na wapinzani. Katika
fremu hiyo, Rais Nkurunziza amekanusha tuhuma za kuhusika kwake na
mchafukoge na kuzituhumu pande kadhaa ikiwemo Rwanda kuwa zinaingilia
masuala ya ndani ya Burundi kwa kuchochea wapinzani na kuwapatia silaha
kwa ajili ya kuchafua usalama nchini humo, tuhuma ambazo viongozi wa
nchi jirani hususan Rwanda wamekuwa wakizikadhibisha vikali. Hivi sasa
na kwa mara nyingine wapinzani wamekutana nchini Tanzania na kuitaka
serikali ya Bujumbura kushiriki mazungumzo ya amani ya mjini Arusha kwa
ajili ya kujadili matatizo ya kisiasa yanayoikabili nchi yao.
Pamoja na hayo si tu kwamba viongozi wa
serikali wamekataa kushiriki mazungumzo hayo, bali wameitaka serikali ya
Tanzania kuwatia mbaroni wapinzani hao na kisha kuwakabidhi kwa
serikali ya Bujumbura. Kabla ya hapo António Guterres, Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa alitangaza kuwa kumaliza mgogoro wa sasa nchini Burundi
ni kati ya mambo yatakayopewa kipaumbele katika utendajikazi wake. Hata
hivyo inaonekana kuwa viongozi wa chama tawala na rais wa nchi hiyo
mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hawajafungua mlango kwa ajili
ya kufanyika upatanishi na kutatuliwa mzozo uliopo. Hii ni katika hali
ambayo taifa hilo lina kumbukumbu ya kushuhudia vita vya ndani vya
kutisha ambavyo vilisababisha maafa ya maelfu ya watu, ambapo kumetanda
hali ya wasi wasi wa kuibuka tena moto wa vita vingine kama hivyo.
Pamoja na hayo hivi sasa Rais Pierre Nkurunziza kwa kutumia jeshi
anawakandamiza wapinzani wake ambapo matokeo yake ni kupanuka
ukandamizaji huo hadi nje ya mipaka ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment