Licha ya kuendelea ukosefu wa amani huko
Kodivaa katika wiki za hivi karibuni, wanajeshi wa kudumisha amani wa
kofia bluu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa wataondoka nchini humo kwa
mujibu wa jedwali la muda ulioainishwa.
Bi Aichatou Mindaoudou Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa nchini Kodivaa ametangaza kuwa kikosi cha kulinda amani cha
umoja huo huko Kodivaa kitaanza kuondoka nchini kuanzia Februari 15
mwaka huu. Kikosi hicho kilianza shughuli zake nchini humo mwaka 2004
lengo likiwa ni kurejesha huko uthabiti baada ya kupasishwa azimio
nambari 1528 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wanajeshi hao
walisalia Kodivaa kwa miaka kadhaa ili kurejesha amani baada ya nchi
hiyo kukumbwa na mgogoro wa kisiasa. Kikosi cha kudumisha amani cha
Umoja wa Mataifa kilichopo hivi sasa huko Kodivaa kinaundwa na karibu
watu elfu sita wakiwemo raia wa kawaida elfu moja. Pamoja na kuwa
kuondoka huko Kodivaa kikosi hicho cha UN kunafanyika kwa mujibu wa
makubaliano yaliyofikiwa hapo kabla, lakini wanajeshi hao wanajiandaa
kuondoka huku migogoro mikubwa ya kiuchumi na malalamiko ya wananchi
kwa mara nyingine tena ikiiathiri nchi hiyo. Hali hiyo imempelekea
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Kodivaa Bi
Aichatou Mindaoudou kuitolea mwito jamii ya kimataifa kuisaidia Kodivaa
kwa kuzingatia hali ya kiusalama inayolegaega ya nchi hiyo
iliyosababishwa na uasi wa hivi karibuni wa wanajeshi wa nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita wanajeshi waliokuwa wakiushikilia mji
wa Buake huko Kodivaa walianzisha uasi wakiitaka serikali iwaongezee
mishahara na marupurupu mengine. Mbali na wanajeshi hao, wafanyakazi wa
sekta ya umma, wakiwemo wafanyakazi wa idara ya zima moto, wale
waliostaafu na vyama vya ushirika nao vile vile katika wiki za hivi
karibuni wamefanya maandamano na migomo wakitaka kuboreshwa hali ya
uchumi wa nchi hiyo. Mivutano hiyo inapamba moto huku kukiwa na wasiwasi
juu ya uwezekano wa kushtadi malalamiko ya kisiasa na hivyo kuanza tena
maandamano ya kisiasa nchini. Kuboreshwa hali ya uchumi, kuongezwa
mishahara na kupunguza idadi ya watu wasio na ajira ni baadhi ya ahadi
alizotoa Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo wakati wa kampeni za
uchaguzi wa rais.
Hali ya kiuchumi ya Kodivaa haijaboreka licha ya kupita miaka kadhaa,
bali kutekelezwa baadhi ya sheria, ikiwemo ile inayohusiana na
kuongezwa umri wa wastaafu na kuongezwa gharama ya bima kumezidisha
zaidi malalamiko ya wananchi.
Hata kama Kodivaa baada ya kupita miaka kadhaa ya kukabiliwa na
migoro imeendesha uchaguzi huru na wa amani wa rais, lakini katika
kipindi cha miezi ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia maandamano
makubwa khususan ya vyama vya upinzani kufuatia kufanyiwa marekebisho
baadhi ya vipengee vya katiba. Wapinzani wanaamini kuwa sheria hizo mpya
zina lengo la kumuongezea mamlaka Rais Ouattara.
Ouattara kwa upande wake ametoa hakikisho kwamba atashughulia matakwa
yaliyowasilishwa na wananchi. Rais huyo ameendelea kuahidi kwamba
atawaongezea wanajeshi mishahara yao na kuwapatia makazi. Inaonekana
kuwa, Rais Alassane Ouattara na serikali anayoiongaza wanafanya juhudi
kudhibiti migogoro iliyojitokeza nchini. Katika mazingira hayo, kuondoka
huko Kodivaa wanajeshi wa kulinda amani wa kofia bluu wa Umoja wa
Mataifa pia ambako kutaanza siku kadhaa zijazo kumezidisha utata kuhusu
mchakato wa matukio yanayojiri nchi hiyo. Kuendelea mivutano huko
Kodivaa pia kumezidisha uwezekano wa kushtadi machafuko na ukosefu wa
amani nchini humo.Sababu hiyo imewafanya baadhi ya wachambuzi wa mambo
wasisitize kuendelea kubaki huko Kodivaa wanajeshi wa kofia bluu wa
Umoja wa Mataifa; hata hivyo uzoefu unaonyesha kuwa njia zote za
kudumisha amani na uthabiti haziishii kwa nafasi ya askari jeshi wa
kulinda amani wa umoja huo, bali hatua nyingine pia zinapaswa
kuchukuliwa ili kuboresha hali ya usalama nchini humo.
No comments:
Post a Comment