Monday, February 13, 2017

RAIS MTEULE WA UJERUMANI: TRUMP NI MSHIRIKA MKOROFI

Rais mteule wa Ujerumani ametoa matamshi makali dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani na kusema kuwa ni rafiki mkorofi anayeeneza chuki ulimwenguni.
Frank-Walter Steinmeier ambaye juzi Jumapili alichaguliwa na Bunge la Ujerumaini kuwa rais wa nchi hiyo ya Ulaya ameiambia televisheni ya ZDF ya Ujerumaini kwamba moja ya ajenda zake kuu wakati wa kipindi chake cha urais itakuwa ni kufanya mazungumzo na Russia na Marekani.
Steinmeier amesema, ingawa ameamua ajenda ya kazi zake itakuwa ni kufanya mazungumzo na Marekani, lakini anajua pia kuwa, Donald Trump atakuwa mshirika mkorofi kwenye mazungumzo hayo.
Maandamano ya kupinga siasa za kibaguzi za Trump yanaendelea kwenye miji ya nchi mbalimbali duniani

Rais mpya wa Ujerumaini alikuwa akimkosoa sana Donald Trump wakati wa kampeni za uchaguzi wa Marekani akimwita kuwa ni muhubiri wa chuki na uhasama duniani.
Amesema pia kuwa wakati wa kipindi cha urais wake, atajaribu kuielekeza Ujerumaini upande wa kufanya mazungumzo na Russia.
Kwa upande wake, Rais Vladmir Putin wa Russia amempongeza Steinmeier kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa ujerumaini na kumwalika atembelee Moscow. 
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Russia, Kremlin imesema, Putin ana matumaini kwamba Steinmeier atatoa mchango mkubwa wa kuboresha uhusiano na ushirikiano baina ya Berlin na Moscow. Steinmeier atachukua rasmi urais wa Ujerumani katikati ya mwezi ujao wa Machi.

No comments:

Post a Comment