Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran,
Bahram Qassemi ameashiria mashambulio ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen
yaliyoanza Machi mwaka 2015 na kuendelea hadi sasa na kueleza kwamba
Wayemeni wana silaha nyingi sana ambapo bila ya kuzingaia ukweli huo,
Saudia ilidhani itaweza kuhatimisha vita hivyo kwa manufaa yake ndani ya
kipindi kifupi mno.
Qassemi ameyaeleza hayo katika mahojiano na jarida la
Al-Arabiyyul-Jadidah linalochapishwa London, Uingereza. Katika mahojiano
hayo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amekanusha uvumi kwamba
Iran inaisaidia Yemen kwa silaha na kufafanua kwamba baadhi ya nchi
zinaituhumu Iran kuwa inapeleka silaha kimagendo Yemen hali ya kuwa kwa
upande mmoja, Tehran haijajiingiza kijeshi wala kifedha katika mgogoro
wa nchi hiyo na kwa upande mwengine Wayemeni hawahitaji silaha za Iran.
Aidha amesisitiza kwamba Saudia inapaswa iache tuhuma na siasa zake
za kiadui dhidi ya Iran na kwamba endapo itafanya hivyo Tehran
iko tayari kufanya mazungumzo ya pande mbili na Riyadh.
Kutangazwa habari za kutumwa silaha kimagendo nchini Yemen kutokea
Iran ni upatu unaopigwa na mashirika na vyombo vya habari vya eneo kila
baada ya muda ili kupata kisingizio cha kuyakariri madai kwamba Jamhuri
ya Kiislamu inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Hata hivyo madai
hayo katu hayajaweza kuthibitishwa; na hata Umoja wa Mataifa pia umekiri
kuwa hakuna silaha yoyote iliyotumwa kutoka Iran na kupelekewa
makundi yanayopigana nchini Yemen. Hata hivyo tuhuma zinazotolewa dhidi
ya Iran zinaweza kuwa na malengo mawili. Lengo la kwanza ni kujenga
hisia kuwa Iran ina nafasi hatarishi katika eneo. Kwa kutumia kisingizio
hicho, Saudia inataka kuonyesha kuwa vita vamizi ilivyoanzisha dhidi ya
Yemen na mauaji ya kinyama inayoendelea kufanya kila siku dhidi ya raia
wasio na hatia wa nchi hiyo ni vita vyenye uhalali wa kisheria. Ilhali
ukweli ni kwamba uvamizi wa Saudia tokea mwanzo wake ulikuwa na sura ya
kichokozi wala hakuna njia yoyote ya kuutetea na kuuhalalisha uvamizi
huo.
Madai ya kupelekewa silaha harakati ya Ansarullah ambayo kwa kweli
inatetea matakwa ya wananchi wa Yemen na kupambana na wavamizi
yanatolewa na nchi kama Saudi Arabia na Uingereza. Nchi kama Uingereza
inaipatia Saudia silaha zilizopigwa marufuku izitumie katika vita vya
Yemen na kimsingi inapaswa kuwajibika kwa hatua yake hiyo. Lakini lengo
la pili la kuzushwa madai ya utumaji silaha Yemen kutokea Iran ni
kufifilisha kushindwa na kugonga mwamba njama ya Saudia ya kutaka
kuidhibiti Yemen. Licha ya kupindukia muda wa miaka miwili tangu
ilipoanzisha mashambulio na hujuma za mtawalia dhidi ya Yemen ambazo
zimeteketeza miundombinu ya miji, barabara, madaraja na bandari, mbali
na kumwaga damu na kuua maelfu ya watu, Saudi Arabia ingali imeshindwa
kuidhibiti nchi hiyo huku yenyewe ikiendelea kupata kipigo kikali kutoka
kwa muqawama wa wananchi wa Yemen.
Kwa hivyo suala la Yemen linapaswa kuangaliwa kwa upande mwengine. Ni
wazi kuwa katika kadhia hiyo umoja wa ardhi yote ya Yemen umevamiwa
waziwazi, na lengo la utawala wa Aal Saud ni kuigawa na kuikalia kwa
mabavu nchi hiyo masikini ya Kiarabu au kuyaunganisha baadhi ya maeneo
yake na ardhi ya Saudia. Kitambo nyuma televisheni ya utawala wa Aal
Saud ilionyesha ramani ya maeneo yaliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu
nchini Yemen na kuyaelezea kuwa ni sehemu ya ardhi ya Saudi Arabia. Kwa
hivyo kujitoa kimasomaso utawala wa Aal Saud hakuwezi kubadilisha ukweli
halisi wa mambo.
Lililo wazi ni kuwa vita vamizi na vya kichokozi vilivyoanzishwa na
Saudia dhidi ya Yemen vimezidi kuvuruga amani katika eneo la Mashariki
ya Kati. Mashambulio na hujuma za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia
vimeshamirisha ugaidi na kuwafanya mamia ya maelfu ya raia kupoteza
makazi yao na kuwa wakimbizi. Pamoja na hayo ungangari na kusimama imara
wananchi na viongozi wa Yemen katika kukabiliana na ugaidi na uvamizi
haujatoa ruhusa kwa wavamizi kuzidi kusonga mbele ndani ya ardhi ya nchi
hiyo. Inapasa kusema kuwa Iran, ambayo ni nchi yenye nguvu katika eneo
hili na yenye kutoa mchango chanya na athirifu haina haja ya kuingilia
masuala ya ndani ya nchi nyengine. Kama ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran imeunga mkono utatuzi wa kisiasa katika mgogoro wa Syria inaunga
mkono pia njia za kisiasa kama suluhisho pekee la kuutatua mgogoro
unaoendelea nchini Yemen.../
No comments:
Post a Comment