Waziri Mkuu wa zamani wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmaajo ameshinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika jana nchini humo..
Farmaajo alitangazwa mshindi baada ya Hassan Sheikh
Mohamud aliyekuwa akitetea kiti hicho kukubali kushindwa katika duru ya
pili ya uchaguzi wa rais wa Somalia uliowashirikisha wabunge.
Farmaajo hakuweza kupata thuluthi mbili ya kura zilizohitajika kwa
ajili ya kushinda uchaguzi huo baada ya kupata kura 184 mkabala na 97 za
mpinzani wake, Hassan Sheikh Mohamud katika duru ya pili ya uchaguzi
huo lakini akatangazwa mshindi baada ya rais anayeondoka kujiondoa
katika duru ya tatu.
Uchaguzi huo wa rais nchini Somalia ulifanyika Jumatano ya jana
ukiwashirikisha wagombea 22 baada ya kuakhirishwa mara kadhaa. Punde
baada ya kutangazwa mshindi, Farmaajo alikula kiapo kama rais mpya wa
Somalia. Kwa sasa rais wa Somalia anachaguliwa na wabunge kutokana na
hali mbaya ya usalama nchini humo.
Wabunge wa Somalia kutoka mabunge mawili ya nchi hiyo wamempigia kura
rais wakiwa katika kituo cha jeshi la anga huku kukiwa na ulinzi mkali
kote katika mji mkuu Mogadishu kutokana na hofu ya magaidi wa Al Shabab
kushambulia na kuvuruga uchaguzi huo.
Kundi hilo la kitakfiri la Al Shabab lilikuwa limetoa taarifa na
kuwataka wafuasi wake wawaue wale wote watakaoshiriki katika uchaguzi
huo na kwa msingi huo mji wa Mogadishu ulikuwa na ulinzi mkali kuanzia
Jumanne. Pamoja na hayo magaidi wa Al Shabaab walitekeleza hujuma katika
uwanja wa ndege wa mji huo.
Kwa kuzingatia hali ya hivi sasa ya Somalia, Farmaajo atakabaliwa na
changamoto nyingi sana. Hivi sasa Somalia ina matatizo mengi ya kiuchumi
na kiusalama na kwa msingi huo Wasomali wengi wanataraji kuwa serikali
mpya itazingatia na kulipa kipaumbele suala la kuimarisha jeshi na
vikosi vingine vya usalama ili kurejesha uthabiti chini humo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM kimeshindwa kurejesha amani Somalia.
Kupunguza mishahara ya wabunge na kuongeza mishahara ya vikosi vya
usalama ni kati ya matakwa muhimu ya wananchi ili vikosi hivyo viwe na
motisha katika kurejesha amani nchini humo.
Pamoja na hayo, uingiliaji wa madola ya kigeni na hitilafu za ndani
ya nchi ni kati ya sababu kuu ambazo zimepelekea utulivu kukosekana
Somalia.
Kutokana na umuhimu wake wa kistratijia katika Pembe ya Afrika na
Lango Bahari la Babul Mandab ambalo ni njia muhimu ya kupita meli za
mafuta na mizigo duniani, Somalia imekuwa ikikodoelwa macho ya tamaa na
madola ya kibeberu.
Hali kadhalika mfumo uliokita mizizi wa kiukoo ni jambo jingine
ambalo limepelekea uthabiti kosekana Somalia kwa muda wa karibu miaka 25
sasa. Malumbano ya koo mbali mbali Somalia ni jambo ambalo limepelekea
iwe vigumu kupatikana serikali ya mshikamano wa kitaifa nchini.
Mbali na malumbano hayo ya kiukoo, pia kuna hitilafu za kisiasa miongoni mwa wanasiasa na wanaharakati nchini humo.
Baada ya kuanguka serikali ya Siad Barre mwaka 1992, Somalia
ilishuhudia kuibuka na kuenea kwa kasi pote la ukufurushaji la Uwahhabi
kutokana na uungaji mkono wa Saudi Arabia. Pote hilo ambalo lina ufahamu
usio sahihi wa Uislamu hasa kuwakufurisha wasiokubaliana na itiakdi zao
ni sababu nyingine ya matatizo ya sasa ya Somalia kwa kuzingatia kuwa
kundi la kigaidi la Al Shabab linafuata itikadi hiyo ya Kiwahhabi.
Mbali na tatizo hilo hivi sasa nchini Somalia kuna makundi kadhaa ya
wanasiasa wakiwemo wale wa kiliberali wanaofungamana na nchi za
Magharibi na wale ambao wanaunga mkono utawla ulioangushwa wa Siad
Barre. Wanasiasa wa kiliberali wanaamini kuwa, kufuata mfumo na mtindo
wa maisha sawa na wa nchi za Magharibi ndio njia pekee ya kuleta umoja
wa kitaifa Somalia. Kundi la wanasiasa wanaofadhilisha mfumo uliokuwepo
wakati wa Said Barre wanataka mfumo wa kisochialisti nchini humo. Mrengo
wa tatu wa kisiasa Somalia ni ule unaofuata utaifa wa Kisomali na
unataka maeneo yote yaliyojitangazia uhuru yarejee katika Somalia moja.
Kwa kuzingatia tafauti hizo za kiukoo, kisiasa na kidini zilizopo
nchini Somalia, itakuwa changamoto kubwa kuweza kurejesha uthabiti wa
kudumu katika nchi hiyo muhimu ya Pembe ya Afrika.
No comments:
Post a Comment