Sunday, July 30, 2017

MAKUMI WAUAWA NA KUJERUHIWA KATIKA MRIPUKO WA MOMU MOGADISHU, SOMALIA

Watu sita wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari kuripuka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Meja Mohamed Hussein, afisa mwandamizi wa polisi nchini humo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa bomu hilo limeripuka katika barabara yenye shughuli nyingi ya Makatul Mukaramah.
Amesema aghalabu ya wahanga wa hujuma hiyo inayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi la al-Shabaab, ni wapita njia na watu waliokuwa ndani ya maduka yaliyoko kandokando ya barabara hiyo.
Afisa huyo wa polisi ya Somalia ameongeza kuwa, yumkini idadi ya vifo ikaongezeka, kutokana na majeraha mabaya waliyopata baadhi ya wahanga wa shambulizi hilo. 
Askari wa AMISOM
Wakati huohuo, makabiliano makali kati ya askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab yameripotiwa katika wilaya ya Bulamareer, eneo la Shabelle ya Chini, yapata kilomita 140 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na AMISOM au jeshi la Somalia kuhusu idadi ya wahanga wa mapigano hayo, ingawaje genge la al-Shabaab linadai kuwa limeua makumi ya askari wa Umoja wa Afrika.
AbdiAziz Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za al-Shabaab amedai kuwa, kundi hilo la kigaidi limeua wanajeshi 39 wa AMISOM akiwemo kamanda wao.

Friday, July 28, 2017

MAREKANI YARUSHA KOMBORA KUIJIBU KOREA KASKAZINI

Korea Kusini na Marekani wamefanya zoezi la pamoja la kurusha makombora ya ardhini baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio jingine la kombora. Afisa wa Ulinzi wa Marekani alithibitisha kufanyika kwa zoezi hilo la kulipiza kisasi bila ya kutoa taarifa zaidi. Korea Kaskazini ilirusha kombora la masafa marefu linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine hapo jana, ambalo wataalamu wanasema lina uwezo wa kufikia miji kadhaa ya Marekani. Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imesema kombora hilo la Korea Kusini liliruka umbali wa kilomita 1,000 kabla ya kuanguka katika Bahari ya Japan. Rais wa Marekani Donald Trump amelilaani jaribio hilo la pili la Korea Kaskazini la kombora la kuruka kutoka bara moja hadi jingine na kulitaja kuwa ni kitisho kwa ulimwengu.

TRUMP AMTEUA KELLY KUWA MKUU WA UTUMISHI WA SERIKLI

Rais wa Marekani Donald Trump amemteua Waziri wa Usalama wa Ndani John Kelly kuwa mkuu wa utumishi wa serikali baada ya kumwachisha kazi Reince Priebus aliyehudumu katika wadhifa huo kwa miezi sita

Kombobild Reince Priebus und John Kelly (Reuters/J. Roberts)
Baada ya miezi kadhaa ya uvumi kuhusu hatima ya Priebus, Trump alitangaza uamuzi wake kwenye mtandao wa Twitter wakati aliwasili mjini Washington baada ya kutoa hotuba jijini New York ambayo aliitumia kummwagia sifa Kelly kwa kazi anayofanya katika wizara ya Usalama wa Ndani.
Alisema "nna furaha kuwafahamisheni kuwa nimemteua Jenerali/Waziri John F Kelly kuwa Mkuu wa Utumishi wa serikali katika Ikulu ya White House".
Wakati ujumbe huo ulianza kusambaa mjini Washington, Priebus aliondoka katika ndege ya rais Air Force One wakati mvua kubwa ikinyesha na akaingia kwenye gari pamoja na maafisa waandamizi wa Ikulu ya White House Steven Miller na Dan Scavino.
Muda mfupi baadaye, Miller na Scavino walitoka nje ya gari hilo na kuingia kwenye gari jingine. Gari lililombeba Priebus kisha likaondoka pamoja na msafara wa rais.
Priebus, kiongozi wa zamani wa Kamati ya Kitaifa ya chama cha Republican, amekuwa akilengwa na uvumi wa mara kwa mara kuhusu usalama wa kazi yake wakati kukiwa na malumbano ya kindani na sintofahamu ndani ya Ikulu ya White House.
Trump ermuntert Polizisten zu mehr Gewalt (Reuters/J. Ernst)
Trump amewafuta kazi maafisa waandamizi wanane tangu alipoingia madarakani
Mnamo siku ya Alhamisi, alishambuliwa hadharani na mkurugenzi mkuu mpya wa mawasiliano katika Ikulu ya White House aliyeteuliwa na Trump, Anthony Scaramucci ambaye alimtuhumu Prebius kwa kutoa habari za kumharibia jina kwa vyombo vya habari.
Priebus alisema aliwasilisha ombi la kujiuzulu kwake siku ya Alhamisi na kuwa rais alikubali ijapokuwa wale walio karibu na rais huyo walisema kutimuliwa kwake kumekuwa kukishughulikiwa kwa wiki kadhaa sasa.
"nadhani rais alitaka kwenda mkondo tofauti," Priebus aliiambia televisheni ya CNN saa chache tu baada ya kutangazwa kutimuliwa kwake. Aliongeza kuwa anakubali kwamba Ikulu ya White House huenda ikanufaika na hatua ya kufanyiwa marekebisho na akasema "mimi daima ntakuwa shabiki wa Trump. Niko kwenye Team Trump."
Kelly ataapishwa rasmi kuchukua wadhifa huo siku ya Jumatatu. Wizara yake ya Usalama wa Ndani inahusika na kuweka usalama mipakani na amechukua msimamo mkali kuhusu wahamiaji walioko ndani ya Marekani.
Tangu alipoingia katika Ikulu ya White House miezi sita iliyopita, Trump amewaachisha kazi mshauri wake wa usalama wa taifa, naibu mshauri wa usalama wa taifa, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI, msemaji wa ikulu, mkurugenzi wa mawasiliano, naibu mwaneshiria mkuu, naibu mkuu wa utumishi wa serikali na sasa mkuu wa utumishi wa serikali, mabadiliko ya viongozi wakuu ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia ya kisiasa nchini Marekani.

MAREKANI YAIWEKEA TENA VIKWAZO IRAN

Marekani imeendeleza uadui wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuziwekea vikwazo taasisi 6 za Kiirani.
Wizara ya Fedha ya Marekani usiku wa kuamkia leo imeziwekea vikwazo taasisi hizo sita za Kiirani kwa kisingizio cha majaribio yaliyofanywa juzi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya roketi la kutuma satalaiti angani la Simorgh ambayo inahusiana kikamilifu na masuala ya kielimu na kisayansi.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani imesema kuwa: Mali na milki za taasisi hizo sita za Iran katika ardhi ya Marekani zinazuiliwa, na taasisi za fedha za kigeni zinazuiwa kufanya muamala wowote na taasisi hizo.
Roketi la kubeba satalaiti angani la Simorgh lilizinduliwa Alkhamisi iliyopita kwa mafanikio katika Kituo cha Masuala ya Anga cha Imam Khomeini. Roketi hilo lina uwezo wa kupeleka angani satalaiti yenye uzito wa kilo 250 umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini. 
Uzinduzi wa roketi la Simorgh, Iran
Siku chache zilizopita pia Kongresi ya Marekani ilipasisha mpango wa vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vilevile tarehe 18 mwezi huu wa Julai Wizara ya Fedha ya Marekani iliwawekea vikwazo watu na taasisi 18 za Iran na nchi za kigeni kwa kutumia visingizio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na uhusiano na miradi ya kutengeneza makombora ya Iran. 
Tangu iliposhika madaraka nchini Marekani, Serikali ya Donald Trump imezidisha uhasama na uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

Friday, July 21, 2017

AL AZHAR YAONYA KUHUSU KUENDELEA ISRAEL KUUVUNJIA HESHIMA MSIKITI WA AL AQSA

  • Askari wa Israel hawawahurumii hata akinamama wanaokwenda kusali Masjidul Aqswa
Chuo Kikuu cha al Azhar cha nchini Miri kimeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na jinai unazozifanya pambizoni mwa Msikiti wa al Aqsa kwani jinai hizo zinawaumiza Waislamu wote duniani.
Chuo Kikuu cha al Azhar cha nchini Misri kilitoa tamko hilo jana Ijumaa huku taifa madhlumu la Palestina likiendelea kusimama kidete kukihami Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Wanajeshi wa Israel wakiwapiga risasi waandamanaji wa Palestina.
Katika tamko lake hilo al Azhar imeutaka ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na taasisi za kieneo na kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuuokoa Msikiti wa al Aqsa mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni.
Tamko la chuo kikuu hicho cha Kiislamu cha nchini Misri limeongeza kuwa, al Azhar inalaani kwa nguvu zake zote uchochezi wote unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Waislamu wa Palestina waliokuwa wanasali na vile vile vitendo vya kikatili na kinyama vya Wazayuni ambavyo vimepelekea kujeruhiwa makumi ya Waislamu wa Palestina akiwemo khatibu wa Masjidul Aqswa, Sheikh Ekrima Sa'id Sabri.
Baada ya vijana watatu wa Kipalestina kufanya operesheni ya kujitolea kufa shahidi dhidi ya Wazayuni katika mji wa Quds siku ya Ijumaa ya tarehe 14 Julai, utawala wa Kizayuni wa Israel uliufunga msikiti huo na kuwazuia Waislamu kuingia msikitini humo kwa muda wa siku mbili.
Vijana wa Palestina wakikabiliana na wanajeshi wa Israel waliojizatiti kwa silaha nzito. Licha ya kuwa mikono mitupu, Wapalestina wameapa kusimama imara kukilinda Kibla cha Kwanza cha Waislamu

Siku ya Jumapili, wanajeshi wa Israel walifungua milango ya msikiti huo lakini kwa masharti magumu ambayo Waislamu wa Palestina wameyapinga na kwa mara ya kwanza, jana Ijumaa, Wazayuni walizuia kusaliwa Sala ya Ijumaa ndani ya msikiti huo mtakatifu. Waislamu walimiminika katika maeneo ya karibu na msikiti huo kutekeleza ibada ya Sala ya Ijumaa, lakini hata hivyo hawakusalimika na ukatili wa Wazayuni.
Viongozi wengi wa nchi za Kiislamu na kimataifa wamelaani jinai hizo za Wazayuni na kuilaumu Israel kwa kutekeleza njama zake za muda mrefu dhidi ya Kibla cha Kwanza cha Waislamu kwa kutumia kisingizio cha opereseheni ya kujitolea kufa shahidi vijana hao watatu wa Palestina.