Mazungumzo ya amani ya Syria chini ya usimamizi wa
Umoja wa Mataifa yanaendelea jijini Geneva, miezi kumi baada ya
kusambaratika kuhusiana na umwagaji damu unaoendelea katika nchi hiyo
iliyoharibiwa na vita
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura alifanya
mikutano tofauti na wawakilishi wa ujumbe wa serikali na upinzani leo
asubuhi katika ofisi za Umoja wa Mataifa nchini Uswisi. Siku moja kabla,
Mwanadiplomasia huyo alipuuza matumaini ya kupatikana makubaliano ya
moja kwa moja katika mazungumzo hayo, lakini pande zote zinafahamu kuwa
mienendo nchini Syria imebadilika tangu mazungumzo yaliandaliwa mara ya
mwisho Geneva mwezi Aprili.
De Mistura anataka pande zote
kujadili uwezekano wa kuundwa serikali ya pamoja ya mpito, katiba mpya
na kuandaliwa uchaguzi. Duru za upinzani zimesema mikutano ya kwanza leo
ilihusu ufafanuzi wa ajenda halisi ya mazungumzo hayo. Mmoja wa wajumbe
wa upinzani Abdulahad Astepho amesema waasi watakuwa na jukumu kubwa
katika duru hii ya mazungumzo.
De Mistura asema kuna matumaini madogo kwenye mazungumzo hayo ya amani ya Syria, jijini Geneva
Mazungumzo
ya Geneva yanakuja baada ya mashauriano ya Astana, mji mkuu wa
Kazakhstan, ambayo yaliratibiwa kwa kiasi kikubwa na Uturuki, mshirika
wa karibu wa upinzani katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe, na
Urusi, ambayo mashambulizi yake ya angani yanawasaidia wanajeshi wa
sewrikali ya Rais Bashar al-Assad. Ni duru ya nne ya mazungumzo
yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa tangu mapema mwaka jana.
Wakati
hayo yakijiri, wanaharakati wameripoti leo kutokea mashambulizi makali
katika mji wa kusini wa Daraa baina ya wanajeshi wanaoiunga mkono
serikali na makundi ya upinzani yanayoongozwa na kundi la al-Qaeda.
Mashirika ya habari ya upinzani pia yameripoti mashambulizi ya anga
yaliyofanywa na serikali karibu na eneo la Hama, katikati ya Syria.
Serikali
inasisitiza kuwa mpango wa kusitisha mapigano hauyalindi makundi yenye
mafungamano na mtandao wa al-Qaeda, wakati waasi wanasema makubaliano
waliyosaini mjini Ankara yanayahusisha makundi hayo.
Nalo shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF limetoa wito kwa
pande zote katika mgogoro wa Syria kuwalinda watoto katika nchi hiyo
iliyoharibiwa na vita. Karibu watoto milioni 10 wa Kisyria wanaoteseka
moja kwa moja na madhara ya kila siku ya mgogoro huu mkubwa wanataka
kitu kimoja tu: amani irejee na wafurahie tena maisha yao ya utotoni.
No comments:
Post a Comment