Tuesday, June 27, 2017

IRAN YALAANI UAMUZI WA MAHAKAMA KUU YA MAREKANI DHIDI YA WAISLAMU

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Marekani dhidi ya Waislamu na kusema kuwa, kutokana na mitazamo yake finyu ya kibiashara, Washington imefumbia jicho wasababishaji halisi wa ugaidi nchini Marekani na kutoa ujumbe usiofaa.
Bahram Qassemi amesema kuwa, uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Marekani dhidi ya Waislamu ni kielelezo cha mienendo ya kibaguzi ya serikali ya Washingon dhidi ya Waislamu na mtazamo usio wa kiadilifu kuhusu wafuasi wa dini hiyo. 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, mtazamo wa watawala wa Marekani kuhusu Waislamu wanaofanya safari au wanaoishi nchini Marekani daima umekuwa mbaya, wa dharau na kuwadhalilisha wafuasi wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu ambao kwa mujibu wa ushahidi wa historia wamekuwa wakiheshimu sheria, kuishi kwa amani na kujiehpusha na vitendo vya utumiaji mabavu na misimamo mikali.
Maandamano ya kupinga amri ya Trump, Marekani
Mahakama Kuu ya Marekani Jumatatu iliyopita iliiruhusu serikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kutekeleza sehemu ya amri ya kuwazuia Waislamu wa nchi kadhaa kuingia katika ardhi ya nchi hiyo. 
Amri hiyo ya Trump haikuwahusisha raia kutoka nchi kama Saudi Arabia na washirika wake ambazo ndiyo waleaji na waungaji mkono wa makundi ya kigaidi. 

IRAN: NJAMA MPYA ZA MAREKANI DHIDI YA SYRIA NI KWA MANUFAA YA MAGAIDI

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kitendo cha Marekani cha kuzusha vurugu mpya nchini Syria kwa kutegemea madai ya uongo, si kwa faida ya yeyote isipokuwa magaidi wa ISIS.
Itakumbukwa kuwa, mapema leo alfajiri, Sean Spicer, msemaji wa Ikulu ya Marekani (White House) amedai bila ya ushahidi wowote kwamba, iwapo Syria itafanya shambulio la kemikali, basi italazimika kutoa gharama kubwa ya shambulio hilo.
Chuki za kidini dhidi ya Waislamu zimeongezeka sana nchini Marekani hasa baada ya kuingia madarakani Donald Trump mwenye chuki kubwa na Waislamu
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Tweeter kwamba, njama za Marekani za kuzusha vurugu mpya nchini Syria kwa madai ya uongo ni kwa manufaa ya magaidi wa Daesh tu tena katika wakati huu ambapo genge hilo linazidi kuangamizwa na wananchi wa Iraq na Syria.
Kambi ya jeshi la anga ya Shayrat nchini Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesema kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani wa kuruhusu kutekelezwa siasa za rais wa Marekani, Donald Trump za kupiga marufuku raia wa nchi za Kiislamu kuingia nchini Marekani, hauwezi kuidhaminia Marekani usalama wake. Pia amesema, inachotakiwa kufanya Marekani ni kuachana na siasa za misimamo mikali na kujiunga na wale wanaopambana kikweli na misimamo hiyo.
Licha ya rais wa Marekani kuwa na chuki kubwa dhidi ya Waislamu, lakini viongozi wa Saudi Arabia walimkaribisha Riyadh kwa heshima zote. Hapa mfalme Salman wa Saudi Arabia akicheza ngoma kwa furaha tele pamoja na Trump mjini Riyadh

Jana Jumatatu, Mahakama Kuu ya Marekani iliiruhusu serikali ya Donald Trump itekeleze marufuku yake ya siku 90 ya kuingia nchini Marekani raia wa nchi za Kiislamu za Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen. Katika miezi ya Januari na Machi 2017, Trump alitoa amri ya kuzuiwa kuingia Marekani raia wa nchi hizo sita za Kiislamu. Hata hivyo hadi hivi sasa amri hiyo ilikuwa imekwama kutokana na majimbo mbalimbali ya Marekani kukataa kuitekeleza.  

Monday, June 26, 2017

KIONGOZI MUADHAMU. MATUKIO YA YEMEN NA BAHRAIN NI JERAHA KUBWA KWA ULIMWENGU WA KIISLAMU

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, matukio yanayojiri nchini Yemen na Bahrain ni jeraha kubwa linaoukabili umma wa Kiislamu na ameutaka ulimwengu wa Kiislamu kulisaidia kwa hali na mali taifa ya Yemen.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi katika hotuba aliyoitoa baada ya swala ya Iddil-Fitri iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran ambapo ameutaka umma wa Kiislamu kusimama imara na kuisaidia Yemen kwa namna ya wazi  kabisa kutokana na ukatili inaofanyiwa. Amesisitiza kwa kusema: "Ni lazima maulamaa wa Kiislamu wachukue hatua kuhusiana na kinachojiri katika baadhi ya nchi za Kiislamu hata kama suala hilo litawakasirisha makafiri."
Kiongozi Muadhamu Sayyid Ali Khamenei akiswalisha swala ya Iddil-Fitri
Kadhalika amezungumzia mafanikio mbalimbali ya kimaanawi yaliyopatikana ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani uliomalizika jana Jumapili, yakiwemo matendo ya ibada na kusema kuwa, shambulio la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH dhidi ya magaidi katika mji wa Deir Ezzor nchini Syria, ni amali tukufu ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kushiriki kwa wingi watu katika matembezi ya siku hiyo tukufu ni miongoni mwa matukio muhimu yaliyotokea ndani ya mwezi humo mtukufu wa Ramadhani. Swala ya Iddul-Fitri nchini Iran imeswalishwa kitaifa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei hapa Tehran, ambapo idadi kubwa ya Waislamu wa mji wa Tehran wameshiriki swala hiyo.
Mashambulizi makali yanayofanywa na Saudia, Israel na Marekani dhidi ya Yemen
Ni zaidi ya miaka mitatu sasa ambapo taifa la Yemen linashuhudia mashambulizi makali na mzingiro wa kila upande wa Saudia na washirika wake wa nchi Kiarabu kwa baraka kamili za Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Ulaya.

Tuesday, June 13, 2017

WATU 15 BAADA YA JENGO KUPOROMOKA

Watu 15 hadi sasa hawajulikano waliko baada ya jengo la ghorofa saba kuporomoka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi Jumatatu usiku.
Kamanda wa Polisi Nairobi Japheth Koome anasema watu 121 waliokolewa punde baada ya jingo hilo kuporomoka saa nne usiku katika mtaa wa Kware eneo la Embakasi mashariki mwa Nairobi.
Koome amesema kuna wakaazi takribani 15 wa jengo hilo ambao hawajulikano waliko kwani baadhi walikataa kuondoka wakati walipotakiwa kufanya hivyo jengo lilipoonekana linaelekea kuporomoka.
Msemaji wa Idara ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa  Pius Masai amesema familia nyingi zilishirikiana na kuweza kuondolewa katika jengo hilo lakini bado waokoaji wanajaribu kuwatafuta watu wanaoaminika kufunikwa na vifusi.
  • Gavana wa Nairbi Evans Kidero alitembelea eneo la tukio na kusema jengo hilo limejengwa kinyume cha sharia. Aidha amesema majengo 30,000 Nairobi yanatakiwa kubomolewa kwa sababu yamejengwa kwa viwango duni na ni hatari kwa maisha ya wakazi. Mwaka jana watu 50 walipoteza maisha wakati jengo lilipoporomoka katika mtaa wa Huruma mjini Nairobi.

Monday, June 12, 2017

MACRON ANYEMELEA USHINDI UCHAGUZI WA BUNGE UFARANSA

Wapiga kura nchini Ufaransa wamerudi tena vituoni Jumapili (11.06.2017) kwa duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge ambayo inatabiriwa utakipa chama cha mrengo wa wastani cha Rais Emmanuel Macron wingi wa viti bungeni.

Frankreich Staatspräsident Macron wählt in Le Touquet (Reuters/C. Petit Tesson)
Wapiga kura nchini Ufaransa wamerudi tena vituoni Jumapili (11.06.2017) kwa duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge ambayo inatabiriwa utakipa chama cha mrengo wa wastani cha Rais Emmanuel Macron wingi wa viti bungeni.
Macron amekuwa akifurahia fungate ya kisiasa tokea alipomshinda mgombea wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen na kuja kuwa rais kijana kabisa wa Ufaransa kuwahi kutokea hapo Mei 7 na kutangaza baraza la mawaziri lisilojikita katika mgawanyiko ulioko  kati ya sera za mrengo wa kulia na kushoto pamoja na kuonekana kujiamini katika mikutano yake na Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Lakini rais huyo amefanya nusu tu ya kazi.Chama chake cha Republique en Marche (Republic on the Move REM) ambacho amekiasisi miezi 14 tu iliopita kinahitaji kuwa na wingi wa viti katika Bunge la Taifa ili kuweza kupitisha mageuzi aliyoahidi wakati wa kampeni yake.
Uchunguzi wa maoni mara kadhaa umeonyesha kwamba chama cha Macron ambacho hakikuwahi kujaribiwa kinaweza kujinyakulia asilimia 30 ya kura katika duru ya kwanza na kukiweka katika njia ya kunyakuwa ushindi wa kishindo katika duru ya pili Ijumapili ijayo.
Chama cha sera za mrengo wa kati kulia cha Republicans na kile cha Socialist vinahofia kushindwa vibaya baada ya wagombea wao kushindwa kufikia ngazi ya marudio ya uchaguzi wa rais kwa mara ya kwanza katika historia ya Ufaransa baada ya kipindi cha vita.
REM yatabiriwa kupata wingi wa viti
Frankreich Wahlen Nationalversammlung Emmanuel Macron (Reuters/P. Wojazer)
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akisalimiana na watu.
Baadhi ya utabiri unaashiria kwamba chama cha REM kinaweza kushinda kama viti 400 katika bunge hilo lenye viti 477 kutokana na azma ya wapiga kura kutaka kumpa rais huyo mpya mamlaka yenye nguvu.
Chama hicho tayari kinaongoza katika majimbo ya uchaguzi 19 kati ya 11 ya himaya za Ufaransa nchi za nje ambayo yamefanya duru yao ya kwanza ya uchaguzi mwishoni mwa juma lililopita.
Hapo Jumapili Macron baada ya kusalimana kwa kupeana mikono na watu waliomtakia heri na kupiga nao picha za simu ya mkononi alipiga kura yake katika mji wa kitalii wa kaskazini wa Le Touqet ambapo yeye na mke wake mwenye umri wa mika 64 Brigitte wana nyumba yao.
Usalama waimarishwa
Frankreich Wahlen Nationalversammlung (Getty Images/AFP/F. Tanneau)
Zoezi la kupiga kura ya bunge.
Wabunge wachache wanatazamiwa kuchaguliwa katika duru ya kwanza.Iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50,wagomea wawili wa juu wanaongoza wataingia duru ya pili sawa na mgombea aliyejikusanyia angalau asilimia 12.5 ya wapiga kura waliojiandikisha.
Vituo vya kupiga kura katika miji mkubwa vitakuwa wazi hadii saa mbili usiku ambao matokeo ya awali yataanza kutolewa muda mfupi baada ya hapo.
Kufikia mchana asilmia 19.24 miongoni mwa wapiga kura milioni 47 wanaostahili kupiga kura ilikuwa imejitokeza ikiwa ni chini kwa asilimia 21.06 katika wakati kama huo wakati wa uchaguzi wa bunge mwaka 2012.
Zaidi ya polisi 50,000 walikuwa katika doria katika nchi ambayo bado iko katika wasi wasi baada ya wimbi la mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi kuuwa zaidi ya watu 230 tokea mwaka 2015.
Katika tuko la hivi karibuni kabisa Mualgeria aliyejipandikiza itikadi kali mwenye umri wa miaka 40 alipigwa risasi na kujeruhiwa baada ya kumshambula polisi na nyundo nje ya kanisa la Notre Dame mjini Paris.

11 WAUAWA HUKU WAFUNGWA WAPATAO ELFU MOJA WAKITOROKA JELA KONGO DR

Watu wasiopungua 11 wameuawa huku wafungwa 930 wakitoroka jela wakati watu wenye silaha wasiojulikana walipovamia jela moja iliyoko kwenye mji wa Beni, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini Julien Paluku ametangaza kupitia taarifa kuwa katika uvamizi huo uliotokea jana, washambuliaji hao walitumia silaha nzito nzito na kuwaua walinzi wanane wa jela hiyo.
Shambulio hilo la jana ni la nne kwa akali la utorokaji jela kutokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita, likionyesha ni jinsi gani hali ya ukosefu wa usalama ilivyoongezeka nchini humo tangu Rais Joseph Kabila alipokataa kungátuka madarakani baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika mwezi Desemba mwaka jana.

Rais Joseph Kabila 

Teddy Kataliko, ambaye ni mwanaharakati katika mkoa wa Kivu Kaskazini amesema haijaweza kufahamika ni nani hasa waliofanya shambulio hilo la kuvamia jela kwa sababu wanamgambo wengi wanaojihami kwa silaha ambao wanajulikana kama Mai Mai wanaendesha harakati zao katika mji wa Beni.
Kwa mujibu wa Polisi, wafungwa wapatao 4,000 walitoroka jela mwezi uliopita katika jela yenye ulinzi na usalama wa hali juu iliyoko kwenye mji mkuu wa Kongo DR, Kinshasa ambapo kundi la watu wanaopigania kujitenga lilihusishwa na hujuma hiyo. Wafungwa wengine wasiopungua watatu walitoroka katika jela nyengine ya mjini Kinshasa siku ya Jumamosi iliyopita.../

Friday, June 9, 2017

MBUNGE MAREKANI: HUJUMA ZA KIGAIDI TEHRAN NI STRATEJIA YA TRUMP

Mbunge katika chama tawala cha Republican nchini Marekani amesema hujuma za hivi karibuni za kundi la kigaidi la ISIS mjini Tehran inaweza kuwa stratijia ya Rais Donald Trump.
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Dana Rohrabacher, ambaye anawakilisha California katika Bunge la Kongresi, ametoa matamshi hayo katika kikao cha Alhamisi cha Kamati ya Sera za Kigeni ya Kongresi ambayo ilikuwa ikijadili kuhusu Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Dana Rohrabacher ambaye alionekana kuunga mkono hujuma za kigaidi za Jumatano dhidi ya watu wa Iran alisema kundi la kigaidi lililotekeleza hujuma hiyo linapaswa kuchochewa zaidi kuishambulia Iran.
Ikumbukwe kuwa siku ya Jumatano, timu ya magaidi wa Daesh (ISIS) walishambulia Haram ya Imam Khomeini MA na eneo la Bunge la Iran mjini Tehran na kuwaua shahidi watu 17 huku wengine karibu 50 wakijeruhiwa. Magaidi watano waliotekeleza hujuma hiyo waliangamizwa na maafisa wa usalama huku wahusika wengine 41 wakikamatwa katika maeneo mbali mbali ya Iran.
Gaidi wa ISIS akiwamiminia raia risasi katika ukumbi wa wageni wa jengo la idara ya Bunge la Iran
Mbunge huyo mwenye misimamo mikali wa chama cha Republican amesema iwapo stratijia ya Trump ni kuchochea hujuma za kigaidi Iran basi anaunga mkono jambo hilo. Amesema anaunga mkono Marekani kushirikiana na ISIS katika vita dhidi ya Iran na kutoa mfano wa namna Marekani ilivyoshirikiana na Joseph Stalin, aliyemtaja kuwa muovu, katika kumuangusha Adolf Hitler katika Ujerumani ya Wanazi.
Ifahamike kuwa kundi la ISIS lilianzishwa miaka kadhaa iliyopita kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Kiarabu hasa Saudi Arabia. Kundi hilo limetenda jinai za kuogofya katika nchi kadhaa hasa Iraq na Syria lakini katika miezi ya hivi karibuni limeanza kupata pigo na kupoteza ardhi ambazo lilikuwa limeziteka katika nchi hizo mbili.

MAY ATAKA KUUNDA SERIKALI NA DEMOCRATIC UNIONIST

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema atabakia madarakani na kuunda serikali,  baada ya uchaguzi mkuu hapo jana ambapo chama chake cha Conservative kilipoteza wingi wake bungeni.

London Theresa May (picture-alliance/empics/J. Brady)
Waziri Mkuu May alielezea uamuzi wake wa kuunda serikali licha ya chama cha Conservative kutokuwa na wingi bungeni, katika taarifa yake kwa waandishi habari nje ya makao yake makuu ya Nambari 10 mtaa wa Downing mjini London, na baada ya kuonana na Malkia Elizabeth kwenye kasri la Buckingham na kumuomba ampe nafasi ya kuunda serikali mpya.
May ameahidi kushirikiana na wale aliowaita marafiki na washirika na hasa katika Chama cha  Democratic Unionist (DUP), ambacho ndicho kikubwa kabisa katika Ireland ya Kaskazini na kinaweza kumpa May uungaji mkono wa kutosha kuweza kutawala.
"Vyama vyetu hivi viwili vimekuwa na uhusiano imara kwa miaka mingi na nina matumaini kuwa tutaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi ya Uingereza," alisema May. 
DUP kinachotetea jimbo hilo libakie kuwa sehemu ya Uingereza na chenye msimamo wa kihafidhina panapohusika masuala ya kijamii, kimeongeza idadi yake ya viti kufikia 10. Chama cha Conservative kimepata viti 318 , Labour 261, Scotish Nationalist (SNP) 35 na Liberal Democrats viti 12.
May ajipanga upya kwa Brexit
London Labour Führer Jeremy Corbyn (Getty Images/C. Furlong)
Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn, ambaye chama chake kimeongeza viti bungeni licha ya kushindwa kupata wingi wa kutosha kuunda serikali.
Akizungumzia majadiliano ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, mchakato unaojulikana kama Brexit, yatakayoanza tarehe 19 mwezi huu, Waziri Mkuu huyo aliyeitisha uchaguzi wa mapema kwa lengo la kujipa nguvu za kusimama imara kwenye mazungumzo hayo alisema serikali yake mpya itaiongoza nchi kupitia mazungumzo muhimu kwa kutekeleza "maamuzi ya umma wa Uingereza kwa kuitoa kwenye Umoja wa Ulaya".
"Nitafanya kazi kuiweka nchi yetu katika hali ya usalama kwa kutekeleza malengo niliyoyaweka baada ya  mashambulizi ya Manchester na London," amesisitiza May.
Mapema leo chama cha DUP kilikataa kutamka lolote kuhusiana na ripoti kwamba kimekubali kukiunga mkono chama tawala cha Waziri Mkuu May, ingawa kilikubali kuwa tayari mazungumzo baina yao yameanza.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaashiria huenda serikali ya May isidumu muda mrefu na wanafikiri kuna uwezekano wa kuitishwa uchaguzi mwengine. 
Kivutio kikubwa katika uchaguzi wa safari hii kuwania viti 650 ni kuchaguliwa kwa idadi kubwa ya wanawake kuliko wakati mwengine wowote, ambapo jumla ya wabunge wanawake 207 wamechaguliwa ikilinganishwa na 196 katika uchaguzi wa 2015. 

WATU 39 WAUAWA KATIKA MASHAMBULIO YA MABOMU YA MAGAIDI WA DAESH IRAQ

Kwa akali watu 39 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya mabomu yaliyofanywa hii leo na kundi la kigaidi la Daesh katika miji ya Babil na Karbala nchini Iraq.
Vyombo vya usalama vya Iraq vimetangaza kuwa, watu wasiopungua 30 wameuawa katika shambulio la kwanza katika mji wa Babil ambapo mtu aliyekuwa amejifunga mabomu alijiripua katikati ya watu. Taarifa zaidi zinasema kuwa, watu 33 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la kujitolea muhanga huku hali za baadhi ya majeruhi zikiripotiwa kuwa mbaya.
Mlipuko huo ulitokea katika mlango wa kuingia katika soko la eneo la al-Musayyib na kwamba, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya wahanga wa shambulio hilo la kigaidi. Taarifa za awali zinasema, mwanamke mmoja ndiye aliyetekeleza shambulio hilo kwa kujiripua katika mji huo ambao wakazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.


Wanachama wa kundi la kigaidi al Daesh nchini Iraq

Aidha katika tukio jengine watu wengine 9 wanaripotiwa kufariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya mtu mmoja kujiripua ndani ya kituo cha mabasi ya mji wa Karbala.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetangaza kuwa, wanachama wake ndio waliohusika na mashambulio ya leo ya kigaidi nchini Iraq.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, raia 354 wameuawa nchini Iraq na wengine 470 kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yaliyofanywa na makundi ya kigaidi.

MOHAMMADI- GOLPAYEGANI: MAADUI HAWAWEZI KULIKATISHA TAMAA TAIFA LA IRAN KWA KUFANYA MAUAJI

Mkuu wa ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatua ya maadui ya kufanya mauaji katu haiwezi kulikatisha tamaa taifa la Iran.
Hujjatul Islam Walmuslmiin Muhammad Muhammadi-Golpayegani, amebainisha kuwa, sababu ya mashambulio ya juzi ya kigaidi hapa mjini Tehran ni safari ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini Saudi Arabia.
Akizungumza katika shughuli ya kuiaga miili ya mashahidi wa mashambulio ya kigaidi ya siku ya Jumatano hapa mjini Tehran, mkuu wa ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, katika safari ya hivi karibuni ya Trump nchini Saudia kuliratibiwa mipango ya kutoa pigo dhidi ya Iran.
Muhammad Muhammadi Golpeygani, Mkuu wa ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Aidha Hujjal Islam Walmuslimiin Muhammad Muhammadi Golpeygani alisoma ujumbe wa rambirambi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika siku chache zilizopita mjini Tehran akisisitiza kuwa, jinai hiyo haiwezi kutia doa katika irada na azma ya taifa la Iran.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuaga miili mitoharifu ya mashahidi wa mashambulio hayo ya kigaidi, Ali Larijani, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mashambulio hayo ya kigaidi yameonyesha jinsi magaidi walivyojikita zaidi katika kulenga mhimili mkuu wa mfumo wa utawala wa kidini nchini Iran wenye ridhaa ya wananchi.

Thursday, June 8, 2017

UN: WAPIGANAJI WA DAESH WANAWAUA WATOTOWANAO KIMBIA VITA MOSUL

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wanawapiga risasi watoto wanaokimbia vita na mapigano katika mji wa Mosul huko kaskazini mwa Iraq.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuwa, mauaji yanayofanywa na kundi la Daesh dhidi ya raia wanaokimbia mapigano katika mji wa Mosul yamekifikia kiwango cha kutia wasiwasi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, katika siku chache zilizopita tu raia 231 waliokuwa wakikimbia mapigano huko Mosul wameuawa kwa kupigwa risasi na wapiganaji wa Daesh.
Daesh inaua watoto wa Iraq 
Taarifa ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pia imesema mauaji ya raia yanayosababishwa na mashambulizi ya anga yanatia wasiwasi. Mashambulizi hayo yanafanywa na Marekani na washirika wake.
Wakati huo huo mjumbe wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Iraq amesema kuwa inakadiriwa kuwa, zaidi ya Wairaq laki moja wanasumbuliwa na hali mbaya kupita kiasi katika mji wa Mosul. 
Raia wanaokimbia vita Mosul
Jeshi la Iraq linaendeleza operesheni ya kukomboa mji huo kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi la Daesh. Operesheni hiyo ilianza tarehe 19 Februari mwaka huu.  

MAWAHABI WADHANIWA KUFANYA MASHAMBILIZI YA KIGAIDI MJINI TEHRANI, IRAN

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, magaidi waliofanya mashambulizi jana Jumatano hapa Tehran wametambuliwa. Imesema, magaidi hao walikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na magenge ya Kiwahabi nje ya Iran.
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imesema hayo leo katika taarifa yake maalumu na kuongeza kuwa, timu ya magaidi hao wa Daesh (ISIS) ambao jana walishambulia Haram ya Imam Khomeini MA na eneo la Bunge la Iran walikuwa ni magaidi watano ambao wana historia ya vitendo vya uhalifu na walikuwa wanachama wa magenge ya Kiwahabi ya wakufurishaji.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, baada ya kujiunga na genge la kigaidi la Daesh, magaidi hao walishiriki kwenye jinai za genge hilo huko Mosul, kaskazini mwa Iraq na Raqqah, kaskazini mwa Syria. 
Operesheni ya kupambana na magaidi wa Daesh katika majengo ya Bunge mjini Tehran, Jumatano, Juni 8, 2017

Taarifa ya Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imeongeza kuwa, katika msimu wa joto wa mwaka jana, magaidi hao waliingia nchini Iran wakiongozwa na Abu Ayesheh, mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa magaidi wa Daesh kwa lengo la kufanya mashambulio kadhaa ya kigaidi katika miji ya kidini ya Iran. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran walisambaratisha kikamilifu kundi hilo ikiwa ni pamoja na kumwangamiza Abu Ayesheh. Baadhi ya magaidi wa timu hiyo walifanikiwa kutoroka wakiwemo magaidi hao watano waliofanya mashambulizi ya kigaidi jana Jumatano hapa mjini Tehran.
Magaidi hao walioangamizwa jana mjini Tehran wametambuliwa kwa majina ya: Seriyas, Fereydoun, Qayyoum, Abu Jahad na Ramin. Jana Jumatano tarehe 8 Juni 2017, mji wa Tehran ulishuhudia mashambulizi mawili ya kigaidi katika Haram ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na jengo la kiidara la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran). 

Wednesday, June 7, 2017

MAPIGANO BUNGENI IRAN

kundi linalojiita Dola la Kiislamu limedai kuhusika na mashambulizi mawili yaliyoteka kwa mfululizo leo hii mjini Tehran, Iran ambayo yanatajwa kusababisha vifo vya hadi watu saba na kuwajeruhi wengine kadhaa.

[No title] (Ilna)
Kundi linajiita Dola la Kiislamu limedai kuhusika na mashambulizi mawili yaliyoteka kwa mfululizo leo hii mjini Tehran, Iran ambayo yanatajwa kusababisha vifo vya hadi watu saba na kuwajeruhi wengine kadhaa. 
Washambuliaji kadhaa wamelishambulia bunge la Iran na mtu alijitoa muhanga alilenga eneo la kaburi la mwanzilishi wa mapinduzi ya Iran hayati Ayatollah Ruhollah Khomeini na kusababisha kifo cha mlinzi na kujeruhi watu wengine 12 katika kile kinachotajwa kuwa mashambulizi ya nadra kutokea. Hayo yanafanyika wakati mizizimo ya risasi ikiendelea katika jengo la bunge.
Kundi la linalojiita dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na mashambulizi hayo kupitia mtandao wake wa habari wa AMAQ. Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA-tukio hilo lisilo la kawaida lililotokea katika mji mkuu wa Iran, Tehran, limesababisha Wizara ya Ulinzi kuitisha mkutano wa usalama wa  dharura. Vyombo vya habari nchini humo vinasema helikopta za polisi zinazunguka jengo la bunge na kwamba mawasiliano ya simu zote za mkononi kwa walio ndani ya jengo hilo yamekatwa.
Sakata katika eneo la  bunge
Iran Angriff auf das Parlament in Teheran (Reuters/TIMA)
Askari wakiwa katika doria katika eneo la bunge
Nalo shirika la habari la ISNA linasema milango yote ya kuingilia na kutoka imefungwa na wabunge na waandishi wa habari ambao walikuwemo katika jengo hilo wakati vikao vikiendelea wameamriwa kutulia katika eneo maalumu. Lakini Televisheni ya serikali baadae ilisema waashambuliaji wanne wanahusika katika shambulizi la bungeni, na kwamba watu wanane wamejeruhiwa. Televisheni hiyo ilimnukuu mbunge mmoja Elias Hazrati aliyesema washambuliaji hao walikuwa wamejihami kwa bunduki aina ya Kalashnov.
Vilevile televisheni hiyo ilisema mlinzi aliuwawa na watu wengine wanne wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la kwenye eneo la kaburi la Khomeini. Mmoja ya washambuliaji aliuliwa na mlinzi na kuna mwanamke aliyetiwa mbaroni. Chombo hicho kiliwaelezea washambuliaji katika eneo la kaburi kama "magaidi" na kuongeza kuwa mmoja alifanya shambulizi la kujitoa muhanga pasipo kutoa ufafanuzi zaidi.
Pamoja na shambulizi katika eneo la kaburi la Khomeini hatari lakini kaburi la kiongozi huyo limekuwa alama muhimu kwa taifa hilo. Kama kiongozi wa kwanza wa Iran, Khomeini alikuwa kuongozi muhimu wa taiifa hilo na alikuwa kiongozi wa kimapinduzi ya mwaka 1979.
Afisa mwanadamizi ambaye hakutaka kutaja jina lake ameilezea hali kuwa mbaya na kuyataja mashambulizi hayo kuwa pigo kwa rais wa nchi hiyo Hassan Rouhani, akihoji inakuwaje bunge lenye ulinzi mkali likashambuliwa.
Rouhani alisalia madarakani baada ya ushindi wa kishindo dhidi ya mgombea mwenye msimamo mkali wa kihafidhina na vikosi vya ulinzi wa Jamhuri, ambavyo ndiyo vyenye nguvu zaidi nchini Iran. Televisheni ya Iran imesema bunge limerejea shughuli zake na kuonyesha picha za kile ilichosema ni kikao cha ufunguzi kikiendelea kama kawaida.

HASIRA ZA ISRAEL BAADA YA UMOJA WA MATAIFA KUUNGA MKONO KUUNDWA NCHI HURU YA PALESTINA

Danny Danon Balozi wa Utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa amekosoa vikali matamshi ya katibu mkuu wa umoja huo Antonio Gutterres ambaye ameunga mkono uundwaji nchi huru ya Palestina.
Dannon amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kujizuia kueneza kile alichodai kuwa ni urongo na kuangazia uhalisia wa mambo katika eneo.
Mjumbe huyo wa utawala wa Kizayuni amedai kuwa ni kichekesho kutuhumiwa kwa ugaidi utawala pekee wa kidemokrasia katika eneo.
Madai hayo ya Dannon kuwa eti utawala wa Kizayuni wa Israel ndio "utawala pekee wa kidemokrasia" Mashariki ya Kati na jitihada za utawala huo za kupotosha ukweli katika eneo hili zinajiri wakati ambao utawala huo umezidisha sera zake za uvamizi na utumiaji mabavu katika eneo. Hivi sasa utawala haramu wa Israel unatambulika kimataifa katika dhihirisho la ukaliaji mabavu, mienendo iliyo dhidi ya binadamu na ubaguzi. Sera hizo za Israel zimezua radiamali za kimataifa.
Kuhusiana na hilo Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumanne alitaka kuundwe nchi huru ya Palestina na kusema hilo limekuwa takwa la walimwengu kwa muda wa miaka 70 sasa.
Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na Israel
Guterres alikuwa akizungumza kwa munasaba wa mwaka wa 50 wa maafa ya 1967 ya kukaliwa kwa mabavu ardhi zaidi za Palestina. Katika taarifa aliyotoa kwa munasaba huo, Gutteres ameitaka Israel ihitimishe ukaliaji wake wa mabavu wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds Mashariki na Miinuko ya Golan.
Aidha amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina na Wazayuni inapaswa kutatuliwa kwa msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
Utawala wa Kizayuni umekasirishwa na kauli ya Guterres katika hali ambayo ukatili wa utawala huo ghasibu umesajiliwa katika nyaraka za Umoja wa Mataifa na walimwengu hawatasahau ukatili huo wa Wazayuni.
Utawala wa Kizayuni ni utawala haramu ambao unaungwa mkono na madola ya Magharibi na uliasisiwa mwaka 1948 kwa lengo la kutekeleza sera za kigaidi dhidi ya Wapalestina na kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina ikiwa ni pamoja na Quds Tukufu. Kwa hivyo tokea kuasisiwa kwake, utawala huo umekuwa ni utawala wa shari na vamizi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika fremu hiyo katika vita vya mwaka 1967, utawala wa Kizayuni katika vita vyake na nchi za Kiarabu ulikalia kwa mabavu ardhi zaidi za Palestina ikiwa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na sehemu ya Baitul Maqqdis na sehemu ya ardhi za nchi za Kiarabu ikiwa ni pamoja na Miinuko ya Golan ya Syria. Kwa hivyo utambulisho wa kivita wa utawala huo uko wazi kwa walimwengu.
Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Israel
Utawala huo umekuwa ukijaribu kubadilisha fikra za walimwengu kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya taasisi za kimataifa.
Maazimio kadhaa ya taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel hasa kulaani sera za ukaliaji mabavu za utawala huo ni jambo linaloonyesha kuwa jamii ya kimataifa haikubali sera za kujitanua za utawala huo.
Matukio ya kimataifa yanaonyesha jamii ya kimataifa haiwezi kustahamili tena kushuhudia jinai za utawala huo wa Kizayuni ambao ni utawala haramu na ambao unapata himaya ya nchi za Magharibi.
Maazimio mbali mbali ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na azimio 242 na 338 yamebainisha wazi kuwa utawala wa Kizayuni unapaswa kuondoka katika ardhi unaozikalia kwa mabavu.
Katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa harakati za kimataifa za kuunga mkono haki za watu wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuinua hadhi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa.
Aghalabu ya nchi za dunia zinaunga mkono kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu na kuna uwezekano kuwa mwaka huu wa 2017 nchi huru ya Palestina itaundwa
Mchakato huu umeutia wasi wasi utawala haramu wa Israel na ndio sababu wakuu wa utawala huo wameanza kutoa matamshi dhidi ya Umoja wa Mataifa kutokana na sisitizo la umoja huo kuhusu ulazima wa utawala huo wa Kizayuni kusitisha ukaliaji mabavu ili taifa huru la Palestina liundwe.

MAGAIDI WASHAMBULIA BUNGE LA IRAN NA HARAM YA IMAM KHOMEINI

Watu wawili akiwemo afisa wa usalama wameripotiwa kuuawa huku watu wengine wanane wakijeruhiwa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia majengo ya Bunge la Iran na Haram ya Imam Khomeini MA, katika mji mkuu Tehran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, watu wanne waliokuwa wamejizatiti kwa bunduki za AK47 na bunduki moja ndogo wamefyatua risasi ovyo wakilenga walinzi wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ambapo mlinzi mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Hata hivyo shirika la habari la ISNA limenukuu mbunge mmoja wa Tehran, Elias Hazrati  akisema kuwa hali hiyo imedhibitiwa na mvamizi mmoja ametiwa mbaroni.
Haram ya Imam Khomeini MA
Wakati huohuo, shirika la habari la Fars limeripoti kuwa, mtu mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya watu watatu waliobeba silaha kuvamia Haram ya Imam Khomeini MA, viungani mwa Tehran. Mmoja wa wavamizi hao ameuawa na maafisa usalama, mwingine ambaye anasemekana kuwa mwanamke amejiripua huku wa tatu akijeruhiwa na kukamatwa na vyombo vya usalama.
Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, fulana lililosheheni mada za miripuko la wavamizi hao katika Haram ya Imam Khomeini MA limepatikana na kuharibiwa.
Genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo ya leo jijini Tehran.

Sunday, June 4, 2017

MFALME WA MOROCCO AKOSA KUHUDHURIA MKUTANO WA ECOWAS KWA AJILI YA NETANYAHU

Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco amekosa kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) unaofanyika leo nchini Liberia kwa kuwa unahudhuriwa na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Awali mfalme huyo alikuwa amekubali mwaliko wa kushiriki kongamano hilo lakini alipofahamishwa kuwa litahudhuriwa na Netanyahu, akatangaza kughairi msimamo huo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imesema Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco amefuta uamuzi wake wa kuhudhuria kikao hicho cha kikanda kwa kuwa kinafanyika chini ya mazingira ya taharuki, mikwaruzano na mkanganyo.
Baadhi ya viongozi wa nchi wanachama wa ECOWAS
Ifahamike kuwa Morocco sawa na nchi nyingi za Kiarabu haina uhusiano wa kidiplomiasia na utawala haramu wa Israel.
Nchi 15 wanachama wa ECOWAS zinahudhuria kongamano hilo eti la kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Israel, zikiwemo Mali na Niger ambazo pia hazina uhusiano wa kidiplomasia na Tel Aviv.
Licha ya kuwa nchi nyingi za Kiarabu zimetangaza kutokuwa na uhusiano na utawala pandikizi wa Israel, lakini duru za habari zinaashiria kuwa aghalabu yazo zina uhusiano wa kisiri na Tel Aviv.

RAIS WA SUDAN: UGAIDI HAUNA MAFUNGAMANO YOYOTE NA UISLAMU

Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan amesema mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni katika nchi jirani ya Misri sawa na hujuma nyingine za kigaidi katika sehemu mbali mbali duniani hazina uhusiano wala mafungamano yoyote na dini ya Kiislamu.
Akihutubu hapo jana katika dhifa ya futari iliyoandaliwa na Wakristo wa Kikhufti mjini Khartoum, Bashir sambamba na kulaani hujuma za hivi karibuni dhidi ya Wakristo nchini Misri amesema harakati za kigaidi popote pale hazina ufahamu wowote kuhusu dini ya wanadamu. 
Rais wa Sudan amenukuliwa na shirika rasmi la habari la nchi hiyo SUNA akisema kuwa, mashambulizi hayo hayakuwa dhidi ya Wakristo wa Kikhufti tu, bali jamii yote ya Wamisri huku akitoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa hujuma hizo. 
Ijumaa iliyopita, watu wasiopungua 28 waliuawa nchini Misri na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi dhidi ya mabasi mawili yaliyokuwa yamewabeba Wakristo wa Kibti kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Cairo.
Moja ya mabasi yaliyoshambuliwa na magaidi wa Daesh nchini Misri hivi karibuni
Kadhalika mwezi Aprili mwaka huu miripuko ya kigaidi katika makanisa mawili ya mji wa Tanta katikati ya mkoa wa al-Gharbiyah na mjini Alexandria nchini humo yalisababisha watu karibu 50 kuuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Mashambulizi mengi ya kigaidi ya miaka ya hivi karibuni nchini Misri yamekuwa yakifanywa na kundi la Ansar Bait al-Muqaddas lililotangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh, na kisha kubadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.