Shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty
International, limesema mwaka 2016 ulikuwa mwaka mbaya katika suala zima
la haki za binaadamu, huku uhalifu wa kivita ukiwa umefanywa duniani
kote.
Ripoti mpya ya mwaka ya Amnesty International iliyotolewa jana mjini
Paris, Ufaransa inaeleza jinsi 2016 ulivyokuwa mgumu na wenye huzuni,
ambapo habari mbaya zilikuwa haziishi, kuanzia matokeo ya kushangaza ya
uchaguzi na kura ya maoni, hadi kwenye mashambulizi ya kigaidi yasiyo na
idadi, kuongezeka kwa wakimbizi na mizozo mikubwa kama vile Syria,
Yemen na Sudan Kusini. Pia inaeleza jinsi wakimbizi wanavyohujumiwa,
huku mataifa yenye nguvu duniani yakishindwa kukabiliana na changamoto
hiyo.
Katibu Mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty amesema
mwaka 2016 ulikuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika rekodi za haki
za binaadamu. Shetty amesema ukweli ni kwamba mwaka wa 2017 unaanza huku
kukiwa na hofu na bila ya kuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake.
Amesema ripoti hiyo imebainisha kuwa moja ya tatizo kubwa la mwaka 2016,
lilikuwa ni kuongezeka kwa matamshi ya chuki kwenye maeneo mengi ya
Ulaya na Marekani na kuongezeka kwa hofu zaidi hadi kufikia kiwango
ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu miaka ya 1930.
Waasi wa Sudan Kusini
''Ulikuwa
mwaka ambao sumu ya ubaguzi wa kisiasa ya ''sisi dhidi ya wao''
ilishika kasi duniani kote. Tulishuhudia kuongezeka siasa za woga na
chuki. Wanasiasa duniani walizigawa jamii, waliwahujumu wachache,
wahamiaji na wakimbizi. Na matokeo ya haya yote yanasababisha ukiukwaji
wa haki za binaadamu,'' amesema Shetty
Ripoti hiyo ya mwaka
imehusisha utafiti kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu kwenye
nchi 159, ambapo 23 kati ya hizo pia zilihusika na uhalifu wa kivita,
ikiwemo Sudan Kusini, Myanmar na Ufilipino. Shetty anasema cha
kushangaza miongoni mwa nchi 159 zilizokiuka haki za binaadamu, ziko
zile ambazo zinaongoza kupigia debe demokrasia kama vile Ufaransa,
Uingereza na Marekani.
Trump ashutumiwa kuhusu wakimbizi
Ripoti
ya Amnesty International imemshutumu Rais wa Marekani, Donald Trump
pamoja na viongozi wengine wa dunia wakiwemo wa Hungary, Uturuki na
Ufilipino, katika kile ilichosema kuwatumia vibaya wakimbizi kwa maslahi
yao kisiasa, badala ya kutafuta kiini kilichosababisha wakimbizi hao
wayakimbie mataifa yao.
Mkurugenzi anayeshughulikia mizozo Amnesty International, Tirana Hassan
Mkurugenzi
wa kushughulikia mizozo wa Amnesty International, Tirana Hassan amesema
sio kweli kwamba eneo moja la dunia limekuwa bora au limefanya vibaya
zaidi ya jingine, bali mwaka 2016 umekuwa ni mwaka uliokiuka haki za
binaadamu duniani kote, hali inayopaswa kukomeshwa mara moja.
Hassan
ameiambia DW kwamba kilicho hatari zaidi lugha ya ''sisi dhidi ya wao''
ambayo imepata umaarufu mkubwa imechochea kuongezeka kwa siasa kali za
kizalendo, huku mbinu kama hizo zikiwa zinawalenga zaidi wakimbizi na
wahamiaji. Hassan amesema mwaka 2017 utakuwa ni mwaka wa kutoa wito kwa
jumuiya ya kimataifa, serikali na wanasiasa kuchukua hatua na kuanza
kuziweka mbele haki za binaadamu.
Hata hivyo, ripoti hiyo imesema
kuwa mwaka 2017 uwe wa kupigania haki za binaadamu kwani maeneo ya
mapambano yako kila sehemu na kila mmoja anaweza kuwa mwanaharakati wa
haki za binaadamu. Aidha, shirika la Amnesty International limesema watu
ambao tayari wanapigania kuzilinda haki za binaadamu, wanahitaji
kuungwa mkono.
No comments:
Post a Comment