Hali ya maisha katika akthari ya nchi za
Kiafrika, imesababisha kuongezeka idadi ya wakimbizi katika bara la
Afrika. Hii ni katika hali ambayo, Mpango wa Chakula Duniani (WPF)
umetahadharisha kuhusu matatizo ya chakula kwa wakimbizi wa bara hilo.
Kwa mujibu wa indhari iliyotolewa
na WFP, takribani wakimbizi milioni mbili katika nchi 10 barani Afrika
wanakabiliwa na matatizo yaliyosababishwa na uhaba wa chakula, suala
ambalo limepelekea kuzuka hali mbaya katika afya ya jamii. Kwa mujibu wa
tangazo la asasi hiyo ya kimataifa, idadi ya wakimbizi barani Afrika
iliongezeka mwaka 2016 na kufikia milioni tano, ikilinganishwa na
wakimbizi milioni 2 na laki sita mwaka 2011. Hii ni katika hali ambayo,
licha ya kuongezeka vyanzo vya fedha, lakini misaada ya chakula
imepungua na haitoshi kukidhi mahitaji ya chakula ya wakimbizi hao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgao wa
misaada ya chakula katika nchi kumi za Kiafrika zikiwemo za Kenya,
Cameroon, Chad, Mauritania, Sudan Kusini na Uganda umepungua hadi
kufikia asilimia 50.
Nchi nyingi za Kiafrika kwa sasa zinakabiliwa na matatizo ya kiuchumi
na mizozo ya kisiasa. Mazingira magumu ya kiuchumi, ukosefu wa ajira
na umasikini umetanda katika nchi hizo jambo ambalo limepelekea akthari
ya raia wa nchi mbalimbali barani Afrika hususan vijana wahajiri
kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta kazi na kuwa na kipato cha
kujikimu kimaisha.
Kupita kwenye njia zenye hatari kubwa
katika mipaka ya Libya na kusafiri kupitia bahari ya Mediterania kila
siku kumewafanya wahajiri wengi wapoteze maisha.
Hata hivyo mwenendo wa juhudi za
wahajiri hao ungali unaendelea. Mwenendo huo umezifanya nchi za Ulaya
zitiliane saini makubaliano na baadhi ya nchi za Kiafrika kwa ajili ya
kuzuia wahajiri hao kuingia barani humo. Katika uwanja huo, makubaliano
yaliyotiwa saini hadi sasa bado hayajatekelezwa kivitendo. Harakati za
makundi ya kigaidi na kuibuka suala la ukosefu wa usalama na amani ni
tatizo jingine linalowakabili wahajiri hao.
Akthari ya maeneo ya Nigeria
yanayoshuhudia harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram yamewafanya
raia wengi kuwa wakimbizi kutokana na kukosekana amani na usalama katika
maeneo yao na hivyo kuomba hifadhi katika maeneo salama au kukimbilia
nje ya nchi. Hii ni katika hali ambayo, wengi wa wahajiri hao hivi sasa
wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na uhaba mkubwa wa chakula.
Katika upande mwingine, uhamaji huo wa watu umesababisha madhara
katika sekta ya kilimo; na kusimama kilimo na kutopandwa mazao
kumepelekea kujitokeza uhaba wa chakula kiasi kwamba, ardhi nyingi za
kilimo katika maeneo hayo zimekauka.
Vita vya ndani na vya kieneo ni
changamoto nyingine ya eneo hilo. Katika nchi changa zaidi barani Afrika
ya Sudan Kusini vita vinaendelea kushuhudiwa katika hali ambayo, njaa
inayakabili maeneo mengi ya nchi hiyo. Takwimu zinaonyesha kuwa, watu
milioni moja na laki nne wanakabiliwa na hatari ya kifo katika nchi za
Nigeria, Somalia na Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja
wa Mataifa UNICEF, ukame katika nchi ya Somalia umewafanya watoto laki
moja na 85 elfu wakabiliwe na janga la njaa. Aidha idadi hiyo
inatarajiwa kuongezeka zaidi na kufikia watoto laki mbili na 70 elfu
katika miezi ya usoni. Majimui ya mazingira haya yamewafanya wahajiri
wanaotafuta chakula, sio tu wasamahe na kuacha mali na vitu vyao bali
wengi wao wajikute wakiangukia mikononi mwa magenge ya magendo ya
binadamu huku wanawake wakikumbana na vitendo vya kubakwa.
Aidha akthari ya watoto walioangukia mikononi mwa magenge hayo ya
magendo ya binaadamu wameuzwa kama bidhaa. Utabiri unaonyesha juu ya
kuendelea ukame katika akthari ya maeneo hayo ya bara la Afrika. Katika
upande mwingine mazingira mabaya ya kisiasa, vita na mashambulio ya
kigaidi nayo yanaendelea kushuhudiwa katika akthari ya nchi hizo. Katika
mazingira kama haya, ni azma na irada pekee ya jamii ya kimataifa
sambamba na kuongezwa harakati za asasi na jumuiya za kieneo kwa ajili
ya kudhamini mahitaji ya chakula na vile vile kupigwa jeki juhudi za
kuhitimisha vita na migogoro katika akthari ya nchi hizo ndio
itakayoweza kuzuia vifo vya mamilioni ya watu barani Afrika.
No comments:
Post a Comment