Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema mfungamano
wa kijeshi wa NATO ni muhimu kwa Marekani pia. Merkel ameyatamka hayo
kwenye mkutano juu ya maswala ya usalama unaoendelea mjini Munich.
Kansela Angela Merkel amesema kwamba hatari kama ile inayotokana na
magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu IS haiwezi kuzuiwa na nchi moja peke
yake, na kwa hivyo ametoa mwito wa kujengwa mfumo wa pamoja duniani ili
kuikabili hatari hiyo. Kiongozi wa Ujerumani pia aliwaambia wajumbe
kwenye mkutano wa mjini Munich kwamba pana ulazima wa kuboresha na
kuoanisha mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Ulaya. Bibi Merkel
amesema kuwa taasisi hizo ni muhimu sana na ndio sababu pamoja na mambo
mengine ameusisitiza msimamo thabiti wa Umoja wa Ulaya katika jumuiya ya
ulinzi ya NATO. Merkel ameahidi kwamba Ujerumani itajitahidi ili
kulifikia lengo lililowekwa la kuchangia asilimia mbili ya pato jumla la
nchi yake kwa ajili ya bajeti ya ulinzi ya jumuiya ya NATO. Hata hivyo
kansela Merkel amekumbusha kwamba jumuiya hiyo ni muhimu sio tu kwa
Ulaya bali pia kwa Marekani vilevile.
Hotuba ya kansela wa
Ujerumani Angela Merkel ilifuatiwa na ile ya makamu wa rais wa Marekani
Mike Pence aliyewahakikishia washirika wa barani Ulaya kwamba Marekani
itaendelea kusimama nao kwa uthabiti katika jumuiya ya NATO. Hata hivyo
makamu wa rais wa Marekani Mike Pence amezitaka nchi wanachama wa
jumuiya hiyo pia zitoe mchango wao kwa haki. Bwana Pence amesema wakati
sasa umefika wa kuchukua hatua zaidi ili kupambana na changamoto za
kijeshi mbalimbali zilizopo sasa duniani.
Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence
Makamu
wa rais wa Marekani ameeleza kwamba ukiiondoa Marekani na nchi nyingine
nne tu wanachama wa NATO hakuna nchi nyingine iliyolifikia lengo la
kuchangia asilimia mbili ya pato jumla la taifa kwa ajili ya bajeti ya
NATO. Bwana Pence amesema kwamba nchi yake sasa inapanga kuwa na nguvu
kubwa zaidi za kijeshi kuliko hapo awali.
Changamoto zinazoikabili NATO
Pamoja
na changamoto zinazoikabili NATO makamu wa rais wa Marekani Mike Pence
ameitaja hali ya mashariki mwa Ulaya ambapo amesema Urusi inajaribu
kuibadilisha mipaka ya kimataifa. Bwana Pence ameeleza kwamba nchi yake
itaendelea kuilaumu Urusi lakini wakati huo huo itajaribu kutafuta
maslahi ya pamoja.
Msimamo wa Marekani juu ya NATO ulitiliwa
mashaka na rais Donald Trump aliyesema kwamba jumuiya hiyo imeshapitwa
na wakati ingawa katika siku za hivi karibuni zimetolewa kauli za kuwapa
uhakika washirika wa barani Ulaya. Baada ya hotuba yake makamu wa rais
wa Marekani Mike Pence alikutana kwa faragha na kansela wa Ujerumani
Angela Merkel.
Wakati huo huo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
Antonio Guterres, katibu mkuu wa NATO Jen Stoltenberg na waziri wa mambo
ya nje wa Urusi Sergei Lavrov wanatarajiwa kutoa hotuba kwenye mkutano
huo wa mjini Munich.
Kwa mujibu wa habari leo alasiri wapinzani
wa mkutano huo wa mjini Munich wanatarajia kufanya maandamano ambapo
watu hadi 4000 wanatazamiwa kushiriki. Mkutano huo wa mjini Munich
unahudhuriwa na wanadiplomasia pamoja na wadau wa maswala ya usalama
kutoka nchi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment