Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatafakari kutoa
amri mpya ya kuwapiga marufuku raia wa baadhi za nchi kuizuru Marekani
baada ya amri yake ya awali kuhusu hilo kupingwa na mahakama ya juu.
Mnamo tarehe 27 mwezi uliopita, Trump aliagiza raia wa Libya, Iraq,
Iran, Somalia, Sudan, Syria na Yemen kupigwa marufuku kuingia Marekani
kwasababu za kiusalama.
Katika mazunguzo na wanahabari ambayo
hayakutarajiwa akiwa katika ndege ya jeshi la angani la Marekani Ijumaa
jioni, Trump ametangaza uwezekano wa kutoa amri mpya ifikapo Jumatatu au
Jumanne wiki ijayo. Hata hivyo hajatoa maelezo ya kina kuhusu marufuku
hiyo mpya.
Alikuwa akielekea katika makaazi yake yaliyoko jimbo
la Florida akiwa na Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe. Wazo la Trump la
kutoa amri nyingine ya rais kuhusiana na suala la kuwapiga marufuku raia
wa nchi za Kiislamu linakuja baada ya mahakama kuu ya rufaa iliyoko San
Franciso kutoa uamuzi wa kupinga amri ya raia ya kuwazuia raia kutoka
nchi hizo saba.
Amri mpya huenda ikawapa wakosoaji wa Trump
ushindi kwa kuhoji kuwa alilazimika kubadilisha msiamo wake kuhusu sera
yake kuu kama rais. Licha ya tangazo hilo la Trump, utawala wake huenda
bado ukapinga uamuzi wa mahakama ya rufaa wa kuzuia marufuku hiyo dhidi
ya wageni.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais wa Marekani Donald Trump
Marufuku
hiyo ya awali ambayo Trump alidai lengo ni kuepusha mashambulizi ya
kigaidi, ilisababisha mtafaruku mkubwa na kupelekea shutuma kali kutoka
nchi zilizolengwa, nchi za magharibi na mashirika makubwa ya kibiashara
ya Marekani hasa ya sekta ya teknolojia.
Jaji wa mahakama ya
Seattle alisitisha agizo la kuwapiga marufuku wasafiri na wahamiaji
kutoka nchi hizo saba na siku ya Ijumma wiki iliyopita, agizo hilo la
mahakama lilithibitishwa na mahakama ya rufaa ya San Francisco na
kusababisha kiongozi mpya wa Marekani kuandika maneno makali katika
ukurasa wake wa Twitter akishutumu majaji na idara ya mahakama.
Maamuzi
hayo ya mahakama yanaibua maswali kuhusu hatua ijayo ya Trump. Afisa wa
ikulu ya rais aliye na ufahamu kuhusu mipango ya Trump amesema iwapo
amri mpya itatolewa itahusisha mchango wa msaidizi wa Ikulu ya rais,
Stephen Miller, ambaye alihusika katika amri ya awali pamoja na maafisa
kutoka baraza la kitaifa la usalama, wizara ya sheria na ile ya usalama
wa ndani.
Haijabainika ni kwa kiasi gani amri mpya ya rais
itakavyoathiri kesi zilizowasilishwa mahakamani na walioathirika na amri
ya awali. Hata hivyo kuna uwezekano amri mpya ya rais ikakumbwa na
changamoto za kisheria na wanaoipinga wakaiomba mahakama kuwaruhusu
kuyafanyia mageuzi malalamishi yao mahakamani.
No comments:
Post a Comment