Mwaka mpya wa 2017 umeanza leo sambamba na
shambulizi lililofanyika katika klabalu moja ya starehe mjini Istanbul
huko Uturuki na kuua watu karibu 40 na kujeruhiwa makumi ya wengine.
Tukio hilo ni ishara kwamba mwaka mpya wa 2017 huwenda ukatawaliwa na machafuko na umwagaji damu zaidi ya miaka iliyopita.
Ugaidi ambao katika miaka hii ya sasa umekuwa zimwi kubwa
linalovuruga usingizi na usalama wa walimwengu kutokana na kupuuzwa
vyanzo na sababu zake halisi na vilevile kutumiwa vibaya na baadhi ya
nchi kwa malengo ya kisiasa, sasa umepanua mbawa zake katika maeneo
mbalimbali ya dunia. Inaonekana zimwi hilo la ugaidi litatafuna idadi
kubwa zaidi ya wanadamu katika mwaka huu wa 2017 na kuenea katika maeneo
mengine ya dunia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kushindwa mtawalia
kundi la Daesh na magaidi wengine katika nchi za Syria na Iraq
kumewafanya wanachama wa makundi hayo warejee katika nchi zao huko
Ulaya, Marekani na kaskazini mwa Afrika, suala ambalo ni hatari kubwa
kwa maisha ya watu, usalama na amani ya nchi hizo.
Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, ugaidi sio changamoto kubwa pekee
inayoikabili dunia katika mwaka huu mpya wa 2017. Hitilafu za kisiasa
kati ya nchi zenye taathira katika mfumo wa kimataifa zinaweza kuyafanya
maisha ya mamilioni ya wanadamu kuwa yenye mashaka makubwa. Kwa mfano
tu tunaweza kuashiria hitilafu zilizopo baina ya rais mteule wa
Marekani, Donald Trump na nchi za Ulaya kuhusu makubaliano ya hali ya
hewa ya Paris. Hii ni kwa sababu, iwapo Trump ataiondoa Marekani katika
makubaliano hayo ya Paris kama alivyoahidi, basi hapana shaka kwamba,
ulimwengu utakabiliwa na uchafuzi mkubwa zaidi wa mazingira na wakati
huo mabadiliko ya hali ya hewa yatakuwa na taathira kubwa zaidi kwa
maisha ya wanadamu.
Katika upande mwingine kuchaguliwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani
kumezidisha wasiwasi kuhusu ushindani wa kibiashara kati ya madola
mkubwa kiuchumi duniani. Iwapo Marekani na China zitazidisha ushindani
mpana juu ya masuala ya kibiashara, basi uchumi dhaifu wa dunia
utakumbwa na mashinikizo zaidi na hatimaye wahasirika wakubwa watakuwa
nchi dhaifu na mamilioni ya watu katika pembe mbalimbali za duniani.
Vilevile utekelezaji unaotarajiwa kuanza mwaka huu wa uamuzi wa
Waingereza wa kujiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya umezidisha
wasiwasi kuhusu masuala ya kiuchumi na kifedha. Zaidi ni kwamba, iwapo
mirengo ya kisiasa yenye mitazamo sawa na ile ya waungaji mkono wa
Brexit (waungaji mkono wa hatua ya kuijiondoa Uingereza katika Umoja wa
Ulaya) itashinda uchaguzi wa mwaka huu nchini Ufaransa, basi kuna uwezo
mkubwa kwamba mwaka 2017 unaweza kuwa mwaka wa mgawanyiko na
kusambaratika Umoja wa Ulaya.
Tukiachilia mbali wasiwasi uliopo kuhusu hitilafu kubwa za kisiasa na
migogoro ya kiuchumi na kiusalama inayoikabili dunia katika mwaka huu
wa 2017, kupasishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
katika siku ya mwisho ya mwaka 2016 linalounga mkono usitishaji vita
nchini Syria ni hatua inayotia matumaini ambayo imeonesha kuwa, migogoro
mikubwa inaweza kutatuliwa kwa njia ya ushirikiano.wa kimataifa.
Mgogoro huo ulianza kutokana na uingiliaji wa madola magharibi na baadhi
ya nchi za Kiarabu katika masuala ya ndani ya Syria na uungaji mkono wa
nchi hizo kwa makundi ya kigaidi. Miongoni mwa changamoto kubwa zaidi
za sasa duniani ni jinsi ya kurejesha amani na utulivu. Changamoto
nyingine ni jinsi ya kulinda matunda ya azimio la aina yake la Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limepiga marufuku ujenzi wa
vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.
Kwa vyovyote vile, japokuwa mwaka huu wa 2017 umeanza kwa shambulizi la kigaidi la Istanbul, lakini iwapo jamii ya kimataifa itakuwa na irada na azma kubwa ya kukabiliana na vyanzo na sababu kuu za ugaidi, machafuko na migogoro wa kisiasa na kiuchumi, basi yumkini katika mwaka huu huu wa 2017 dunia ikashuhudia mabadili mengi chanya na yenye matunda kwa mwanadamu.
No comments:
Post a Comment