Umoja wa Afrika umesema nchi za Afrika ziko
tayari kupokea wakimbizi baada ya Marekani kupasisha sheria tata ya
kibaguzi dhidi ya wakimbizi.
Akizungumza pambizoni mwa mkutano wa AU unaomalizika leo mjini
Addis Ababa, Ethiopia, Smail Chergui, Kamishna Mkuu wa Masuala ya Amani
na Usalama wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, bara la Afrika linafaa kuwa
mfano mzuri wa kuigwa duniani kwa kuendelea kuwapokea wakimbizi na
wahamiaji, baada ya Marekani kutangaza kuwa itafunga mipaka yake kuzuia
wakimbizi na wahamiaji kuingia nchini humo.
Ameongeza kuwa, historia inaonyesha kuwa nchi za Kiafrika
zimekuwa zikiwapokea wakimbizi kwa moyo mkunjufu huku akitoa mfano wa
Kenya, ambayo ina kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Dadaab.
Chergui amesema vikosi vya kieneo vinapigana kufa kupona kuyatokomeza
makundi ya kigaidi kama al-Shabaab na Boko Haram, hivyo haingii akilini
Marekani kutangaza kuwafungia nje wakimbizi kwa kisingizio cha
kupambana na ugaidi.
Smail Chergui, Kamishna Mkuu wa Masuala ya Amani na Usalama wa Umoja
wa Afrika amesema kuwa, Marekani inafaa kutilia maanani wajibu wake wa
kimataifa inapochukua uamuzi wowote wa kibaguzi na ambao
unaweza kuhatarisha zaidi maisha ya wakimbizi.
Mwenyekiti anayeondoka wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosazana
Dlamini-Zuma hapo jana alikosoa mikakati ya kibaguzi inayochukuliwa na
serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa kisingizio cha kupambana
na ugaidi.
No comments:
Post a Comment