Umoja wa Ulaya umekaribisha makubaliano ya
amani baina ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wapinzani
wa nchi hiyo.
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya,
na Neven Mimica, Kamishna wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa na
Maendeleo cha umoja huo, sanjari na kukaribisha kutiwa saini makubaliano
hayo ya kisiasa baina ya pande mbili nchini Kongo DR, wameonyesha pia
matumaini kwamba mapatano hayo yatapelekea kupatikana amani na usalama
wa kudumu nchini.
Naye Jean-Marc Ayrault, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema,
makubaliano kati ya serikali ya Kinshasa na wapinzani ni mwanzo wa
kuikwamua nchi hiyo kutokana na mgogoro wa kisiasa. Serikali na
wapinzani wa nchi hiyo walifikia makubaliano hayo chini ya uangalizi wa
maaskofu wa Kanisa Katoliki.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Rais Joseph Kabila ataendelea kuwa
rais hadi mwishoni mwa mwaka huu. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, utawala wa rais huyo ulifikia tamati tarehe 19
mwezi Disemba uliopita.
No comments:
Post a Comment