Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia tarehe 31
mwezi Disemba mwaka jana alieleza kuwa magaidi elfu tatu raia wa Tunisia
wametapakaa katika pembe mbalimbali za dunia khususan huko Iraq, Syria
na Libya.
Beji Caid Essebsi aliongeza kuwa baadhi ya ripoti zinasema
kuna jumla ya magaidi elfu kumi wa Tunisia lakini takwimu hizo si sahihi
na kuwa magaidi raia wa Tunisia walioko Iraq, Syria, Libya, Yemen na
Afrika idadi yao ni 2926.
Tunisia ni nchi pekee ya Kiarabu ambayo imeweza kuvuka kwa
mafanikio kipindi cha mpito baada ya mageuzi na mapinduzi ya wananchi
mwaka 2011. Kwa kutambua hali ya mambo na uzoefu wa migogoro ya Misri,
Libya na Yemen, vyama, makundi ya kisiasa na shakhsia wa Tunisia
waliweza kuvuka kipindi cha mpito kwa maafa na hasara za kiwango cha
chini. Katika kipindi cha miaka sita ya hivi karibuni, Tunisia
haikukabiliwa na vitisho vingi vya usalama ikilinganishwa na nchi tatu
za Libya, Yemen na Misri na tishio kuu zaidi ambalo limekuwa likiitatiza
nchi hiyo ni matatizo ya kiuchumi. Pamoja na hayo imejikuta ikihusika
bila ya kutaka na machafuko na migogoro inayozikabili nchi nyingine za
Kiarabu na raia wengi wa nchi hiyo hususan tabaka la vijana wamejiunga
na makundi ya kigaidi katika nchi za Syria, Iraq, Libya na Yemen. Kwa
sasa makundi ya kigaidi yamedhoofika sana hususan huko Syria na Iraq,
na uwezekano wa kurejea nchini karibu magaidi elfu tatu raia wa Tunisia
limegeuka na kuwa changamoto kubwa ya kiusalama kwa nchi hiyo.
Baadhi ya vyama vya siasa nchini Tunisia kikiwemo chama cha Nidaa
Tounes cha Rais Beji Caid Essebsi vinaamini kuwa, kurejea nchini magaidi
hao ni tishio kubwa kwa usalama wa Tunisia. Chama cha Nidaa Tounes
kinapinga suala la kurejea nchini magaidi hao. Hata hivyo baadhi ya
wanachama wa chama cha An Nahdha katika Bunge la taifa wanaamini kuwa,
magaidi ambao ni raia wa Tunisia wana haki ya kurudi nchini kwa sababu
wao ni raia wa nchi hiyo. Wakati huo huo wananchi wa Tunisia wamekuwa
wakifanya maandamano na kutangaza upinzani wao dhidi ya suala la kurejea
nchini magaidi hao.
Licha ya baadhi ya wanachama wa chama cha Nidaa Tounes kupinga jambo
hilo, lakini Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia ametangaza rasmi kuwa,
haiwezekani kuwazuia magaidi hao kurejea nyumbani kwa mujibu wa katiba
ya nchi hiyo. Essebsi amesema kuwa iwapo wananchi wote watapinga suala
la kurejea magaidi nchini, basi katiba itafanyiwa marekebebisho.
Msimamo huo rasmi wa Rais wa Tunisia unaonyesha kuwa, magaidi
waliotajwa hatimaye watarejea nchini humo. Kurejea magaidi hao kunaweza
kuharibu matunda ya mapinduzi ya nchi hiyo ya mwaka 2011 na kuzidisha
pia tisho la ugaidi kwenye orodha ndefu ya matatizo ya kiuchumi na
kiusalama ya Tunisia.
No comments:
Post a Comment