Maafisa usalama nchini Nigeria wamewafyatulia
mabomu ya kutoa machozi wafuasi wa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya
nchi hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anaendelea kuzuiliwa kinyume
cha sheria.
Shirika la habari la Press TV limeripoti kuwa, mamia ya wafuasi
wa Sheikh Zakzaky hapo jana walifyatuliwa mabomu ya kutoa machozi
walipokuwa wakishiriki maandamano ya amani ya kuonyesha uungaji mkono
wao kwa kiongozi wao, nje ya bunge la nchi hiyo katika mji mkuu Abuja.
Maafisa wa polisi wa Nigeria waliyavunja maandamano hayo ya amani kwa
mabomu ya machozi, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa. Waandamanaji hao
ambao walikuwa wamebeba picha za Zakzaky na maberamu yenye ujumbe
unaosema, "Muachieni huru Zakzaky" walisikika wakiikosoa vikali serikali
ya Abuja kwa kuendelea kumzuilia Sheikh Zakzaky licha ya agizo la
mahakama.
Itakumbukwa kuwa Mahakama ya Shirikisho la Nigeria hivi karibuni
ilitoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini serikali
ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo inavunja waziwazi amri hiyo ya
mahakama kwa kukataa kumwachilia huru kiongozi huyo wa Harakati ya
Kiislamu.
Umoja wa Ulaya na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty
International ni baadhi ya taasisi za kimataifa zilizotoa taarifa
zikiwataka viongozi wa Nigeria kuheshimu amri ya mahakama ya kumwachilia
huru mara moja kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment