Adama Barrow ameapishwa na kuwa Rais mpya wa
Gambia huku Yahya Jammeh aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 22
aking'ang'ania madaraka ya nchi.
Baadhi ya duru zinasema kuwa Barrow ameapishwa leo kuwa rais
mpya na wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi wako tayari kuingilia
kati. Sherehe za kuapishwa Adama Barrow zimefanyika nje ya nchi katika
ubalozi wa Gambia nchini Senegal.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mawaziri na viongozi mbalimbali wa
serikali ya Rais Jammeh wameendelea kujiuzulu na hivyo kuzidi
kumdhoofisha kiongozi huyo mwenye nia ya kung'ang'ania madaraka.
Makamu wa rais nchini Gambia Isatou Njie-Saidy amejiuzulu saa chache
kabla ya muda wake wa kuongoza kutimia. Asidha Waziri wa Mazingira na
Elimu ya Juu pia amejiuzulu, ikiwa ni msururu wa mawaziri kumtoroka
Jammeh kufuatia hatua yake ya kukataa kujiuzulu baada ya zaidi ya miongo
miwili ya utawala.
Wakati huo huo, majeshi ya mataifa ya magharibi mwa Afrika
yanatarajiwa kuingia nchini Gambia leo ili kuhimiza uhamisho wa mamlaka.
Baadhi ya ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa, vikosi vya
Senegal tayari vimeingia nchini Gambia.
Katika upande mwingine Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
lilitazamiwa kufanya mkutano wa dharura hii leo kuhusiana na mgogoro wa
kisiasa na kunukia machafuko ya umwagikaji damu nchini Gambia.
Rais Yahya Jammeh ambaye alikuwa amekubali kushindwa na Adama Barrow
katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Desemba na hata kumpongeza
mpinzani wake huyo, ghafla alibadilisha uamuzi na kuyakataa matokeo kwa
madai kuwa zoezi la uchaguzi lilitawaliwa na dosari nyingi na sasa
anataka uchaguzi wa rais ufanyike tena.
No comments:
Post a Comment